Friday, September 29, 2017

JAFO: WATENDAJI MSILETE LELEMAMA USIMAMIZI MIRADI YA MAENDELEO

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni, Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu na Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki (CCM) Mhe Daniel Mtuka
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akiwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakikagua chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akitembelea na kukagua mradi wa maji Kintinku/Lusilile wilayani Manyoni
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akimshukuru Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo kwa ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua mradi wa maji Kintinku/Lusilile wilayani Manyoni
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo akikagua chumba cha dawa katika Kituo cha Afya Kintinku wilayani Manyoni, Mwingine ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu
  
Na Mathias Canal, Singida

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Tamisemi) Mhe Seleman S. Jaffo (Mb) amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida kuanza haraka Mradi wa Ujenzi wa Chumba Cha upasuaji, na Ujenzi wa wodi ya kisasa.

Naibu Waziri Jaffo ametoa maagizo hayo wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa kituo Cha afya Kintinku mara Baada ya kutembele na kujionea uduni wa upatikanaji wa Huduma katika kituo hicho.

Alisema Mradi huo utaambatana na Ujenzi wa maabara kwa ajili ya vipimo kwa wagonjwa, Ujenzi wa eneo la kuchomea taka na Ukarabati wa eneo la kuhifadhia maiti.

Jafo ameonyesha kukerwa na ucheleweshwaji wa kuanza Ujenzi huo licha ya serikali kupeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2017/2018 zitakazotosha kukamilisha Ujenzi wote.

Alisema katika awamu ya Pili zitatolewa fedha kiasi cha shilingi milioni 220 zitakazotumika kununua vifaa vyote katika Chumba Cha upasuaji na vifaa tiba kwa ujumla.

Naibu Waziri Jafo alisema kitendo Cha kuchelewa kuanza Ujenzi huo kinachelewesha kuwapatia huduma bora wananchi ambayo inahubiriwa na serikali ya awamu tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.

"Haiwezekani Rais anatoa fedha kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya Afya halafu kuna watu wachache wanashindwa kusimama vizuri fedha Hizo Jambo ambalo linapelekea serikali kulaumiwa na wananchi" Alisema Jaffo

Katika hatua nyingine Mhe Jaffo alimuagiza mhandisi wa Maji Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Vijijini Eng Gasto Mbondo kutekeleza mpango wa shughuli za utoaji wa Huduma ya maji kupitia Mradi wa kisima Cha Kintinku/Lusilile kilichopo Kijiji Cha Mbwasa (Mbwasa Well Field) kwani eneo Hilo linaonekana kuwa na maji ya kutosha.

Akikagua mradi huo Mhe Jaffo alisema tatizo kubwa kwa wananchi Ni pamoja na changamoto sugu ya upatikanaji Huduma za maji hususani vijijini na kukamilika kwa mradi huo utapunguza umbali na muda wanaotumia wananchi kutafuta maji. 

Awali Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Eng Gasto Mbondo akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za utoaji wa Huduma ya maji alisema kuwa Mradi huo wa maji wa Kintinku/Lusilile utakapokamilika unatarajia kuhudumia watu wapatao 45,417 kwa kuongeza 19.2% kutoka 42.1% iliyopo mpaka 61.3% na utakuwa na Vituo 81 vya kuchotea maji (DPs).

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utasimamiwa kwa karibu na ofisi yake ili kuongeza Hamasa na tija.

Pia alisema katika Mradi wa Ujenzi wa majengo kwa ajili ya kituo Cha Afya Kintinku asilimia kubwa ya mafundi watatoka katika Wilaya ya Manyoni ili kutoa ajira kwa wananchi husika.

MWISHO.

MAMIA WAFUNGULIWA KWENYE MKUTANO MKUBWA WA INJILI JIJINI MWANZA

 Na George Binagi-GB Pazzo
Wakazi wa Jiji la Mwanza wakiwemo waumini wa dini mbalimbali wameendelea kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano mkubwa wa injili ulioandaliwa na kanisa la kanisa EAGT Lumala Mpya chini ya Mchungaji Dkt.Daniel Moses Kukola.

