Thursday, May 31, 2018

WACHEZAJI NA WATUMISHI WA KLABU YA SINGIDA UNITED FC WAPEWA MIFUKO 50 ya CEMENT KILA MMOJA

Akizungumza na vyombo vya habari hiii leo,Mkurugenzi wa Singida United Ndg. Festo Sanga @sanga_nation amesema, Uongozi wa klabu kuanzia chini ya Rais na mwenyekiti wa timu hiyo wameamua kutoa mifuko ya Cement kwa kila mchezaji na mtumishi wa klabu hiyo kama shukrani na pongezi kwa namna walivyopambana kufanikisha sehemu ya malengo ya klabu kwa msimu wa 2017/2018.

Tukio hilo ambalo kama sila kwanza hapa nchini, basi ni tukio la heshima na upendo wa hali ya juu katika kuimarisha mahusiano ya klabu na wachezaji, Singida United imetoa mifuko hiyo kama alama katika maisha ya wachezaji na watumishi kwamba katika maisha ya soka kuna maisha mengine ya kuanza kujitegemea mapema.

Tayari wachezaji na Watumishi wameshachukua mifuko hiyo kwaajili ya ujenzi wa makazi yao huko makwao.

MBUNGE RITTA KABATI AWATEMBELEA WAFUNGWA WA GEREZA LA WILAYA YA IRINGA NA KUTOA MISAADA MBALIMBALI


 Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati  akiwa na viongozi mbalimbali wa chama cha mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa pamoja viongozi wa gereza la Iringa alipoenda kutoa sadaka ya tende,pesa taslimu kiasi cha shilingi laki saba (700,00) na msaada wa mataulo maalumu kwa wafungwa wa Gereza manispaa ya Iringa kwa ajili wanawake kuyatumia wakati wakiwa katika kipindi cha hedhi

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati ametoa sadaka ya tende,pesa taslimu kiasi cha shilingi laki saba (700,00) na msaada wa mataulo maalumu kwa wafungwa wa Gereza manispaa ya Iringa kwa ajili wanawake kuyatumia wakati wakiwa katika kipindi cha hedhi.


Akizungumza na waandishi wa habari mbunge Ritta Kabati alipowatembelea wafungwa wa Gereza la wilaya ya Iringa alisema kuwa lengo la kwenda kuwatembelea wafungwa ni kwenda kuzijua changamoto ambazo wamekuwa wanakabiliana nazo wakiwa kifungoni.

“Mimi nimekuwa muumini mkubwa sana kwa kujihusisha na maswala ya kijamii hivyo hii leo sio mara yangu ya kwanza kuja hapa Gerezani nimekuja mara nyingi na nimesikiliza kero nyingi na ndio maana zimekuwa zikitatuliwa mara kwa mara kwa kuwa huwa nawasemea vizuri nikiwa bungeni kwenye kuchangia hoja” alisema Kabati

Kabati alisema kuwa licha ya kuwa anakwenda kuwatembelea mara kwa mara lakini huwa anabeba zawadi kwa ajili ya wafungwa,hata hivyo alifanikiwa kutoa zawadi ya sadaka ya tunda la tende kwa ajili ya wafungwa waislamu ambao wamefungwa katika gereza  hilo.

“Huu ni mwezi mtukufu hivyo nimeamua kuja na tende hizi angalau na wafungwa waislamu na wapate tunda hilo ambalo waislamu wengi wamekuwa wakilitumia wakati mfungo wa ramadhani na huu ndio wakati sahihi ndio maana nimefanya hivyo” alisema Kabati

Aidha Kabati alisema kuwa ametoa msaada wa mataulo maalum kwa wafungwa wanawake kwa ajili ya kuwayatumia wakati wakiwa kwenye kipindi hedhi pamoja na kuchangia kiasi cha shilingi laki saba (700,00) pesa taslimu.

