Monday, November 23, 2015

Kubenea Kumburuza Mahakamani Spika wa Bunge Job Ndugai Kwa Kuvunja Kanuni Na Kuwaruhusu Polisi Kuingia Bungeni

Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema atamfikisha mahakamani Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa kuvunja kanuni baada ya kuwaingiza polisi ndani ya ukumbi wa chombo hicho.

Polisi hao waliingia ndani ya ukumbi huo wiki iliyopita wakati Rais John Magufuli alipofika kwa ajili ya kuhutubia Bunge.

Kubenea alisema kitendo cha askari kuingia ndani ya Bunge kwa mara ya mwisho kilitokea nchini Uingereza mwaka 1930 na hakijawahi kutokea tena isipokuwa nchini.

Alisema kuwa kesi hiyo anatarajia kuifungua Mahakama Kuu wiki ijayo kwa ajili ya kutaka tafsiri ya kanuni hiyo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel alisema hakuna kanuni iliyovunjwa kwa askari hao kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge.

Wakati Kubenea akiandaa mpango huo, Kamati ya Wabunge CUF imesema Spika Ndugai ndiye chanzo cha yaliyotokea bungeni.

Ijumaa wiki iliyopita wakati Rais akiingia kutoa hotuba ya kuzindua Bunge, wabunge hao walipiga kelele wakitaja jina la mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuonyesha msimamo wao dhidi ya uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo.

Walipiga kelele hizo wakati Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein akiingia kwenye ukumbi huo na baadaye wakati Dk Magufuli akiingia ukumbini na wakagoma kunyamaza hadi walipotakiwa kutoka nje na askari kuitwa ndani.

Wabunge wa upinzani wanadai kuwa Dk Shein si Rais wa Zanzibar, wala makamu wake wa pili, Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho kwa madai kuwa muda wao uliisha Novemba 2, baada ya Uchaguzi Mkuu.

Jana wabunge wa CUF chini ya Mwenyekiti wake, Juma Hamad Omary walitoa tamko lililokemea na kutoa tahadhari kwa mambo mawili huku wakimtaka Ndugai kutoyumbishwa na Serikali.

Katibu wa Umoja huo, Hamudu Hassan Bobal alisema vurugu zisingetokea endapo Bunge hilo lingezingatia tamko la barua ya Ukawa na kusikilizwa hoja ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyeomba mwongozo akitaka kujua Dk Shein na wenzake wanaingiaje bungeni wakati madaraka yao yaliisha tangu Novemba 2.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More