Jana mamia ya wananchi walijitokeza kwenye mkutano huo unaofanyika kwenye uwanja wa Sabasaba Ilemela Jijini Mwanza na kukutana na mlipuko mkubwa wa injili kutoka kwa watumishi wa Mungu akiwemo mwinjilisti Rojas Matias kutoka Marekani chini ya huduma ya MORE International Ministry.

Aidha waimbaji Ambwene Mwasongwe, Mbilikimo Watatu, Samwel Lusekelo, Joseph Rwiza, Sam D, Havillah Gospel Singers na wengine wengi wameendelea kukonga nyoyo za wahudhuriaji kwenye mkutano huo.

“Maandalizi ya mkutano huu ni ya kuvutia, tuna majukwaa matatu makubwa, vyombo vya muziki wa injili vizuri na pia tunatoa zawadi mbalimbali ikiwemo vyakula na nguo kwa wanaohudhuria mkutano huu”. Alisema Mchungaji Dkt.Kulola na kuwahimiza watu wote kufika kwenye mkutano huo ili wakutane na nguvu ya Mungu na kufunguliwa.


Mkutano huo ulianza juzi jumatano Septemba 27 na utafikia tamati jumapili Oktoba Mosi, 2017 katika Uwanja wa Sabasaba Ilemela Jijini Mwanza ambapo mamia ya wananchi waliokuwa wakiteswa na majini pamoja na magonjwa mbalimbali wanazidi kufunguliwa, na leo huduma ya maombezi inaanza mapema majira ya saa nne asubuhi na mkutano utaanza saa tisa alasiri hadi saa 12 jioni.
Mwinjilisti Rojas Matias kutoka Marekani akihubiri kwenye mkutano huo
Watumishi mbalimbali wakiendelea kutoa huduma ya maombezi jana ambapo zaidi ya 20 walifunguliwa mapepo huku wengine wengi wakiponywa magonjwa mbalimbali
Mwimbaji wa muziki wa injili Ambwene Mwasongwe kutoka Dar es salaam akihudumu kwenye mkutano ho
Baada ya ibada, kanisa la EAGT Lumala Mpya kwa kushirikiana na wachungaji kutoka Marekani lilitoa zawadi kwa wananchi
Tazama picha zaidi HAPA

WATANZANIA WANG'ARA SHINDANO LA MWANDISHI BORA WA SAYANSI NA KILIMO AFRIKA

 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Uganda na Mjumbe wa Bodi ya ASARECA, Dr. Ambrose Agona (kushoto), akimkabidhi cheti Mwandishi wa Star Tv Dino Mgunda kuwa mshindi wa pili kwa waandishi wa Televisheni kwenye shindano hilo lililofanyika jana nchini Uganda.

 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Uganda na Mjumbe wa Bodi ya ASARECA, Dr. Ambrose Agona, akimkabidhi cheti Mwandishi wa Tanzania Koleta Makulwa kutoka Radio Free Afrika ambaye alipata tuzo na kuwashinda wenzake ambao walikuwa wanashindana katika eneo la Radio.
 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Uganda na Mjumbe wa Bodi ya ASARECA, Dr. Ambrose Agona, akimkabidhi cheti Mwandishi wa Tanzania wa gazeti la Guardian, Gerald Kitabu ambae alishinda tuzo ya umahiri wa habari za sayansi katika eneo la magazeti huku akiwaashinda waandishi wengine kutoka nchi zingine saba za Afrika.  
Keki ikikatwa katika hafla hiyo

Na Mwandishi Wetu

Mwandishi wa gazeti la Guardian, Gerald Kitabu ameshinda tuzo ya umahiri wa habari za sayansi katika eneo la magazeti huku akiwaashinda waandishi wengine kutoka nchi zingine saba za Afrika.