“Mimi ni mwanamke hivyo najua mahitaji yetu sisi akina mama hivyo msaada wangu huu wa haya mataulo maalum utaweza kuwasaidia kwa kipindi ambacho wapo Gerezani kwa kuwa wanaweza kuyatumia na kuyafua na kuendelea kutumia tena na pesa ambazo nimetoa nyingine zilikuwa ahadi za msimu ulipita nilipokuja kutelea hapa hivyo nimetoa hizo pesa pamoja na kuwaongeza nyingine” alisema Kabati

Kabati aliwapongeza viongozi wa gereza hilo kwa kuanzisha kiwanda kidogo ndani ya gereza hilo na kuwanya wafungwa kuongeza ujuzi na wengine kuendelea kukuza vipaji vyao wakiwa gerezani.

Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Iringa
Nicolina Lulandala alimpongeza MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa kujitoa kuisaidia jamii ambayo imekuwa ikikumbana na changamoto nyingi.

“Toka jana juzi na siku zilizopita watanzania na wanairinga tumeshuhudia shughuli anazozifanya huyu mbunge hivyo ni lazima sisi cha viongozi wa chama kumuunga mkono kwenye juhudi zake maana tusipofanya hivyo tutamkatisha moyo wa kujitolea kama ambavyo anafanya sasa” alisema Lulanda


Lulanda aliwapongeza pia viongozi wa gereza kwa kuanzisha kiwanda kidogo ndani ya gereza kitu ambacho kinaongeza ufanisi wa kazi kwa wafungwa na kuendelea kukuza vipaji vyao na kuibua pia vipaji vipya ndania ya gereza.

“Mimi na wezangu ambao tumefika hapa gerezani tumefurahi sana kitendo cha kuona kuwa kuwa kunakiwanda cha kutengeneza vikapu fagia na vitu vingine kweli nimefarijika ndio maana tukashawishi hata kuvinunua bidhaa ambazo wanazingeneza ambazo zinaubora mzuri kweli” alisema Lulanda

Wednesday, May 30, 2018

FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY WATOA SOMO KUELEKEA UCHAGUZI NCHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Bw. Francis Kiwanga akitoa ufafanuzi mbele ya wageni waalikwa mapema leo jijini Dar es salaam wakati akifungua  mkutano wa kujadili nafasi ya Asasi za kiraia katika chaguzi zijazo hapa nchini.

Asasi za kiraia nchini zimetakiwa kujitoa katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kwa wingi katika chaguzi mbalimbali ikiwemo ya serikali za mitaa na wa serikali kuu wa mwaka 2020.

Hayo yamesemwa mapema leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society Bw. Francis Kiwanga alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi, wenye lengo la kujadili hali ilivyo kabla ya kufikia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani.
Mzee Gallus Abeid kutoka Mwalimu Nyerere Foundation akichangia mjadala mapema leo jijini Dar es salaam katika Mkutano wa Uchaguzi ulioandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Foundation for Civil Society.

Katika Mkutano uliowakutanisha wadau kutoka Asasi mbalimbali za Kiraia, Taasisi za elimu ya juu, vyama vya wafanyakazi, vyama vya dini mashirika yanayoshughulikia amani nchini  kujadili nafasi na wajibu wao kama azaki kuelekea chaguzi zijazo hapa nchini.
Bwana Kiwanga amesema kuwa ushiriki wa wananchi katika kupiga kura umekuwa ni mdogo sana kwani 2010 wamepiga asilimia 43 peke yake na kwa mwaka 2015 ni asilimia 67 ya wananchi wote wenye sifa za kupiga kura.
Baadhi ya washiriki kutoka asasi mbalimbali za kiraia wakifuatilia kwa umakini mkutano.


Ameeleza kuwa  hii inatokana na wananchi kutokuwa na imani na viongozi wanaochaguliwa kwani wanaamini hata usipopiga kura basi mgombea wa chama fulani atapita kwa njia yeyote ile, hivyo taasisi zinazohusika ikiwemo wizara ya tamisemi na NEC pamoja na ZEC kuboresha utendaji wao wa kazi ili kurejesha imani hiyo kwa wananchi.


Amesema  kuwa asasi za kiraia zina jukumu kubwa la kushirika katika mchakato kabla, kipindi chenyewe cha uchaguzi na baada ya uchaguzi kwa kuwapa hamasa wananchi lakini pia kuomba nafasi za uangalizi katika kipindi hicho.
Wageni waalikwa wakifuatilia mkutano kwa umakini.

