Tuesday, February 28, 2017

AZANIA GROUP KUWAKILISHA TANZANIA KATIKA MASHINDANO YA A.MASHARIKI YA STANDARD CHARTERED

Timu ya Azania Group, ndiyo itakayowakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda ya Afrika Mashariki, ya Benki ya “Standard Chartered-Road to Anfield” yatakaofanyika uwanja wa Jakaya Kikwete Youth Park Jumamosi, Machi 4. Azania walipata ushindi huo kwa kuichakaza timu ya H&R Consultancy mabao ya 6-5 kwa penati dhidi ya katika mchezo wa kukata na shoka uliofanyika mwishoni mwa wiki na kufanikiwa kuipeperusha bendera ya Tanzania. Kwa maana hiyo, Azania Group wanatarajia kumenyana uso kwa uso na washindi wa michuano hiyo kutoka nchi za Kenya na Uganda. Washindi wa michuano hiyo nchini Uganda ni timu ya Cocacola wakati kidedea wa kombe hilo nchini Kenya ni Radio ya Capital FM.
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (kushoto) na Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa Benki hiyo, Juanita Mramba wakikabidhi kikombe kwa Bw Sikaba Hamisi ambaye ni Nahodha wa timu Azania Group, Mshindi wa kitaifa wa mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017 (Road to Anfield), mashindano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya JK Youth Park, Gerezani jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutwaa ushindi huo, Nahodha wa Azania Group, Bw. Shabaka Hamisi alisema maandalizi yao mazuri ndiyo siri ya ushindi wao na kuongeza kwamba wapo tayari kuwanyoa hao wageni asubuhi kabisa. “Katika jambo lolote kama unataka kufanya vyema, maandalizi mazuri yanasaidia sana. Kwa upande wetu, tulifanya mazoezi yakutosha na ndiyo maana leo tumeibuka washindi.” Alisema. Aliongeza, “Siyo kwamba wenzetu walikua wabovu, ila umakini na utulivu kwa upande wa wachezaji wangu ndiyo kilichotusababishia kupata matokeo mazuri.” Alisema mazoezi ya kujipanga kwa ajili ya mechi tayari yameshaanza kwa ari na nguvu mpya, akiongeza kuwa ushindi kwao ni lazima. Kwa upande wake, Phillip David, nahodha wa H&R Consultancy alisema kukosekana kwa ukosefu wa umakini katika ushambuliaji ndiyo uliosababisha timu yake kupoteza mechi hiyo, hata hivyo alishukuru kwa kuibuka mshindi wa pili wa mashindano hayo.
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (kushoto) na Mkuu wa Mahusiano na Masoko wa Benki hiyo, Juanita Mramba (kulia) wakifurahi katika picha ya pamoja na timu ya Azania Group wakikabidhi kikombe kwa timu Azania Group,Mshindi wa kitaifa wa mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017(Road to Anfield), mashindano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya JK Youth Park,Gerezani jijini Dar es Salaam.
“Kama ulivyoona, mechi ilikuwa moja moja hadi tukaingia kwenye matuta. Wenzetu walipata penati sita wakati sisi tulifunga tano. Nafasi ya kushinda ilikuwa upande wetu lakini Mungu hakupenda iwe ivyo,” alisema. Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Tanzania Limited, Sanjay Rughani aliwaasa wachezaji wa Azania Group kuwa wajiandae kikamilifu ili waubakishe ubingwa nchini Tanzania. “Sisi hakuna zawadi nzuri ambayo tunaitaka kutoka kwenu zaidi ushindi. Fanyeni mazoezi ya kutosha ili Jumamosi inayokuja muweze kushinda mechi zenu zote dhidi ya hizo timu kutoka Kenya na Uganda. Na sisi kama wadhamini tutakua pamoja nanyi ili kuhakikisha kwamba mnapata ushindi hapa nyumbani,” alisema Sanjay. Naye Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa Benki hiyo, Juanita Mramba, aliwapongeza kwa ushindi huo lakini akiwatahadharisha kuwa safari yao ndiyo kwanza imeanza. “Leo mmeshinda mashindano haya, Jumamosi kazi yenu ni kubwa zaidi kwani mtacheza na wageni wawili, hivyo jipangeni vizuri zaidi mkiutumia vyema uwanja wa nyumbani,” alisema. Ukiachia mbali Azania ambao waliondoka na kombe za dhahabu, washindi wa pili H&R Consultancy walijitwalia kombe la shaba, huku washindi wa tatu PWC wakitwaa kombe la Bronze.
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Tanzania Sanjay Rughani (kushoto) akikabidhi kombe kwa Nahodha wa timu ya HR Consultants, Phillip David ambao ni washindi wa pili wa mashindano ya Kombe la Standard Chartered 2017 (Road to Anfield), yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya JK Youth Park, Gerezani jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia tukio hilo ni Mkuu wa Wateja Binafsi wa Benki ya Standard Chartered, Michael Shio (kulia).