Kitabu alikuwa anachuana na waandishi kutoka nchi za Nigeria, Burkina Faso, Ghana, Ethiopia, Kenya, Tanzania na Uganda. Shindano hilo lilifanyika jana katika Hoteli ya Speke Resort Munyonyo iliyoko nje kidogo ya jiji la Kampala.

Kwa ushindi huo, Kitabu ambaye ni mshindi wa jumla wa shindano la Tanzania, alijinyakulia kitita cha dola za marekani 1,500 pamoja na simu aina ya iPhone 7+ yenye thamani za dola za Marekani 1,200. 

Mwandishi mwingine wa Tanzania aliyepata tuzo ni Koleta Makulwa kutoka Radio Free Afrika ambaye aliwashinda waandishi wengine ambao walikuwa wanashindana katika eneo la Radio. ambapo Tanzania ilizidi kung'ara baada ya Mwandishi wa Star Tv Dino Mgunda kuwa mshindi wa pili katika waandishi wa televisheni. 

Koleta aliondoka na kitita cha dola za Marekani  1,500, simu aina ya iPhone 7+ ya thamani ya dola za marekani  1,200 wakati  Dino Mgunda alipata zawadi ya dola za marekani  1,000 na simu ya iPhone7+  ya thamani ya dola za marekani 1,000.

Katika shindano hilo jumla ya waandishi 20 waliwakilisha nchi hizo. waandishi hao ni wale ambao walikuwa washindi katika shindano la nchi mahalia, shindano ambalo lilifanyika mwanzoni mwa wiki hii katika nchi hizo ikiwemo tanzania. 

Shindano hilo liliandaliwa na Jukwaa la wazi la Bioteknolojia za Kilimo (OFAB) ambalo linahamasisha matumizi ya bioteknolojia katika kilimo ili kuwezesha nchi za Afrika ziweze kujitosheleza kwa chakula.

Mshindi wa jumla katika shindano hilo la jana ni  mtangazaji wa kituo cha  TVC, Omolara Afolayan kutoka Nigeria. Washindi waliteuliwa na jopo la majai watano.

HATIMAYE WANANCHI WANAOTAKIWA KUPISHA MRADI WA SHANTA GOLD MINE WILAYANI IKUNGI WATEKELEZEWA MALIPO YAO

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliowahusisha wananchi wa Kijiji cha Mang’onyi, Sambaru na Mulumbi kwa ajili ya kulipa fidia za wanufaika kwa ajili ya kupisha Mradi wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Gold Mining Ltd.
Wananchi wa Kijiji cha Mang’onyi, Sambaru na Mulumbi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kulipwa fidia za wanufaika kwa ajili ya kupisha Mradi wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Gold Mining Ltd.
Meneja wa Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Shanta Gold Mining Ltd Philbert Rweyemamu akielezea utaratibu wa ulipaji fidia kwa wanufaika.
Wananchi wa Kijiji cha Mang’onyi, Sambaru na Mulumbi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kulipwa fidia za wanufaika kwa ajili ya kupisha Mradi wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Gold Mining Ltd.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akisalimiana na Meneja wa Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Shanta Gold Mining Ltd Philbert Rweyemamu mara baada ya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kulipwa fidia za wanufaika kwa ajili ya kupisha Mradi wa uchimbaji madini.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akisalimiana na wananchi mara baada ya mkutano wa hadhara kwa ajili ya kulipwa fidia za wanufaika kwa ajili ya kupisha Mradi wa uchimbaji madini.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliowahusisha wananchi wa Kijiji cha Mang’onyi, Sambaru na Mulumbi kwa ajili ya kulipa fidia za wanufaika kwa ajili ya kupisha Mradi wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Gold Mining Ltd.
Wananchi wa Kijiji cha Mang’onyi, Sambaru na Mulumbi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kulipwa fidia za wanufaika kwa ajili ya kupisha Mradi wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Gold Mining Ltd. 