Amesistiza uhalali wa kuwapata viongozi ambao ni matwakwa ya wananchi kwani hii inaweza kuleta kitu kizuri kwa kuwa atakuwa kapewa Baraka zote na wananchi na pia watashirikiana nae kwa hali na mali kwa kuwa wanajua ndio chaguo lao sahihi.
Kwa upande wake Mzee Gallus Abeid kutoka Mwalimu Nyerere Foundation amesisitiza uwepo wa amani katika kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi kwani amani ndio msingi wa mambo yote.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa uchaguzi ulioandaliwa na shirika la Foundation for Civil Society wakiwa katika picha ya pamoja mapema leo jijini Dar es salaam.


Amesema  kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa hivyo inapotokea watu wanamchagua mgombea Fulani alafu matokeo yanabadilishwa na kupewa mtu mwingine hii sio sawa na inaweza kutowesha amani ya nchi

Lakini pia hali ya mtu anatumia muda mwingi kwenye foleni ya kujiandikisha na mwisho wa siku anaenda kupiga kura anaambiwa jina lako halipo kwenye daftari hali hii inasababisha watu wengi kuacha kujiandikisha kupiga kura na kupoteza haki yao ya msingi.

PDF WAWATAKA WAZAZI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA MTOTO WA KIKE KATIKA HEDHI


Diwani wa kata ya Mtambula, Isack Kilamlya akitoa neno kwa wazazi na wanafunzi juu ya kutambua na kutoa elimu juu ya hedhi na jinsi ya kujihifadhi kwa watoto wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi duniani
Afisa mradi wa shirika lisilo la kiserikali la peoples development forum (PDF) ambalo linafadhiwa na UNICEF 
upande wa usafi wa mazingira lishe bora watoto Adventina Lazaro akitoa neno kwa wazazi na wanafunzi juu ya kutambua na kutoa elimu juu ya hedhi na jinsi ya kujihifadhi kwa watoto wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi duniani


 Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Mwesa wakiwa na mabango yakiwa na maandishi yaliyoandikwa kwa maneno tofauti tofauti wakatika maadhimisho ya siku ya hedhi duniani
 Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi ya Mwesa  wakitengeneza pedi za asili kwa kuonyesha kuwa sio lazima kununua dukani bali waweza kutengeneza hata nyumbani kwako na zikakustili vizuri tu

NA FREDY MGUNDA, MUFINDI IRINGA.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la peoples development forum (PDF) ambalo linafadhiwa na UNICEF mkoani Iringa wilaya ya Mufindi limelenga kuwawezesha wasichana kutimiza ndoto za maisha yao kwa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowafanya wabaki nyuma katika kuhudhuria masomo kipindi wakiwa katika hedhi. 

Hayo yamezungumzwa na afisa mradi wa shirika lisilo la kiserikali la peoples development forum (PDF) upande wa usafi wa mazingira lishe bora watoto Adventina Lazaro wakati wa maadhimisho ya siku ya hedhi Duniani ambapo wilaya ya Mufindi yalifanyika katika shule ya msingi Mwesa kata ya Mtambula,tarafa ya Kasanga lakini kimkoa yalifanyika kwa mara ya kwanza katika Bustani za Manispaa na kuhudhuriwa na wanafunzi wa kike kutoka shule mbalimbali za sekondari za mjini hapa

Lazaro alisema kuwa changamoto kubwa ambayo wanakabiliana nayo watoto wa kike wengi walioko mashuleni ni kipindi cha hedhi ambapo baadhi yao wamekuwa hawana elimu, kutojiamini na utoro mashuleni wanapokuwa kwenye vipindi vya hedhi hali inayosababisha utoro. 

lazaro alisema kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anahudhuria masomo yake kwa mwaka mzima pasipo kuwa na vikwazo vinavyosababishwa ama na mazingira duni au ukosefu wa bajeti katika kupata taulo hizo maalum za hedhi. 