KAWAIDA Timu ya Azania Group, ndiyo itakayowakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda ya Afrika Mashariki, ya Benki ya “Standard Chartered-Road to Anfield” yatakaofanyika uwanja wa Jakaya Kikwete Youth Park Jumamosi, Machi 4. Azania walipata ushindi huo kwa kuichakaza timu ya H&R Consultancy mabao ya 6-5 kwa penati dhidi ya katika mchezo wa kukata na shoka uliofanyika mwishoni mwa wiki na kufanikiwa kuipeperusha bendera ya Tanzania. Kwa maana hiyo, Azania Group wanatarajia kumenyana uso kwa uso na washindi wa michuano hiyo kutoka nchi za Kenya na Uganda. Washindi wa michuano hiyo nchini Uganda ni timu ya Cocacola wakati kidedea wa kombe hilo nchini Kenya ni Radio ya Capital FM.

UNESCO KUENDELEA KUSAIDIA REDIO JAMII KUKUZA DEMOKRASIA

Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeahidi kuendelea kuzisaidia redio jamii kwa lengo la kuhakikisha sauti za wanyonge zinapazwa na kusikika ili kukuza demokrasia nchini. Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA), Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues alisema UNESCO alisema kuwa wakati umefika kwa wadau wa sekta ya habari kufikiri kwa kina namna ya kuhabarisha umma kwa kuangalia namna ya uwasilishaji ambapo kwa sasa changamoto kubwa ni kasi ya ukuaji wa teknolojia ya habari na namna ambapo redio zinaweza kushindana na vyombo vingine. Alisema kwa wanahabari wanapaswa kuwa makini na taarifa wazitoazo kwa jamii kwani kumekuwa na mazoea ya baadhi yao kuripoti habari bila kufanya uchuinguzi wa kina huku wakitumia chanzo kimoja cha habari badala ya kujiuliza maswali mengi ili kupata taarifa sahihi.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Habari wa UNESCO, Ofisi za Tanzania, Christophe Legay akizungumza machache wakati wa mkutano mkuu wa wajumbe wa Bodi ya Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA) unaoendelea katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
Aliwashauri wanachama wa COMNETA, wawe na umoja, mshikamano na kupendana ili kuepuka migogoro inayoweza kuyumbisha ustawi wa mtandao huo. “Ninawaomba sana, COMNETA, muwe mfano wa kuigwa kwa kuepuka migongano ya wenyewe kwa wenyewe ikiwamo kugombea madaraka ili kuwa umoja wa mfano kwa katika tasnia ya vyombo vya habari hapa nchini’.
‘Vipindi mbalimbali vya kuhamasisha maendeleo vinavyorushwa na redio hii vimesaidia sana kuhamasisha wananchi na sasa mwamko wa maendeleo umekuwa mkubwa hapo Micheweni” alisema Zulmira Rodrigues
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya COMNETA, Mohamed Tibanyendera akizungumza na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari jamii waliokutana kwenye mkutano mkuu ili kujadili changamoto na kufanya uchaguzi wa viongozi wapya uliodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania-COMNETA, Prosper Kwigize alisema kuwa ipo changamoto kwa baadhi ya maafisa habari mikoani na wilayani kuleta urasimu mkubwa katika utoaji wa taarifa zinazohitajika kwa waandishi wa habari hivyo kukwamisha upatikanaji wa habri kwa umma. Pia kuna changamoto mbalimbali kwenye chama hicho hivyo ni vyema kuzitafutia suluhiso la msingi ili mtandao huwe imara.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya COMNETA, Mohamed Tibanyendera alisema kuwa kwa siku za nyuma redio ilikuwa ni chombo cha kuaminika katika utoaji wa habari hivyo kujijengea umaarufu na kuaminika zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna upotoshaji mkubwa. Pia aliweza kuyatolea majibu maswali yaliyoulizwa na wajumbe wa bodi ya COMNETA ili kuimarisha uwajibikaji katika Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania-COMNETA.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA), Prosper Kwigize akizungumza na viongozi wa vyombo vya habari jamii wakati wa mkutano mkuu wa COMNETA unaondelea katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya COMNETA, Balozi Christopher Liundi akizungumza jambo wakati wa mkutano mkuu Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA) unaofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam chini ya udhamini wa UNESCO.
Katibu wa Bodi ya Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania (COMNETA), Marco Mipawa akisoma marejesho kwenye mkutano mkuu unaondelea OUT jijini Dar es Salaam. Pichani juu na chini ni Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya COMNETA ambao pia ni Mameneja na wawakilishi wa vituo vya redio jamii nchini wakishiriki kutoa maoni kwenye mkutano mkuu wa COMNETA unaoendelea katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
Kutoka kushoto ni Afisa Programu wa Mawasiliano na Habari wa UNESCO, Nancy Kaizilege na Mkufunzi wa Redio Jamii UNESCO, Rose Haji Mwalimu wakirekodi mambo muhimu katika mkutano mkuu wa COMNETA unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Mkutano ukiendelea.