Na Mathias Canal, Singida


Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya dhahabu (Shanta Gold Mining Limited) iliyopo katika kijiji cha Sambaru Kata ya Mang’onyi Wilayani Ikungi, Mkoani Singida huenda ikaanza uchimbaji wa madini ya dhahabu hivi karibuni baada ya kuanza kulipa fidia ya zaidi ya Bilioni 1.6 wanufaika wa awamu ya pili inayohusisha wananchi kutoka Vijiji vitatu vya Mang'onyi, Sambaru na Mulumbi.


Kampuni hiyo tayari imekamilisha ulipaji wa awamu ya kwanza kwa kulipa zaidi ya Milioni 900.2 Wanufaika waliolipwa fedha hizo wanaotokana na mazoezi mawili ya uthamini yaliyofanywa kwenye eneo la mradi kwa ajili ya upanuzi wa kambi.


Malipo hayo yatakamilisha umiliki wa maeneo hayo kwa Kampuni ya Shanta Gold mining kwa ajili ya uchimbaji na kuwafanya wananchi hao kupisha mradi wa uchimbaji dhahabu pasina kinyongo chochote.


Malipo hayo ya awamu ya pili na ile ya kwanza yamelipwa kwa wanufaika wote wa fidia katika Vijiji vyote vilivyopo Katika Kata ya Mang'onyi yanaondoa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa maeneo mbalimbali waliopo kwenye eneo la mradi huo waliotaka kufahamu hatima ya malipo yao.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliowahusisha wananchi wa Kijiji cha Mang’onyi na wawakilishi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Shanta Gold Mining Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu alisema kuwa kampuni hiyo inapaswa kutumia muda mfupi katika ulipaji wa fidia kama ilivyofanya katika awamu ya kwanza.


Alisema kuwa Kampuni hiyo ya uchimbaji imeanza kutekeleza sheria ya madini inayoelekeza miezi sita kabla ya kuanza uchimbaji wawekezaji wanapaswa kuanza kulipa fidia.


Naye Meneja wa Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Shanta Gold Mining Ltd Philbert Rweyemamu alisema kuwa kampuni yake imeanza kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu mwezi Disemba 2016 ya kuwalipa wanufaika hao fidia ambayo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa mradi huo.


Alisema kuwa malipo yanafanywa na kampuni hiyo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya sambamba na wenyeviti wa serikali za vijiji vyote vilivyopo ndani ya mradi.


Kuanza kwa uchimbaji wa madini katika eneo hilo kutaibua ajira nyingi kwa wananchi Wilayani Ikungi na Taifa kwa ujumla jambo litakalosaidia ukuzaji wa pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake.


Katika Awamu ya Kwanza Kampuni ya Shanta Gold Mining Ltd iliwalipa wanufaika 92 wenye umiliki wa Viwanja 121 thamani yake ikiwa ni Shilingi 902,412,247.00 Hulu awamu hii ya Pili wakilipwa Wamiliki 114 wenye Viwanja 156 vyenye thamani ya Shilingi 1,663,112,018.01


Aidha, Kuanzia leo Septemba, 2017 wanufaika wa fidia wameanza kufanya uhakiki wa malipo yao na ufunguaji Akaunti kwa ajili ya malipo ikiwa ni matakwa ya kisheria.


Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji Cha Mang'onyi Ndg Mohamed H. Ramadhani alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu kwa kutoa maagizo ya kulipwa haraka fidia za kila wanufaika Jambo ambalo limetekelezeka kwa haraka katika kipindi Cha muda mfupi.


Sambamba na hayo aliongeza kuwa Mkuu huyo wa Wilaya anafanya kazi kubwa katika kuwaunganisha wananchi wote ili kupata stahiki zao na kufurahia Rasilimali za Nchi yao.