Aliwataka wadau na wananchi kwa ujumla kuvunja ukimya juu ya suala la hedhi salama kwa mtoto wa kike na kuwezesha mtoto wa kike kupata taulo maalum kila mwezi na mkoa wa Iringa una mkakati maalum wa kumaliza changamoto hizo. 

“Changamoto mbalimbali zinazowakabili wasichana wanapokuwa kwenye vipindi vya hedhi yanapaswa kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuwa yanachangia kurudisha nyuma jitihada za kuwainua watoto wa kike nchini na kuwataka mabinti kuondoka na aibu ya katika suala la hedhi hivyo mkakati upo kumaliza kwa kuwapatia bure mataulo maalum watoto wa kike” alisema lazaro 

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayo dhamira ya dhati kuhakikisha elimu bure inapatikana kwa jinsia zote hivyo basi suala la hedhi salama kwa wa kike ni jambo la msingi katika ngazi ya familia, jamii, na hata mashuleni kuwapatia elimu itakayowezesha kuwa na ufahamu wa masuala ya hedhi.

Awali diwani wa kata ya Mtambula, Isack Kilamlya alisema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuvunja ukimya juu ya masuala ya hedhi ikiwemo kuondokana na dhana potofu kwamba hedhi ni ugonjwa pamoja na namna bora ya kuhakikisha mtoto wa kike anajiweka katika hali ya usafi ili abaki shuleni badala ya kukosa masoko kila apatapo hedhi. 

Kilamlya Alisema ukosefu wa mazingira bora kama vyoo, maji safi na salama pamoja na vyumba mahsusi vya kubadilishia nguo, hasa kwa watoto wa kike wanapokua katika hedhi mashuleni kuna changia utoro. 

“Hakuna vikwazo zaidi wezesha wanawake na wasichana kupata hedhi salama hivyo wananchi wanapaswa kutoa ushikiano kwa shirika hilo lina mikakati ya kuwezesha watoto wa kike kupata elimu kwa mtoto kike kama wanafunzi wengine na kuhudhuria masomo yake akiwa huru” alisema Kilamlya

Akisoma risala kwa mgeni rasmi Adili Mlema mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi ya Mwesa alisema kuwa analishukuru shirika lisilo la kiserikali la peoples development forum (PDF) ambalo linafadhiwa na UNICEF kutoa elimu ya maswala ya hedhi ambayo sasa yamekuwa msaada kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Mlema aliongeza kwa kuwataka wazazi na viongozi mbalimbali wa serikali na wasio wa serikali kutoa elimu ya hedhi kwa jamii husika ili kuondoa aibu ambayo wazazi wengi wanayo katika kuwaeleza watot wao wa kike.

“Bila shirika lisilo la kiserikali la peoples development forum (PDF) hadi leo hii tungekuwa hatuna elimu ya maswala ya hedhi ambapo wanafunzi wengi walikuwa wanaona aibu kuja shule siku wakiwa katika siku za hedhi” alisema Mlema

Naye mmoja wa wazazi aliyehudhulia siku ya hedhi wilaya ya Mufindi Emeliziena Danda aliwataka wazazi kutoa elimu juu ya hedhi kwa watoto wa kike wanakaribia kuvunja ungo ili wajue elimu hiyo.

“Nawapongeza sana shirika lisilo la kiserikali la peoples development forum (PDF) kuwa kututoa aibu wananchi kwa kutuambia ukweli ambao leo hii tumekuwa huru kuwaambia watoto wenu na watoto wetu nao wamekuwa huru kutuambia nini kinachiwatokea” alisema Danda.

Tuesday, May 29, 2018

MBUNGE RITTA KABATI ATOA SADAKA YA TENDE KWA WAUMINI WA DINI YA KIISLAM MANISPAA YA IRINGA


 Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati akiongea na viongozi wa misikiti yote ya manispaa ya Iringa wakati wa utoaji sadaka ya tende kwa waumini wa dini ya kiislamu wa manispaa ya Iringa kwa ajili ya kuadhimisha mfungo wa ramadhan kwa waislamu wa wote wa manispaa ya Iringa. 


 Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza amemshukuru mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa kutoa sadaka ya tunda la tende kwa waiislamu katika  kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan.
 Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza akikabidhi tende alizokabidhiwa na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa kutoa sadaka  kwa waiislamu katika  kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan.
Mkuu wa walimu na msimamizi wa misikiti ya Dhinureyn Tanzania Abdul Salam Ahmad Ayub akimshukuru mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa sadaka aliyoitoa kwa waislam katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan.
Baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi (CCM) na viongozi wa misiki ya manispaa ya Iringa walipohudhulia zoezi la utoaji wa sadaka ya tende ilitolewa na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati ametoa sadaka ya tende kwa waumini wa dini ya kiislamu wa manispaa ya Iringa kwa ajili ya kuadhimisha mfungo wa ramadhan kwa waislamu wa wote wa manispaa ya Iringa

Akizungumza wakati wa kukabidhi sadaka hiyo katika msikiti wa Dhinureyn Gangilonga Kabati alisema kuwa kila mwaka amekuwa akifutulisha katika maeneo mbalimbali hivyo mwaka huu ameamua kununua tende na kugawa kwenye misikiti yote ya manispaa ya Iringa.

“Unajua mwaka huu tende ni tunda ambalo linahitajika katika kipindi hiki cha mfungo na kuna watu ambao hawana uwezo wa kununua tende hizi na ukiangalia mwaka huu tende zimepanda bei sana hivyo kwa kiasa ambacho nakipata nimeamua kutoa sadaka hii kwa waumini wa kiislam” alisema Kabati

Kabati aliwataka wananchi wengine kuendelea kumuabudu mwenyezi mungu pale ambapo tunapata nafasi ili kupunguza maovu ambayo tumekuwa tukiyatenda kwa kukusudia au bila kukusudia na kufanya hivyo basi mwenyezi mungu atatuongezea pale ambapo tumepunguza kwa ajili ya kumtumiaka mungu.

“Katika kipindi hiki nawaomba wazazi,walezi na viongozi wetu naomba tutoe elimu kwa vijana wetu kwa kuwapa elimu ya dini pamoja maadili ya nchi yetu kwa lengo la kuwajenga vijana wawe wanamcha mungu hasa kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan” alisema Kabati

Kabati alisema kuwa ametoa sadaka ya tende tani mbili ambayo ipo katika halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa ajili ya misikiti yote na vituo vya watoto yatima ambavyo vinawatoto wa kiislam ambao wanafunga katika kipindi hiki cha mfungo.

“Mimi nimeleta tani mbili ili kuongezea nguvu wafungaji wa kipindi hiki lakini kutoa sadaka kwa mwenyezi mungu katika kipindi ambacho waislamu wapo kwenye mfungo wa ramadhan nakuwasidia wale ambao hawana uwezo wa kununua tunda hili la tende” alisema Kabati

Kwa upande wake mgeni rasmi Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza amemshukuru mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati kwa kutoa sadaka ya tunda la tende kwa waiislamu katika  kipindi hiki cha mfungo wa ramadhan.

“Tunashukuru sana kwa sadaka hii ambayo umetusaidia kwa waislam wa manispaa ya Iringa kwa msaada wako ambao utasiadia kwa wale ambao wanamahitaji maalumu na mungu atakuongezea aple ulipopunguza na mungu akubariki” alisema Masenza

Masenza aliwaomba maimamu kuwagawia tende hizo waislam ambao hawana uwezo wa kununua tende tukani ili nao wapate hiki chakula cha kwanza pindi unapofungua na wale wenye uwezo wa kununua tende dukani basi waendelee kununua

Naye mkuu wa walimu na msimamizi wa misikiti ya Dhinureyn Tanzania Abdul Salam Ahmad Ayub alisema kuwa msaada aliotoa mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringakupitia chama cha mapinduzi (CCM) Ritta Kabati utawasaidia waislam waliofunga.

“Sadaka hii aliyoitua huyu mbunge Kabati umekuja wakati muafaka na umamanufaa makubwa sana kwa waislam kwa kuwa tumehimizwa kufuturu kwanza tende hivyo kwa muislam kula tende ni fadhila kubwa sana”alisema Ayub

Ayub alisema kuwa katika kipindi hiki cha mfungo waislam tunatakiwa kupeana vyakula ili kila mtu ambaye hana kitu aweze kupata chakula na ndio alivyofanya huyu mbunge Ritta Kabati kwa waislam wa manispaa ya Iringa.

