Monday, November 16, 2015

Mwakyembe Azungumzia Tetesi za Yeye Kuwa Waziri Mkuu

Mbunge Mteule wa Jimbo la Kyela,  Dkt. Harrison Mwakyembe (pichani) amesema Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania atatokana  na uteuzi utakaoidhinishwa na  Bunge na si taarifa zilizopo sasa katika mitandao ya kijamii.
 
Dkt. Mwakyembe ambaye amewahi kuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi,  Waziri Mkuu anateuliwa na Rais ambaye huwasilisha jina hilo kwa Spika wa Bunge na baadaye kupigiwa kura na Wabunge.
 
 Mbunge huyo aliyasema hayo jana Jumapili  (Novemba  15, 2015) Mjini Dodoma wakati alipokuwa akihojiwa na vyombo vya habari kuhusu tetesi zilizopo katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kuhusiana na jina lake kutajwa kuwa ndiye Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano.
 
“Mimi siwezi kuwasemea wananchi na siwezi  kusema kuna watu wengi wanasema hivi,  kwani nafasi ya Uwaziri Mkuu haiji kwa njia ya kura ya maoni, wala kwa  njia ya mitandao ya kijamii ni nafasi ya uteuzi inayoidhinishwa na bunge na ni mamlaka ya Rais wa nchi” alisema Dkt. Mwakyembe.
 
Aidha, Mhe. Mwakyembe aliwataka Watanzania bila kujali itikadi za dini na vyama vyao wamuombee Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili aweze kuchague viongozi watakao wajibika na ambao wataendana na kasi ya Mhe. Rais.
 
Wabunge wengine waliotajwa kuwepo kwa uwezekano wa kuteuliwa nafasi ya Uwaziri Mkuu wa Awamu ya Tano ya Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli ni pamoja na Mhe. William Lukuvi, Mhe.  Prof. Sospeter Muhongo na Mhe. January Makamba.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More