MWISHO

SEKTA YA MANUNUZI YA MTANDAONI NA CHANGAMOTO ZAKE NCHINI TANZANIA

Na Jumia Travel Tanzania

Miongoni mwa sekta ambazo zimewapatia utajiri mkubwa wafanyabiashara mbalimbali duniani ni pamoja na biashara kwa njia ya mtandao. Leo hii ukiyataja majina ya kampuni kama vile Alibaba au Amazon ni watu wachache wasioyafahamu licha ya kutokuwepo nchini Tanzania. Waasisi wa makampuni hayo wamo kwenye orodha ya watu matajiri duniani, Bw. Jeff Bezos mwasisi wa Amazon ni tajiri nambari 3 huku Jack Ma ambaye ni mwasisi wa Alibaba yeye ni tajiri nambari 23.
Utajiri wa wafanyabiashara hawa sio kama wanamiliki biashara katika nchi mbalimbali bali uwezo wa makampuni yao kuwafikia wateja mahali popote walipo. Kuwafikia wateja hao Jumia Travel ingependa kukufahamisha si kwa njia nyingine bali ni kupitia mtandao wa intaneti. 

DAWA NI KULALAMIKA AU KUCHUKUA HATUA?

Image may contain: 1 person, sittingNa Emmanuel J. Shilatu 

Mara nyingi Rais Magufuli amekuwa akitoa kauli akisisitiza Watu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili wajiimarishie kipato binafsi. Watu wanapolalamika kuwa maisha ni magumu, hakuna pesa mitaani jibu analolitoa Rais Magufuli anasisitiza Watu kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupambana na hali ya maisha iliyopo.

Rais Magufuli sio kiongozi wa kwanza nchini kusisitiza juu ya Wananchi kufanya kazi kwa bidii. Kumbukumbu zinaonyesha hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere naye pia alikuwa akisisitiza juu ya Watu kufanya kazi kwa bidii.

Wakati tunapata uhuru wetu mwaka 1961 kutoka kwa Waingereza kila Mtanganyika alikuwa na maana yake kichwani ya kuelewa nini maana ya uhuru. Wapo walioamini kuwa huo ndio utakuwa mwisho wa ubaguzi wa rangi, hadhi, kabila uliokuwa ukifanywa na Wakoloni; wengine waliamini kupata uhuru ni kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu, nyonyaji na za kidhalimu za Wakoloni.

Licha ya mawazo mazuri waliyokuwa nayo baadhi yao, lakini kwa upande wa mwasisi mwenyewe wa uhuru wetu alikuwa na mtazamo tofauti kabisa na zilivyokuwa mawazo ya watu. Yeye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa na maana ya kipekee kabisa juu ya dhana nzima ya uhuru.

Kwa upande wa Baba wa Taifa letu Mwalimu Nyerere aliamini na kusema ya kuwa “tumefanikiwa kuwaondoa Wakoloni na hivyo tupo huru. Na uhuru maana yake ni kazi”. Mwisho wa kunukuu.

Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa na maana ili tuweze kupiga hatua kimaendeleo ni lazima tuutumie huu uhuru wetu vilivyo katika kupiga hatua kimaendeleo kupitia kufanya kazi kwa bidii na maarifa yetu yote ili kuleta maboresho ya kina katika Nyanja zote zile za kimaisha yaani uchumi, kijamii na kisiasa. Bila ya kufanya kazi kwa bidii, uhuru wetu ni sawa na mzoga.

Na ndio maana Mwalimu Nyerere kama kiongozi alianza kwa kuonyesha mfano wa dhahiri wa kuanzisha mapambano kwa vitendo dhidi ya maadui zetu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

Sehemu kubwa ya mafanikio yake yalitokana ama ni kupitia kuanzisha maazimio, mashirika, kauli mbiu na sera mbalimbali. Hayo yote aliyafanya kwa vitendo zaidi na si porojo, lawama, maandamano, wala manung’uniko.