“Zamani watu walikuwa wanatandika jamvi nje wakati wa kufutulu ili waweze kufutulu na waislam ambao hawana uwezo na ndio uzalendo wenyewe huo,hivyo tunamuombea mbunge huyu aendelee na moyo huo huo” alisema Ayub

AMREF YAISHUKURU SERIKALI KUAMINI UTENDAJI WAO

 Mkurugenzi wa Amref Tanzania, Florence Temu (aliyekaa kushoto), akisaini mkataba wa kufanya kazi pamoja na Tayoa. Kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tayoa, Peter Masika. Anayeshuhudia katikati ni Mkurugenzi wa Bodi ya Uratibu ya Miradi ya Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu inayofadhiliwa na mfuko wa dunia Dr. Rachae Makunde.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Health Promotion Services (THPS), Redemputa Mbatia, akipeana mkono na Mkurugenzi wa Amref Tanzania, Florence Temu baada ya kusaini mkataba huo.
 Wadau wa masuala ya Afya wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Faustine Ndugulile, akihutubia kwenye uzinduzi huo.
 Emiliani Busara kutoka MDH, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
 Mchungaji Basilisa Ndonde akizungumza kwenye uzinduzi huo.
 Mkurugenzi wa Amref Tanzania, Florence Temu (aliyekaa kushoto), akisaini mkataba wa kufanya kazi pamoja na MDH. Kulia ni Emiliani Busara kutoka MDH.
 Mkurugenzi wa Amref Tanzania, Florence Temu, akihutubia kwenye uzinduzi huo.
  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Faustine Ndugulile (wa pili kushoto), akiwa na viongozi wengine katika uzinduzi huo.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tayoa, Peter Masika (kulia), akipeana mkono na Mkurugenzi wa Amref Tanzania, Florence Temu baada ya kusaini mkataba huo.
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tayoa,, Peter Masika, akihutubia.
 Mkurugenzi wa Bodi ya Uratibu ya Miradi ya Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu inayofadhiliwa na mfuko wa dunia Dr. Rachae Makunde ,  akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mkapa Foundition, Rahel Sheiza (kulia),  akipeana mkono na Mkurugenzi wa Amref Tanzania Florence Temu baada ya kuisaini makubaliano ya kufanya kazi pamoja.

Na Dotto Mwaibale

MKURUGENZI Mkazi wa Amref nchini Tanzania, Florence Temu ameishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli na zilizopita kwa ushirikiano inayotoa kwao.

Temu alitoa shukurani hizo kwenye uzinduzi wa mradi wa Amref Health Africa wa kupambana na Ukimwi na Kifua Kikuu unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Kwenye uzinduzi huo ambao mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee na Watoto, Dr.  Faustine Ndugulile walihudhuria pia Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri  wa Amref Tanzania, Dr. Eric Van Praag, Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na Ukimwi (UNAIDS), Dr. Leo Zekeng  na viongozi na wawakilishi wa mashirika mbalimbali  yaliyopewa dhamana ya kusimamia mpango wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ili kufikia asilimia 90 ya  waishiyo na   VVU kupatiwa tiba na asilimia 90 ya walio kwenye tiba za VVU 90 wafanikiwe kufubaza VVU.

Temu alisema kuwa, baada ya kupitia michakato ya kutambua asasi itakayochukua jukumu la 'Principle Recipient' katika mkondo wa taasisi zisizokuwa za serikali, mwanzoni mwa mwaka jana, Amref Health Africa Tanzania ilihidhinishwa rasmi na hatimaye Februari 21 walisaini kama Principle Recipient wa mkondo wa taasisi zisizo za serikali Mfuko wa Dunia wa Fedha zenye thamani ya Bilioni 55 na milioni 256 na laki 7 (yaani $24,969,174) kwa ajili ya kuibua na kutibia VVU na Kifua Kikuu, wakikabidhiwa jukumu la kusimamia na kuratibu afua za kwenye jamii zihusuzo Ukimwi na Kifua Kikuu kwa kupitia asasi ya kijamii, takriban asilimia 10% ya fedha hizo zitaelekezwa katika afua za kukabiliana na Kifua Kikuu katika jamii.

