Monday, November 2, 2015

Ikulu Yakanusha Kikwete Kutopokea Simu Ya Maalim Seif Shariff Hamad

Wakati saa 48 zilizotolewa na mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kutaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar zikiwa zimemalizika, Ikulu ya Jamhuri ya Muungano imesema haijapokea maombi ya Maalim Seif kutaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete.

Ijumaa iliyopita, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari visiwani Zanzibar kuwa baada ya ZEC kufuta uchaguzi Jumanne iliyopita, alifanya jitihada kadhaa za kuwasiliana na Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ili kuzungumzia suala hilo kwa maslahi ya Zanzibar lakini wito wake huo umekuwa ukipuuzwa.

Maalim Seif alisema tangu kufutwa kwa uchaguzi, amefanya juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wenzake wa kitaifa akiwamo Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, lakini wote wamekuwa wakimkwepa, licha ya kuanza kuwatafuta kwa kutumia mawasiliano ya simu na ujumbe kupitia wasaidizi wao, akitaka wakutane.

Hata hivyo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa Ikulu imesikitishwa na madai ya Maalim Seif, ikieleza kuwa siyo kweli.

Badala yake, Ikulu imesema haijapokea ombi lolote kutoka kwa Maalim Seif la kutaka kukutana na Rais Kikwete tangu siku ya kupiga kura na hata baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi wa Zanzibar.

Taarifa hiyo ya Ikulu imesema kile ambacho Rais Kikwete amekipokea ni malalamiko ya CUF kuhusu baadhi ya vitendo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi Zanzibar na ombi kwa ajili ya kuwezesha mazungumzo kati ya Maalim Seif na Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange.

“Baada ya hapo, Rais Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuchunguza madai haya ya CUF na kumletea taarifa. Kadhalika, ametoa maelekezo ofisini kwake ya kuwezesha mazungumzo kati ya Jenerali Mwamunyange na maafisa wa CUF,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa Rais Kikwete amekuwa akiguswa na hali ya kisiasa na usalama wa Zanzibar kama ilivyo kwa Watanzania wengine na amekuwa akifanya kazi bila kuchoka huku akipata ushauri wa kina juu ya kilichotokea Zanzibar siku chache zilizopita na kupata ufumbuzi.

Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa wakati jambo hilo likiwa bado katika mikono ya ZEC ambacho ni chombo huru cha uchaguzi, Rais Kikwete yuko tayari kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wake ili kupata suluhisho jema kuhusiana na hali ya Zanzibar.

Uchaguzi  Kufutwa
Suala la kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar linadaiwa kuviingiza visiwa hivyo katika mgogoro wa kikatiba na kisheria.

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitaja sababu tisa za kufikia uamuzi wa kufuta uchaguzi huo kuwa ni pamoja na kura kuongezeka katika baadhi ya majimbo kisiwani Pemba na pia baadhi ya makamishna wa Zec kutanguliza itikadi za vyama hadi kuvua mashati ili kupigana.

Kadhalika, alisema katika baadhi ya vituo, masanduku ya kupigia kura yaliporwa na kwenda kuhesabiwa nje ya vituo, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria ya uchaguzi na pia, kuna taarifa ya kufukuzwa kwa baadhi ya mawakala wa wagombea na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Hata hivyo, waangalizi wa ndani na wa kimataifa, wakiwamo Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Madola  Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), waangalizi wa Marekani na Uingereza, katika ripoti zao wamesema uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu ulikuwa huru na wa haki na kutaka Zec ikamilishe kazi ya kuhesabu kura na kumtangaza mshindi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More