Friday, November 20, 2015

Lipumba Amtahadharisha Rais Magufuli Kuhusu Dr. Shein Kuhudhiria Bungeni Leo

Wakati Rais John Magufuli akitarajiwa kuzindua na kulihutubia Bunge leo, ametahadharishwa kutoambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa maelezo kuwa si rais halali wa Zanzibar kikatiba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Profesa Ibrahim Lipumba alisema Zanzibar haina Rais, hivyo kiongozi huyo kushiriki Bunge kwa nafasi hiyo ni kuvunja Katiba ya nchi.

Profesa Lipumba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha CUF, ameungana na msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walioutoa mjini Dodoma juzi wakidai kuwa Dk Shein hapaswi kuingia kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Magufuli atakapohutubia.

Alishauri endapo kuna ulazima wa Rais wa Zanzibar kuhudhuria, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itangaze matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais wa Zanzibar na rais aliyeshinda aapishwe.

Lipumba pia amemtaka Rais Magufuli kutumia nafasi yake ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Tanzania kuishauri ZEC kurejea matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 na kumtangaza mshindi.

“Wazanzibari hawawezi kuruhusu uchaguzi kurudiwa, ” alisema Lipumba.

Alisema anashangazwa na hatua ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuondoka madarakani na kumwachia Magufuli mgogoro wa Zanzibar. Alisema Kikwete alipaswa kuhakikisha matokeo yanatangazwa na mshindi anaapishwa.

Alisema Kikwete alipoingia madarakani alionyesha kusononeshwa na mgogoro wa Zanzibar na kuahidi kuupatia ufumbuzi wa kudumu lakini inashangaza kuona akiondoka madarakani huku kukiwa na mgogoro mkubwa.

“Ninamuomba Rais Magufuli asilifumbie macho suala hili, awaeleze wenzake wa CCM waache kumuwekea vikwazo katika kipindi chake hiki cha kuliongoza Taifa,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kuiminya demokrasia Zanzibar ni kuwapa fursa watu wenye itikadi kali kuwashawishi Wazanzibari hasa vijana kuamini kuwa hawawezi kupata haki kwa kupitia sanduku la kura.

Alisema endapo kauli ya Wazanzibari kupitia kura zao haitaheshimiwa, wananchi wake watapoteza imani kuwa hawawezi kupata mabadiliko kwa njia ya kidemokrasia.

“Hili ni jambo la hatari sana, si kwa Wazanzibari pekee, bali kwa Watanzania wote na ukanda mzima wa Afrika Mashariki…tusijenge mazingira ya kuwapa fursa watu wanaotaka mabadiliko kwa njia haramu,” alisema Lipumba.

Alisema kitendo cha CCM kukataa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kinaweza kuliingiza Taifa kwenye mgogoro wa kisiasa na kiusalama, Magufuli akatae kupelekwa huko,” alisema Profesa Lipumba.

Akizungumzia mtazamo wake juu ya Serikali ya Magufuli, Profesa Lipumba alisema ameanza vizuri kwa kutamka nia yake ya kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kupiga marufuku safari za nje.

Alisema hatua hiyo ni ishara kuwa ataweza kuwatumikia Watanzania kwa moyo.

Alimtaka Rais Magufuli kutekeleza dhamiri yake ya kupambana na ufisadi kwa kuwafungulia mashtaka na kuwafunga wote waliochota fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow. 
 
“Ni vema pia akaunda baraza dogo la mawaziri na ajiwekee vipaumbele vichache vyenye tija kwa Taifa na wananchi atakavyoweza kuvisimamia kwa karibu,” alishauri Lipumba.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More