Sunday, November 29, 2015

Viongozi Waliojiuzulu Chadema Warejea Tena

Viongozi wa Chadema Mkoa wa Rukwa waliotangaza kujiuzulu nyadhifa zao ndani ya chama hicho hivi karibuni, wamesitisha uamuzi wao na kurejea madarakani.

Mratibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe alisema hayo juzi wakati akizungumza na mwandishi wetu  kwa njia ya simu kutoka mkoani Mbeya.

Mwaisumbe alisema wamekubaliana na viongozi hao kurejea katika nyadhifa zao za kisiasa ndani ya chama hicho.

Alisema kikao baina ya viongozi wa Chadema wa kanda hiyo na waliotangaza kujiuzulu kilidumu kwa zaidi ya saa 11 juzi na kufikia uamuzi wa kurejea madarakani kwa viongozi hao.

Akizungumzia sababu za kujiuzulu kwa viongozi hao ambazo ni kutolipwa fedha mawakala wa wagombea wa chama hicho mkoa na kutoridhishwa na uteuzi wa mgombea ubunge wa viti maalumu, Aida Kenan, alidai zina mashiko lakini kabla ya kutangaza katika vyombo vya habari kuachia ngazi walipaswa kuwasiliana na uongozi wa juu wa chama.

Aliongeza kuwa, mathalan katika suala la mawakala kulikuwa na fomu maalumu ambazo wagombea walizijaza kuonyesha kuwa wanaweza kubeba gharama zote za mchakato wa uchaguzi au la.

Alisema wagombea waliojaza fomu kuonyesha hawana uwezo wa kuwalipa mawakala, chama kilibeba gharama hizo na fedha zilitolewa kwa kila mgombea kwa kuwa wao ndiyo walijua nani ni wakala na fedha hizo hazikupelekwa kwa viongozi wa mkoa kama inavyodaiwa.

Kuhusu uteuzi wa Kenan katika nafasi ya ubunge wa viti maalumu, alisema jina lake lilitokana na maombi ya Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) ambao walikuwa na nafasi mbili, lakini hakutokana na kura ambazo wagombea wa Chadema walipata kwenye Mkoa wa Rukwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa mkoa ambao awali walijiuzulu, Mwenyekiti Zeno Nkoswe na Katibu Ozem Chapita walikiri kukubali kurejea madarakani baada ya kufanya kikao na viongozi wa chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

“Nimeafiki kurejea katika wadhifa wangu wa uenyekiti wa mkoa, lakini bado nawasubiri na viongozi wa kitaifa kuna mambo tuyaweke sawa. Si unajua wao wanatutuhumu kwamba tulikimbilia kwenye vyombo vya habari na sisi tuna hoja zetu,” alisema Nkoswe.

Baada ya makubaliano na viongozi hao walifanya kikao na madiwani waliochaguliwa kupitia chama hicho, ili kuhakikisha wanaongoza Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga. Chadema ina viti 10 kati ya 19 vya udiwani.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More