ZOOMTANZANIA.COM YATANGAZA AFISA MTENDAJI MKUU MPYA

Bi Mili Rughani, gwiji katika anga la teknolojia Afrika, akabidhiwa kijiti cha uongozi wa tovuti namba moja ya matangazo Tanzania, ZoomTanzania.com, katika kuendeleza safari ya mafanikio. Miaka ya hivi karibuni imekuwa ya kusisimua sana kwa hii kampuni ya dot-com ya Kitanzania. Mnamo Septemba 2014, Ringier Afrika ilichukuwa asilimia kubwa ya umiliki wa kampuni ya Zoom Tanzania. 



Hii iliwezesha upatikanaji wa rasilimali na utaalamu unaohitajika zaidi ili kukua zaidi. Kisha mwaka 2016, ZoomTanzania.com ilikuwa jiwe kuu la msingi katika muungano wa Ringier Africa na One Africa Media, na kufanikisha kuundwa kwa kundi linaloongoza kwa matangazo ya mtandaoni barani Afrika - Ringier One Africa Media (ROAM). "Imekuwa ni safari ya kusisimua sana," alisema Kirk Gillis, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa ZoomTanzania. "Miaka michache iliyopita Zoom ilikuwa na wafanyakazi wanne, katika ofisi ndogo ikiwa na ndoto kubwa huku ikiangaika kuweza kufanya malipo ya wafanyakazi."


 Leo hii, ZoomTanzania ni tovuti namba moja ya matangazo nchini Tanzania na ina wafanyakazi 35 wengi wao wakiwa ni vijana wachapakazi mahodari, wenye vipaji na wataalamu wakuendesha hili gurudumu la matangazo ya mtandaoni kisasa zaidi. ZoomTanzania imeshuhudia ukuaji na utendaji mkubwa na wenye kuvutia sana. Kwa mujibu wa wataalamu wa Google, 

ZoomTanzania inapata zaidi ya watumiaji 1,000,000 na watumiaji wapya karibu 350,000 kila mwezi. Zoom pia inajivunia kuwa na watumiaji waliosajiliwa zaidi ya 225,000, na tovuti inazalisha maulizo zaidi ya 135,000 kati wanunuzi na wauzaji kila mwezi! Uamuzi wa kujiuzulu kutoka Zoom Tanzania ulikuwa ni mgumu sana kwa Mr Gillis. 


"Muungano wa ROAM ulitengeneza fursa muafaka kwangu kujitoa Zoom na kujikita katika biashara zangu nyingine, lakini nilihitaji kumpata Kiongozi mwenye nguvu, mjasiriamali, na mwenye uwezo mkubwa wakidigitali ili aiongoze Zoom iweze kufikia uwezo wake kamili." Akiwa mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 15 ya kiutendaji katika sekta ya usimamizi wa masoko ya kitigitali na IT barani Afrika, Bi Rughani ana kila sifa ya kuchukuwa wasifu huu. Anakuja ZoomTanzania.com akitokea Microsoft makao ya Kenya, ambapo alisimamia Ufumbuzi wa biashara ndogo na za kati ( Small and Medium Business (SMB) solutions) kwa ajili ya nchi 10 za Afrika ikiwemo Tanzania. "Ninaiacha Zoom katika mikono salama na yenye uwezo mkubwa na ni imani yangu kampuni itanufaika sana na mtazamo mpya na safi wa Milli," alisema Gillis. 


 "Nafurahishwa zaidi kwa sababu yeye ni Mtanzania." ZoomTanzania.com ilitengenezwa na Watanzania, kwa ajili ya Watanzania, na sasa Mtanzania ataiongoza ZoomTanzania kuelekea mafanikio zaidi Bi Rughani alianza ZoomTanzania Januari 2017, na mipango ya makabidhiano ya uongozi inakwenda vizuri sana. "Hii ilikuwa nafasi ya kusisimua sana kwangu," alisema Bi Rughani. 