Aliongeza kuwa, kwenye mapambano ya maradhi hayo wataifikia mikoa 15 ambayo ni Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Simiyu, Singida,Tanga na Ruvuma.

"Tunatarajia kupitia mfuko huu jumla ya watu 546,880 watafikiwa na huduma ya kupima VVU na kujua majibu, pia wasichana wa umri rika/ balehe na wanawake 162,064. Lakini pia kuibua na kuwapa rufaa wenye maambukizi ya kifua kikuu wapatao 16,465 watapata uchambuzi zaidi kwenye uwakilishi utakaofuata," alisema Temu.

Aliongeza kuwa, Amref inathamini kwa dhati jukumu walilopewa la kuratibu na kuongoza mradi huo uliofadhiliwa na Global Fund kwa miaka mitatu ijayo na kuahidi kufuata muongozo stahiki uliopo katika kutekeleza mradi huo, kwa dhana hiyo wanaahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau husika kadiri watakavyoweza.

"Tutashirikiana moja kwa moja kama Amref lakini pia kwa kuwatumia sub recipients wetu ambao ningependa muwatambue," alisema Temu na kuwataja kuwa ni Tanzania Health Promotion Services (THPS), Management and Development fo Health (MDH), Benjamin Mkapa Foundition (BMF) na Tanzania Youth Alliance (TAYOA).
Aliongeza kuwa, wanatambua changamoto zilizopo katika kufikia jamii  hasa kwenye malengo ya kuwafikia wanaopaswa kujua hali yao ya maambukizi, ambapo kulingana na takwimu za Tanzania HIV Impact Survey ambao ni asilimia 52.2% ya walio na umri wa miaka 15-64 tu ndiyo wamepima na kujua hali zao za maambukizi; na uhaba wa wanaume kufikia huduma hizo, pia kuwepo kwa makundi yenye mazingira hatarishi zaidi ya kuambukizwa na kuambukiza VVU, pia haja ya kuibua wenye kifua kikuu na kuhudumia wenye TB sugu katika jamii, hizo ni baadhi tu!

Temu alisema wanatambua juhudi za Serikali ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha anafikia asilimia hizo 90 tatu na nia ya kutokomeza kifua kikuu na kudhibiti maambukizi na kupeleka huduma hizo katika ngazi za jamii kuimarisha mifumo ya usambazi dawa na vifaa tiba, kusomesha wataalam, kuboresha vituo vya afya na hospitali na mifumo ya rufaa ni juhudi za wazi na wanaipongeza wizara ya afya inayoongozwa na Waziri Ummy Mwalimu akishirikiana kwa karibu na naibu wake Dr. Faustine Ndugulile.

"Mfano nichomekee kidogo hapo jinsi Amref kwa kupitia brand ya Angaza tulivyoweza kuleta huduma rafiki za upimaji wa VVU ulivyoweza kuifikia jamii ya rika zote na jinsi zote na hata kuwa huduma rafiki kwa jinsi za kiume yaani wanaume, tunashauri serikali iendelee kutumia hiyo brand kwani tunaamini neno Angaza ni rafiki na linaondoa hofu na linaleta ujasiri hata kwa wanaokuwa na VVU," alisema Temu.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, wanashukuru uthubutu wa wataalam wa wizara ya afya kuweza kuongeza wapimaji wa VVU kutoka kwa wataalam wa maabara hadi wahudumu wa afya walio wa maabara.

Alimalizia kwa kusema, wao Amref na wadau  wakiwemo SRs, wataendelea kufanya kazi kwa karibu na kufuata miongozo ya Global Fund, Sera na mitakati ya kitaifa, maelekezo ya vikao mbalimbali vya TNCM na hata kusimamia matumizi ya fedha za ufadhili huo na kutumia vyombo vilivyopo katika kutafuta ushauri ikiwemo wizara ya afya na vitengo vyake ambavyo ni Sekretariet ya TNCM,lfa PR-1 (Wizara ya Fedha) na Programme za NACP na NTLP pamoja na GF Office ya Wizara ya Afya.