Pia Mwalimu Nyerere alikuwa na falsafa ama dhana ya kimaendeleo ambapo aliamini maendeleo sahihi hayawezi yakapatikana nje ya uwepo wa mambo makuu manne ambayo ni “watu”, “ardhi”, “siasa safi” na “uongozi bora”.

Naam!! “Watu” ni kiungo kimoja wapo kikuu cha hakikisho la maendeleo chanya yeyote yale ndani ya familia, jamii ama Taifa kwa ujumla wake. Mathalani, endapo tutakuwa na miundombinu bora ni watu ndio wamechangia uwepo wake; ama kama tutakuwa na mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula, biashara na kiada basi ujue ni watu wameweka jitihada za kutosha.

Halikadhalika kama kuna amani na utulivu nchini basi ujue ni watu wamechangia hilo. Jamani, hata Wahenga walisema: “usione vyaelea, ujue vimeundwa”, na waundaji wenyewe ni Wananchi (mimi, wewe na Yule).

Licha ya uwepo wa utajiri wa nguvu kazi takribani Watu Milioni 50 lakini bado watu hao hao ndani ya jamii wanachojua wao ni utegemezi pekee. Kivipi?

Kwa jinsi tuanavyoishi utadhani tunawangojea baadhi ya watu kutoka nje ya nchi ili waje watuletee maendeleo kwetu yaani imefika kipindi kwa mtu hata kutandika kitanda chake mwenyewe anacholalia imekuwa ni kazi kubwa kwake.

Kuna kipindi ulitolewa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) uliobaini asilimia 71 ya Watanzania wanatumia muda mwingi kufanya shughuli zisizokuwa za uzalishaji mali wala tija kwa Taifa hasa za kufanya starehe mbalimbali.

Hii ni hatari sana na inaonyesha namna gani baadhi ya Watanzania tusivyojitambua. Kikubwa ambacho kinaonekana ni kujikita mizizi ya dhana nzima ya kibaguzi iliyojengeka akilini ama kwenye mitazamo ya watu ambapo tumediriki kuwaachia viongozi pekee huku tukijiengua katika kapu la dhana ya neno “serikali” wakati kiuhalisia na kimaantiki na Wananchi nao pia ni sehemu ya Serikali.
Ni kweli kabisa kwamba Serikali ni chombo cha utawala kilichoshika dola ama nchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo Wananchi. Na wanaoiwezesha ama kuipa mamlaka hayo Serikali ni Wananchi. Bila ya watu hakuna serikali na pia Serikali haina uhalali wa kuwepo bila ya kuwepo kwa watu.

Na kundi lingine linalounda Serikali ni viongozi. Hivyo Serikali ni muunganiko kati ya viongozi na Wananchi. Daima na tena ni dhambi kubwa sana kuwatenganisha makundi haya (Wananchi na viongozi) katika chungu hiki Serikali.

Wananchi siku hizi wamekuwa washadidiaji wakubwa wa siasa na bila ya wao kujitambua ya kwamba hutumia muda mwingi sana kushindia na kulalia katika dimbwi la porojo za kisiasa bila ya kujibidiisha. Maendeleo yatapatikanaje bila ya sisi wenyewe kujishughulisha?

Utakuta vijana walio wengi kutwa wanashinda kwenye kucheza “pool table” na kukaa vijiweni tu; Wazee ama akina Baba nao kutwa wanacheza “bao” ama “draft” tu; na akina Mama nao kila kukicha wapo vibarazani wakisutana na kupashana umbea tu. Hayo ndio maisha ya kila siku ya baadhi ya wanajamii ya kutokupenda kufanya kazi kwa bidii.

Mwananchi huyo huyo anaitegemea Serikali ije impatie fedha mikononi bila ya yeye kujishughulisha kwa kufanya kazi yeyote ile ya kumpa kipato. Hakuna Serikali yeyote ile duniani inayoweza kuwapatia wananchi wake pesa lukuki bila ya wao kujishughulisha.

