Thursday, November 19, 2015

Vigogo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Waanza Kuhojiwa na Polisi Kwa Kuvuruga Uchaguzi

Vigogo wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), wameanza kuhojiwa na Jeshi la Polisi Zanzibar baada ya kuvurugika kwa Uchaguzi Mkuu na kusababisha Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka huu.

Viongozi waliohojiwa na Polisi  ni Makamishna na Watendaji wa tume hiyo akiwamo Makamu Mwenyekiti, Jaji Abdulhakim Issa Ameir.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi, alithibitisha mjini hapa Mjini jana kuwa Makamishina wa Zec na Watendaji, wameanza kuhojiwa na maofisa wa upelelezi kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar Ziwani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema hadi sasa uchunguzi umefikia hatua kubwa na baada ya kukamilika, majalada ya uchunguzi yatapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim, kabla ya wahusika kufikishwa mahakamani.

“Tunawahoji Makamishna na Watendaji wa Tume, Makamu Mwenyekiti yeye tayari tumemhoji, bado Mwenyekiti na maofisa wengine,” alifafanua DDCI Msangi.

Alisema Polisi waliingia kazini baada ya kuripotiwa kuwa uchaguzi umevurugwa na kazi inayofanyika ni kukusanya ushahidi na vielelezo kabla ya wahusika kufunguliwa mashitaka kwa kuhujumu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Alisema uchunguzi huo umegawanyika sehemu tatu na kuwahusisha Tume, waathirika na wananchi kutoka sehemu mbalimbali katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

Aidha, alisema kuna mambo mazito yameanza kuonekana tangu kuanza kufanyika kwa uchunguzi, lakini alisema ni mapema kueleza uchunguzi huo utachukukua muda gani kukamilika.

"Wahusika watafikishwa mahakamni baada ya majalada ya uchunguzi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar kabla ya kufikishwa mahakamani," alisema Msangi.
Hata hivyo, Naibu Mkurugenzi huyo alisema hali ya Zanzibar ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida tangu Zec ilipofuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

Akitangaza kufuta uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Zec, Jecha alisema kuna sababu tisa zimemfanya kuchukua hatua hiyo.
Alizitaja kuwa ni pamoja na vituo vya wapigakura na idadi ya kura katika visanduku zilikuwa nyingi kuliko idadi ya watu waliosajiliwa katika daftari la wapigakura katika vituo vya uchaguzi.

Aidha, alisema kuna visanduku vya kura viliporwa na kuhesabiwa nje ya vituo kinyume na sheria pamoja na mawakala wa vyama kupigwa na kufukuzwa katika vituo vyao vya kazi siku ya uchaguzi.

Tayari Zec imetangaza rasmi katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu kufutwa kwa uchaguzi huo na kuwataka wananchi kusubiri kutangazwa tarehe ya kurudiwa.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More