 "Nina imani kubwa katika ukuaji wa soko la mtandaoni Tanzania, na ZoomTanzania.com ina nafasi kubwa sana kuchangia kwenye ukuaji huu." Wakati Bi Rughani akizidi kusimamia kazi za kila siku, Bw Gillis bado yupo hadi Machi mwaka 2017 akisimamia uzinduzi wa tovuti mpya na iliyoboreshwa zaidi. 


Uzinduzi wa tovuti mpya ya ZoomTanzaniainatarajiwa kuongeza kasi ya tovuti na kuwarahishishia watumiaji, ikiwa ni pamoja na mfumo mpya wa matangazo ili kuongeza ufanisi katika kuwakutanisha wauzaji na wanunuzi. "Jiandaeni kupokea mambo makubwa na mazuri "Mr Gillis na Bi Rughani," katika miezi ijayo utaona mfululizo wa vitu vipya vitakavyoongeza ufanisi kwa wauzaji kuonyesha bidhaa na huduma zao kwa Watanzania kwa ujumla."

BOHARI YA DAWA (MSD) YAPIGA HATUA KUWEZESHA UZALISHAJI DAWA KWA NJIA YA UBIA NA SEKTA BINAFSI (PPP)

 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bwana, Laurean Bwanakunu (kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri  ya Mji wa Kibaha Bi.Jenifa Omolo wakibadilishana hati baada ya kusaini makubaliano ya umilikishwaji wa eneo la ardhi, lenye ukubwa wa mita za mraba 400,000 Dar es Salaam leo, ambayo itatumika kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kuzalishia dawa na vifaa tiba Kibaha mkoani Pwani.

Monday, February 27, 2017

SAMANI ZA NDANI ZAMNG’ARISHA JACQUELINE NTUYABALIWE KWENYE FORBES

KATIKATI ya foleni katika jiji la Dar es Salaam ndani ya gari nyeupe aina ya Mercedes S550, Jacqueline Ntuyabaliwe, mrembo wa miaka 38, macho yake yalikuwa yametulia katika simu yake ya mkononi. Alikuwa akiangalia seti ya samani za eneo la kulia chakula. Kwa bashasha, baada ya muda kidogo anatanua picha hiyo kisha ananisogezea simu yake ya mkononi kunionesha picha anayoiangalia.

 “Hii ni moja ya samani tulizonazo,” anasema huku akinionesha seti hiyo ambayo imetengenezwa na Molocaho by Amorette, kampuni ya kutengeneza samani aliyoianzisha hivi karibuni. 