Kama hauamini, jaribu kufanya utafiti katika nchi zilizoendelea utakubaliana nami kuwa hakuna Taifa lolote lile lenye raia wasiojibidiisha kwa kutegemea mteremko kutoka kwa Serikali zao. Yatazame mataifa kama ya Marekani, Uingereza, China au Urusi wakazi wake wanavyotambua ya kuwa thamani ya pesa yao na uchumi wa nchi unategemea zaidi ni kwa jinsi gani watu wa ndani (wao wenyewe) wanavyozalisha mali.

Lakini sie hatujitambui na tupo bize kwa kujiteketeza na porojo kila uchwao. Hapa tumesaliti Mwalimu Nyerere na alivyoamini maana ya uhurukuwa ni kufanya kazi kwa bidii, umasikini hautatuacha kweli? Nani wa kulaumiwa ni serikali na viongozi wake ama ni sisi Wananchi?

Hii yote inatokana na jamii kuziasi mitazamo miongozo na falsafa za Mwalimu Nyerere (mathalani ile ya “Uhuru ni kazi”) hali inayosababisha kiwango cha idadi ya watu maskini kuzidi kukua nchini licha ya kujaariwa rasilimali na mali za asili kwa kuyachakachua maendeleo yetu wenyewe. Kisa? Porojo kutawala maisha yetu.

Tusiishie kuwalaumu tu Viongozi wetu kila kukicha huku tukisahau jinsi sisi tulivyo wavivu sana wa kupindukia. Watanzania tulio wengi hatupendi kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu. Watanzania tulio wengi hatupendi njia nyoofu na sahihi badala yake tunapenda njia ya mkato ya kujipatia vipato vyetu. Watanzania wengi tunapenda sana kufanya madili, ama “michongo” kama wanavyoita watoto wa mjini.

Kwenye salam zao ama maongezi mengi ya Watanzania ni nadra sana kukosa kusikia maneno kama vile “mambo mengine niaje, ishu vipi ama madili yakoje”. Ni dhahiri kuwa hapa inatafutwa njia ya mkato ya mafanikio katika maisha. Hali hii huzaa matokeo endelevu mabovu ndani ya jamii kama vile utapeli; ujambazi; ongezeko la mihadarati na madawa ya kulevya; mauaji ya maalbino na vikongwe; pamoja na uchafu ama uozo mwingine kadha wa kadha unaofanana na huo.

Chanzo haswa cha uwepo wa utafutaji mambo kwa njia ya mkato halijasababishwa na Viongozi ndani ya Serikali bali msingi wake mkuu niWatu tulio wengi kutaka matokeo chanya yenye faida na matunda kwa haraka na hata pia kukata tama ya kimaisha kwa haraka zaidi kutokana na kujinyima fursa ya uvumilivu na ustahimilifu ndani yetu.

Mapambano ya maisha ni sawa na vita kali ambapo si tu jukumu la viongozi bali hata nasi Wananchi tuna wajibu mkubwa wa kufanya kazi kwa bidii na si kulalama tu kila kukicha.

Kuna usemi mmoja unaosema “Wanaofanikiwa zaidi ni wale walioshindwa mara nyingi” Je utashindwaje, kama hujajaribu mara nyingi? Je mafanikio katika maisha yanapatikana kwa mara moja tu? Haya ni maswali muhimu na ya msingi sana kwa Watanzania, kujiuliza.

Ifike mahali tujitambue ya kwamba kelele, tuhuma, lawama, dharau kwa viongozi wetu hazitatusaidia endapo sisi kwa sisi hatujaamua kujibidisha ipasavyo. Utakuta ndani ya jamii fulani tupo zaidi ya watu laki mbili lakini tunamtegemea kiongozi mmoja tu awe ni Mbunge ama Diwani ili aweze kutuletea maendeleo. Endapo sisi tulio wengi tumeshindwa kuwa kitu kimoja wenye nia moja ya umoja, mshikamano na tukaamua kwa dhati kujiletea maendeleo; Je, kiongozi mmoja pekee atawezaje?

