Monday, November 23, 2015

Mbaroni Kwa Kusafirisha Matenga 8 ya Bangi

POLISI mkoani Morogoro inawashikilia watu watatu, wakazi wa Manispaa ya Morogoro na Kinondoni, Dar es Salaam kwa tuhuma za kusafirisha matenga manane ya bangi iliyohifadhiwa pamoja na ndizi.

Bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa katika gari kubwa iliyokuwa ikitokea mkoani Singida kuelekea Dar es Salaam na miongioni mwa wanaoshikiliwa ni pamoja na dereva wa gari hilo, Venance Patrick (44), mkazi wa Kiwanja cha Ndege, mjini hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 21, mwaka huu saa tisa usiku katika eneo la mizani Mikese katika barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamanda Paulo, Patric alikuwa akiendesha gari namba T 269 BJN aina ya Volvol Semi yenye tela namba T 215 AGC. Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Jumanne Makila (28) mkazi wa Kiwanja cha Ndege na Juma Mbaraka (30) mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam.

Kamanda huyo alisema, askari waliokuwa katika operesheni maalumu barabara kuu walifanikiwa kukamata gari na watuhumiwa hao wakiwa na bangi ndani ya gari yenye uzito wa kilo 120 ikihifadhiwa kwenye matenga manane kwa kuchanganywa na ndizi mbichi. Alisema polisi wakikimilisha upelelezio watawafikisha mahakamani watuhumiwa hao.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More