“Samani hizi zimetengenezwa kutokana na mbao zilizotwaliwa kutoka katika mashua za zamani za mizigo kwenye fukwe za Tanzania upande wa bahari ya Hindi,” anasema mjasiriamali huyo. Samani hizo za eneo la kulia chakula (Dining Table) anasema zimeagizwa na familia moja iliyopo Ulaya ambayo siku za karibuni ilitembelea duka lake (showroom) Dar es Salaam wakati wakiwa likizo na kwamba anajiandaa sasa kuisafirisha seti hiyo ya samani kwa wateja wake wapya wa Ulaya. 
Lakini kwanza alichokuwa anakifanya kwa siku ile ni kwenda kiwandani kuangalia seti hiyo ya samani kwa mara ya mwisho kabla ya kusafirishwa ili kujihakikishia kwamba imemaliziwa urembeshaji kwa namna inavyotakiwa kuwa.
Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi.
Jacqueline Ntuyabaliwe, anayetaka umaridadi uliokamilika, ni binti ambaye huangalia vitu vidogo vidogo kuona kama vipo sawa katika hali inayokubalika viwe. Pamoja na kuwa na ratiba yenye changamoto sana (Yeye ni Balozi wa WildAid na yumo ndani ya bodi kadhaa; mama wa watoto pacha wavulana; mke kwa mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa na akiendesha taasisi ya hisani ya elimu), Ntuyabaliwe huhakikisha anakagua kila samani inayozalishwa kiwandani kwake kabla ya kuuzwa au kusafirishwa. “Napenda kitu bora chenye uhakika!” anasema mlimbwende huyo wa zamani wa Tanzania ambaye pia ni mwanamuziki. “Kila kitu tunachokifanya Molocaho lazima kiwe chenye uhakika hakina makosa wala dhaifu, lazima kiwe kimetulia,” anasema mrembo huyo. “Tunashindana na watu maarufu duniani wanaofanya vyema kwa hiyo kama sisi tusipofanya vyema kuliko wao tutashindwa,” aliongeza.
The Crown Chair by Molocaho
Ntuyabaliwe, mzaliwa wa Tanzania, aliyefunzwa kubuni uzuri wa ndani, ni mwanzilishi na mbunifu mkuu wa Molocaho by Amorette, kampuni ya Tanzania inayojishughulisha na utengenezaji wa samani bora kwa namna mteja anavyohitaji, samani, nyuzi, taa, urembaji, samani za nje na kwenye bustani. Molocaho inatengeneza samani zenye mahadhi ya kiafrika ikichanganya utamaduni wa Tanzania katika mazingira ya kisasa na kumalizia na ubunifu wa kimataifa. Molocaho, moja ya makampuni ya Afrika Mashariki ya samani yanayokua kwa kasi, imejipatia nafasi kubwa ya heshima kwa kuhakikisha kwamba inatumia mali ghafi na mbao njema pekee za Tanzania kutengeneza samani zenye kwenda kimataifa. “Mpango wetu mkubwa ni kujenga nembo ya biashara ya samani za Tanzania inayotambulika kimataifa. Ni dhahiri itatuchukua muda kufikia huko , lakini tumedhamiria,” alisema wakati tukizunguka naye katika duka kubwa la maonesho la Molocaho lililopo eneo la Masaki jijini Dar es Salaam. Ntuyabaliwe ni mojawapo ya watu wanaotambulika kirahisi kabisa nchini Tanzania. Mwaka 2000 alishinda taji la urembo la Miss Tanzania na kuiwakilisha Tanzania katika shindano la ulimbwende la dunia ( Miss World). Baada ya muda alipata heshima ya kuwa mmoja wa wanamuziki mahiri na kuweza kutoa nyimbo kadhaa zilizoshika chati Afrika Mashariki. Pamoja na kuwa mlimbwende na mwanamuziki anasema mapenzi yake makubwa ni ubunifu wa uzuri wa ndani wa nyumba. "Mimi ni mbunifu kutoka moyoni,” anasema. “Kwa namna ninavyokumbuka, mimi ninavutiwa na ubunifu wa ndani na wa samani, sanaa na fasheni na nimekuwa mwanafunzi bora kabisa wa masuala ya ubunifu na historia yake. Kama mtoto mara zote nilikuwa nachora vitu mbalimbali. Ni mojawapo ya vitu ninavyovifanya kwa raha kubwa.” Wakati muziki wake unakamata chati akajiona amekinai na hivyo kuingia katika awamu nyingine ya maisha yake. Alitoka na kwenda shule Uingereza. Huko alienda kujifunza ubunifu wa ndani na lengo kubwa ni kuboresha weledi katika hilo na mwaka 2012 alianzisha kampuni ya Amorette, yenye makao makuu Dar es Salaam iliyokuwa inajishughulisha na masuala ya urembaji wa ndani. Amorette imepata mafanikio makubwa na Ntuyabaliwe amekuwa akifanya kazi na watu wengine wenye kaliba ya juu katika masuala ya ubunifu wawe binafsi au makamapuni ya kimataifa nchini Tanzania, akichanganya mawazo na ubunifu wao kutengeneza bidhaa zenye kaliba ya juu katika ubunifu, staili, rangi