Ndugu zangu, kwanini alaumiwe dobi kutakasa kaniki wakati tunajua rangi ya kaniki? Ni lazima tutambue ya kwamba sisi raia pia tunahusika vilivyo na huu umaskini wetu na si vyema kuwasukumizia mzigo wote wa lawama viongozi wetu pekee. Watanzania tulio wengi tunapoteza muda mwingi kwa kukaa vijiweni, kushabikia siasa tu, kupiga soga na kucheza bao muda wote. Je, tukiamua kujishughulisha kwa kuutumia muda huo ipasavyo tungekuwa wapi kimaendeleo hivi sasa?
Waswahili walisema usimuhadithie mtu ndoto yako uliyoota jana usiku lakini hapa ni kinyume kwani siri tunasema na bayana tunaambizana. 

Binafsi huwa Napata ukakasi pindi nionapo Serikali ina sera na majukumu lukuki lakini Watanzania tulio wengi hatushiriki vyema na hata hatutimizi wajibu wetu kwa wakati. Mwenye jukumu la kulifuatilia Taifa letu kwa ukaribu na utendaji ni serikali pekee ama na Wananchi pia? Je, kwa uwajibikaji huu, maisha bora kwa kila Mtanzania yatapatikana kweli?

Mara nyingi sera tulizonazo zinategemea zaidi umoja, mshikamano, ushirikiano na nia ya dhati ya uwajibikaji wa pamoja kiutekelezwaji. Kamwe maisha bora kwa kila Mtanzania hayaji kwa kuota au kupiga soga ama kwa kungojea mpaka uone Tanzania (nchi yako) imekufanyia nini na badala yake ujiulize wewe mwenyewe umeifanyia nini Tanzania?

Kuna wanamapinduzi, wanaharakati na watu mashuhuri wengi tu hapa Duniani ambao hawakungoja mpaka waone nchi zao zimewafanyia nini na badala yake walijiuliza wamezifanyia nini nchi zao?
Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela, Martin Luther King Jnr, Kwame Nkurumah, Chifu Mkwawa ni baadhi tu ya Wanaharakati na wakombozi wa kweli dhidi ya Uhuru na ubaguzi wa ngozi nyeusi ambao milele na milele watabakia kuwa ni mashujaa maarufu wa ulimwengu. Jiulize mwenyewe wewe je utakumbukwa, ama tutajivunia nini kutoka kwako? Je, ni kwa huo ugoigoi wako ama kwa uwajibikaji wako?

Tuache uvivu na tujitume vilivyo kwa kuchangamkia fursa na Baraka tulizojaaliwa. Mungu ametujaalia wingi wa ardhi yenye rutuba ifaayo kwa kilimo, misitu, wanyama pori na vyanzo vingi vya kujiletea maendeleo.

Hata kama Rais John Pombe Magufuli ni mzuri kiasi gani hatoweza kuleta maendeleo tarajiwa kwa Watu endapo sisi wenyewe Watanzania (Watu) hatutafanya kazi kwa bidii na badala yake tutasikia uchumi wa Taifa umekuwa lakini pato binafsi la Mtanzania likiendelea kushuka. Dawa ya kukuza mapato binafsi ni kwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuzichangamkia fursa za kiuchumi tulizojaaliwa.

Tanzania isiyo na maradhi inawezekana; Tanzania yenye uchumi imara mpaka kwa Wananchi wake inawezekana; Tanzania yenye huduma bora zaidi za kijamii inawezekana; Hakika Tanzania yenye maisha bora zaidi pia inawezekana. Hii itawezekana tu endapo kila mmoja wetu atatimiza wajibu ipasavyo kwake na kwa Taifa lake. Tuache kulalamika tu, tuanze kuchukua hatua ya kujituma kutimiza wajibu wetu ipasavyo wa kufanya kazi kwa bidii.

0767488622


Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More