Naye Dr. Ndugulile akizungumza katika uzinduzi huo, aliishukuru Amref na wadau wengine waliopewa jukumu la kupambana na maradhi ya kifua kikuu pamoja na Ukimwi ambao ni THPS, MDH, BMF na TAYOA.

Naibu waziri huyo aliwataka wote kuwa wabunifu na wenye mikakati ili kufikia malengo ya  kupambana na maradhi hayo kama walivyoyaanisha kwenye mchanganuo wa bajeti waliyoomba.

Alisema milango ipo wazi kwa wao kufika ofisini kwao kwa lengo la kuhitaji ushauri wowote watakaouhitaji.


JUMIA FOOD YASHIRIKIANA NA WATEJA KUSAIDIA WATOTO


Na Jumia Food Tanzania

Katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jumia Food kwa kushirikiana na wateja wake inaendesha kampeni ya kusaidia kituo cha kulelea watoto yatima cha Maunga kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kampuni hiyo inayojihusisha na huduma ya chakula kutoka migahawa mbalimbali jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao, imeona ni vema kuwashirikisha wateja wake kwani wao ndio wadau wake wakubwa.

Kampeni hiyo inayokwenda kwa jina la ‘STANDY BY ME,’ kwa kiasi kikubwa inawategemea wateja kwa sababu kwa kila huduma ya chakula watayoifanya kupitia mtandao wa Jumia Food itakwenda moja kwa moja kumsaidia mtoto mmoja kituoni hapo.


Akifafanua namna wateja wanavyoweza kuchangia, Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Food Tanzania, Kijanga Geofrey, amesema kuwa, “ni rahisi kushiriki kwenye kampeni hii kwani hatua za kufuata ni zilezile za kawaida anazozifanya mteja anapoagiza chakula. Kinachobadilika ni pale anapotaka kukamilisha huduma yake katika sehemu ya malipo itampasa atumie nenosiri 'ASANTE.’

Baada ya kuweka nenosiri hilo mteja atakuwa amejihakikishia kuchangia mtoto mmoja wa kituo cha Maunga. Kitakachofanyika kwa upande wa Jumia Food ni kuhesabu idadi ya huduma zote za kuagiza chakula zilizofanywa kwa kutumia neno ‘ASANTE.’ Idadi hiyo ndiyo itakayobainisha kuwa ni wateja wangapi wamehamasika kushiriki katika kampeni hiyo.
“Ningependa kuwatoa wasiwasi wateja wetu kwamba watapata huduma yao ya chakula kama siku zote, huku Jumia Food ikipeleka sehemu ya mchango wao kuwasaidia watoto hao. Kwa hiyo, sisi pia tutachangia kiasi fulani ambacho baada ya kukusanywa kitatumika kununulia mahitaji mbalimbali ambayo yatawasilishwa katika kituo cha Maunga. Ningependa kuchukua fursa hii kuwataka wateja wetu na watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi zaidi ili kuwawezesha watoto hawa kupata mahitaji yao ya msingi,” alihitimisha Geofrey.

Kama haujawahi kutumia huduma za Jumia Food, ni rahisi kufanya hivyo. Unaweza kuagiza huduma ya chakula kwa kuingia kwenye tovuti yao ambayo ni www.food.jumia.co.tz au kupitia App yao inayopatikana kwenye simu ya mkononi. Baada ya kuingia, jaza jina la eneo ulipo, itakuja orodha ya migahawa kadhaa iliyo karibu nawe pamoja na aina ya vyakula unavyohitaji, kamilisha huduma kwa kuhakikisha gharama ya huduma pamoja na kujaza taarifa zako binafsi ambazo zitatumika kuletewa chakula na muwakilishi kutoka Jumia Food.  

Huduma za Jumia Food zinaweza kutumiwa na mtu wa kipato chochote kwa sababu unaweza kuagiza chakula kuanzia shilingi 500 na kuletewa mpaka mlangoni kwako.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More