ili wateja wake wawe na maisha mazuri ama majumbani mwao au katika mazingira yao ya kazi. Na katika muda wote wa kufanya hayo, mjasiriamali huyu alikuwa na tabia ya kuchora muonekano wa samani. “Napenda samani , sijui kwanini labda kwa sababu ya kazi yangu ya ubunifu wa maeneo ya ndani, lakini nadhani ni kwa kuwa naamini samani zako zinakuonesha wewe ni mtu wa namna gani. Awali nilitengeneza michoro ya samani kwa ajili ya kujenga ubunifu tu, lakini mara nyingi mume wangu huangalia michoro hiyo na kunipongeza. Alikuwa akisema kwamba situmii vyema kipaji changu. Mara nyingi amekuwa akinihimiza kujikita katika usanii na kuanzisha kampuni ya kushughulika nao,” anasema Ntuyabaliwe akikumbuka alivyoanza. Mume wake, Dkt.Reginald Mengi, ni tajiri mwenye mafanikio makubwa nchini Tanzania ambaye ameujenga utajiri wake kwa kufanya karibu kila kitu kuanzia uzalishaji wa kinywaji cha Coca-Cola hadi uchimbaji wa madini na kumiliki vituo vya televisheni na magazeti. “Ukiwa na mume mwenye mafanikio makubwa namna hii, unashawishika kusaka mafanikio. Kwa hiyo nikatengeneza mpango biashara, kuanza kuajiri wafanyakazi na hivyo kuiweka hai ndoto yangu.” Amorette, ikiwa ni chata yenye mafanikio makubwa miongoni mwa watu wa daraja la juu nchini Tanzania na huku ikipanda kwa kasi na watu wakiifuata, Septemba 2016 Ntuyabaliwe alizindua Molocaho by Amorette kama kampuni ya kubuni na kutengeneza samani. Miezi michache tu tangu kuundwa kwake kampuni imefanya vyema na inaonekana kunedelea kukua kimafanikio. "Tumekuwa katika pilikapilika sana," anasema na kuongeza: " Sikuwa natarajia kufanya biashara kama tulivyofanya katika miezi michache iliyopita." Ntuyabaliwe ndiye mbunifu mkuu wa Molocaho. Akitumia ufundi wa asili katika mazingira ya sasa, Ntuyabaliwe hubuni na kutengeneza samani za kuvutia kwa ajili ya majumbani na maofisini na hata kwa watu binafsi. Ukiangalia samani za Molocaho utabaini uzuri wake kusukwa kwa namna rahisi lakini yenye hisia kali na hivyo kufanya ubunifu wake kuwa wa bashasha , uliotulia na wenye kutuliza kiu. Lakini ukiangalia kwa karibu zaidi utabaini kwamba kile unachokiona rahisi ni tata, kimeumbwa kwa namna ambayo ni makini na yenye ugumu wa aina yake kwa lengo la kukupatia kitu bora kabisa. Hivyo ndivyo Ntuyabaliwe anavyotaka unapoangalia samani zake yaani unaziona za kawaida lakini zenye uzuri na ubora wa hali ya juu. Kwa Ntuyabaliwe,ubunifu wa samani za Molocaho unatokana na wakati mwingine na mambo ambayo hukuyatarajia kabisa. Wakati mwingine tukio asili linaweza kabisa kusababisha ubunifu wa aina Fulani. Mathalani tukio la radi (mwale na mlipuko) ndio uliotengeneza kiti kinachoitwa radi ambacho kimefanya vyema katika mauzo ya ndani na nje. Katika kiti hiki sehemu ya kuegemea kuna mwale wa radi. Molacaho hutengeneza vitu kwa namna ambavyo mteja anataka na maana yake kazi zake nyingi ni za oda. 
 “Wateja wetu huangalia kitabu chetu cha aina mbalimbali za samani kisha wanachagua wanachotaka na kutueleza kitu gani cha ziada wanataka kiwepo. Na hapa huwa tunafanya mazungumzo na wateja wetu ili tuweze kufahamu hasa wanachofikiria na wanachohitaji,” anasema Ntuyabaliwe. Samani zinazotengenezwa kutokana na maagizo kwa kawaida ni gharama kwa kuwa hutengenezwa kwa mahitaji ya mteja. Ntuyabaliwe anakiri kwamba Watanzania wengi hawana uwezo wa kununua bidhaa zake. Wengi wa watanzania ni maskini; Bidhaa za Molacaho zinaanzia kokote kule kuanzia dola za Marekani 250 kama stuli hadi dola za Marekani 6,000 kwa kitanda. “Bidhaa zetu zimepambanua wateja,” anasema na kuongeza kwamba wao si rahisi lakini pia si ghali sana. “kazi zetu si rahisi sana na wala si ghali sana hapa mjini. Mwishoni wa siku huwa tunapata taarifa kutoka kwa wateja wetu kwamba tuna bei nzuri kulinganisha na bidhaa tunazotengeneza.” Wakati Ntuyabaliwe anatengeneza fedha amesema pia anatengeneza mfumo wa kuwaendeleza mafundi nchini Tanzania. Mapema mwaka huu, Amorette, kampuni yake inayoshughulika na ubunifu wa masuala ya ndani ilianzisha programu ya kusimamia mafunzo kwa mafundi wa hapa Tanzania. 

