Tuesday, November 17, 2015

Mtu Mwingine Auawa Kinyama Geita... kifo chake Utata Mtupu

Mtu ambaye hajafahamika jina wala makazi, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Katoro wilayani Geita, baada ya kufikishwa na polisi akiwa hajitambui.

Mtu huyo anasadikika kupigwa na watu wasiojulikana Jumamosi saa mbili usiku, huku tukio hilo likihusishwa na chuki za kisiasa zinazohusiana na vurugu zilizosababisha kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Daniel Izengo alisema 
saa 2:30 usiku walimpokea mtu huyo aliyefikishwa na polisi akiwa na majeraha makubwa sehemu za kichwani.

Awali, mganga huyo alisema watu wawili walijeruhiwa katika vurugu zilizosababisha kifo cha Mawazo ambao walifikishwa kwenye kituo hicho wakatibiwa na kuruhusiwa.

Pia alisema watu watatu walifikishwa kituoni hapo juzi akiwamo Mawazo, Elizabeth Paschal (48) na Bahati Michael (38) wote wakiwa wakazi wa Katoro.

Dk Izengo alisema hali ya Mawazo ilibadilika na 
kumwandikia rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Geita ambako alifariki dunia, huku majeruhi wengine wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa baada ya hali zao kuridhisha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Lotson Mponjoli alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea, ikiwamo kuwatafuta watuhumiwa.

Hilo ni tukio la pili ndani ya siku chache, la kwanza likiwa la kifo cha Mawazo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More