 Lengo kuu ni kuwafanya mafundi wa Tanzania kufikia uwezo wa kubuni na kutengeneza bidhaa zenye hadhi ya kimataifa. Chini ya programu hii, mafundi ambao tayari wana ujuzi na kufanya shughuli za useremala au kitu kinachofanana na hicho wanapewa mafunzo ya miezi miwili na mafundi wanaotambulika kimataifa. Nia ni kuhamisha maarifa, ujuzi na teknolojia kutoka kwa wataalamu hao wa kimataifa na kuwawezesha watanzania kubadilika katika utendaji. Molocaho pia wamejikita katika kuhifadhi mazingira kwa kuhakikisha kwamba hakuna wanachotupa kinachotokana na mchakato wa kutengeneza samani. Kampuni hii hutumia bidhaa za mbao kutoka katika vyanzo mbalimbali na pia inaunga mkono kampeni mbalimbali za upandaji miti nchini Tanzania. “Mwishoni mwa siku biashara si tu iwe inayoleta faida lakini pia lazima ijali maslahi ya jamii ambapo biashara hiyo ipo,” anasema. 

Leo hii, Molocaho imeajiri zaidi ya wafanyakazi wa kudumu 30 huku wakiwa katika njia nzuri ya kutengeneza faida katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwake. “Hakika tumeanza,” anasema Ntuyabaliwe wakati tunaondoka katika duka la Molocaho. 

"Tutaendelea kumkuza mtoto huyu ili siku moja awe kampuni kubwa. Wewe tufuatilie tu" Imeandikwa na Mfonobong Nsehe , wa Forbes na kutafsiriwa kwa wasomaji wa Kiswahili na Mzige Media kupitia TheBeauty.co.tz

ZAIDI YA SHILINGI MILIONI NNE ZAPATIKANA KWENYE HARAMBEE ILIFANYWA NA MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA ILEJE

 Mkurugenzi wa halmashauri ya Ileje Haji Mnasi akiwa kwenye harambee ya uchangiaji wa vifaa vya ujenzi wa zahanati ya ushirika wa Rungwa iliyopo katika wilya ya Ileje.
 Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ileje Haji Mnasi  alihesabu kiasia cha shilingi milioni nne na zaidi kwa lengo la ufanikishaji wa upatikanajiwa vifaa vya kumalizia ujenzi wa zahanati ya ushirika wa Rungwa.


Na fredy Mgunda.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ileje Haji Mnasi afanikisha azima ya ujenzi wa zahanati bora katika ushirika wa rungwa kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa wilaya ya Ileje.


Akizungumuza wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa zahanati hiyo  mkurugenzi Mnasi alisema kuwa wameamua kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha hutuma za afya kwa wananchi ili wafanye kazi kwa kujituma.

“Kauli mbiu ya Rais wetu ni hapa kazi tu sasa ukiwa na jamii ambayo dhohofu huwezi kufikia malengo ya hapa kazi hivyo nimefanya harambee hii kumuunga mkono Rais kwa kuboresha huduma za afya katika wilaya yetu ya Ileje na kuwafanya wananchi kufanya kazi kwa kujituma huku wakiwa na afya njema na kuendelea kulijenga taifa kwa kufanya kazi kwa kujituma”.alisema Mnasi

Mnasi alisema wananchi wanatakiwa kujitoalea kwa hali na mali kufanikisha ujenzi wa zahati hiyo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa jamii.

“Leo hii tumefanya harambee ya kuchangia kupatikana kwa vifaa vya kumalizia ujenzi wa zahanati unaogharimu kiasi cha shilingi milioni sita na nashukuru mungu nimefanikiwa zaidi  kupata shilingi milionii nne  hivyo lengo limetimia kilicho baki ni utekelezaji tu labda niwaombe kuzitumia pesa hizi vizuri kununua vifaa ya ujenzi ili wananchi waanze kupata huduma bora”. Alisema Mnasi

Aidha Mnasi alizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa ushirika wa Rungwa kwa ujenzi wa zahanati hiyo ambayo itarahisisha uwepo wa huduma bora kwa jamii husika.

“Tuna taasisi nyingi sana katika wilaya yetu hivyo naziomba nazo zijitahidi kuwa na malengo ya ujenzi wa zahanati ili kuendeleza kutoa huduma bora kwa jamii na kuifanya jamii kuwa huru kufanya kazi kwa nguvu huku wakiwa na afya bora”.alisema Mnasi

Nao baadhi ya waumini wa ushirika wa Rungwa walimushukuru Mkurugenzi huyo kwa kuendelea kujituma kufanya kazi kwa wananchi wa chini na kuwaboresha huduma za afya.

“Tulikuwa tunahitaji zaidi ya milioni sita lakini uwepo wa mkurugenzi Mnasi katika harambee ya leo kumesaidia kupata pesa nyingi ambazo zimefanisha azma ya umaliziaji wa ujenzi wa zahanati yetu”.walisema washirika

SPIKA MSTAAFU WA ZANZIBAR, PANDU KIFICHO AONGOZA MAHAFALI YA NNE YA CHUO KIKUU CHA BAGAMOYO (UB), KAWE JIJINI DAR ES SALAAM

Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, akimtunuku Mtihimu wa kwanza wa Falsafa ya Udaktari (PhD), Fadhil Innocent baada ya kuhitimu katika mahafali ya nne ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB) yaliyofanyika leo katika Viwanja vya Chuo hicho, Kawe jijini Dar es Salaam. Katikati ni Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Dk. Costa Mahalu. Kificho alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.




 Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho (katikati), akiwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Dk. Costa Mahalu (kushoto) na Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Jaji mstaafu Steven Bwana baada ya kuwasili kwenye mahafali hayo.
Mtihimu wa kwanza wa Falsafa ya Udaktari (PhD), katika chuo hicho, Fadhil Innocent (wa kwanza kushoto), akiwa na wahitimu wa wengine katika mahafali hayo.


Maandamano yakifanyika kuelekea eneo yalipifanyika 
mahafali hayo.
Maandamano yakiendelea.
Wahitimu ndani ya majoho.
Wageni waalikwa wakiwa kwenye mahafali hayo.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Wimbo wa taifa ukiimbwa wageni waalikwa wakiwa wamesimama kwa heshima ya wimbo huo.
Mgeni rasmi Mheshimiwa Kificho (katikati), akiwa meza kuu na viongozi wengine. Kutoka kulia ni Mkuu wa Chuo cha Sayansi, Dk.Abdillah Chande, Dean Chuo cha Elimu, Dk.Mary Mosha, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Dk. Costa Mahalu, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Dk.William Kudoja na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Jaji mstaafu, Steven Bwana.
Wahitimu wa shahada ya kwanza katika ngazi mbalimbali wakiwa kwenye mahafali hayo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Dk.Costa Mahalu akihutubia.
Mgeni rasmi wa mahafali hayo, Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, akisoma hutuba yake.
Ndugu na jamaa za wahitimu hao wakiwa kwenye mahafali hayo.
Wageni waalikwa ndani ya mahafali hayo.
Mwonekano katika mahafali hayo.
Mtoto wa Mwanahabari Happyness Katabazi, Queen Japhet  Mwaijande, akimpongeza mama yake kwa kutunukiwa shahada ya kwanza ya sheria katika mahafali hayo.
Mtihimu wa kwanza wa Falsafa ya Udaktari (PhD), katika chuo hicho, Fadhil Innocent akiwa katika picha ya pampja na ndugu zake.

Na Dotto Mwaibale

CHUO Kikuu cha Bagamoyo (UB), kimefanikiwa kutoa   falsafa ya kwanza ya  Udaktari (PHD), licha ya  changamoto ya utoaji elimu katika majengo ya kupanga kwa gharama kubwa.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Dk. Costa Mahalu kwenye mahafali ya nne yaliyofanyika leo katika viwanja vya chuo hicho, Kawe jijini Dar es  Salaam.

Alisema  katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 499  wamefanikiwa kumaliza masomo yao kwenye fani mbalimbali, wanafunzi 45 ngazi ya cheti na Stashahada 47.

Wengine waliohitimu  shahada 334,Shahada ya udhamiri 71 na shahada ya udamivu ni mmoja licha  ya uongozi wa chuo hicho kukutana changamoto  nyingi ndani ya miaka mitano lakini wanamshukuru mungu kwa hatua hiyo.

“Namshukuru mungu kwa kutupatia kibali cha  kufikia hatua hii ya kufanya mahafali, lakini bado tumekuwa na changamoto ya majengo kwa bado tupo kwenye  majengo ya kupanga,” alisema.

Alisema iwapo serikali itabariki kama ambavyo vibali tayari vimetolewa, hivyo watakuwa na uhakika wa mahafali ya mwakani yatafanyika  kwenye majengo ya chuo  yanayojengwa Kiromo  wilayani Bagamoyo.

Aliongeza kuwa chuo kimekuwa na malengo  ya kuwasomesha wahitimu wa chuo  kwa kuwapeleka vyuo vingine katika shahada ya uzamivu ili kupunguza tatizo la wahadhiri ambalo vyuo vingi nchini wanakabiliana nalo.

Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Pandu Amier Kificho aliupongeza uongozi wa chuo hicho kwa jitihada zao za kuendeleza  chuo hicho katika mazingira magumu.

Alisema kitendo cha kuendelea kutoa huduma ya elimu inaonesha dhamira ya dhati  ya watoa maona kuhusu namna ya kuendeleza elimu nchini Tanzania katika fani mbali mbali.

“Kwa hatua hii hata aliyekuwa anabeza ameanza kujiuliza kuwa tulidhani watashindwa kumbe wameweza, hivyo hiyo itakuwa sifa nzuri ya kusonga mbele,”alisema.

Awali Kaimu Mkuu  wa Chuo hicho Taaluma, Dk.William  Kudoja alisema  wanaendelea na utaratibu wa kuongeza kozi zingine baada ya kukamilisha ujenzi wa majengo yao Bagamoyo.

“Tunaomba wadau, ikiwamo serikali kuhakikisha  wanatusaidia  ili kumiliki majengo yetu wenyewe na kuepuka gharama kwenye majengo ya kupanga,” alisema.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More