Thursday, March 14, 2024

ADEM YAWAPIGA MSASA WALIMU WAKUU 4,620 WA MIKOA 6 TANZANIA BARA

Katibu Tawala Wilaya ya Nachingwea Mbarouk Balozi amefunga mafunzo  ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule za msingi yaliyoendeshwa kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi za Mikoa wa Simiyu, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara chini ya mradi wa BOOST na kusimamiwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM)
Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi -ADEM Dkt. Alphonce Amuli ameeleza kuwa hadi sasa ADEM imeshatoa mafunzo kwa walimu wakuu 4,522 katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo, na katika awamu hii mafunzo hayo yametolewa kwa Walimu Wakuu 4,620 katika Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Simiyu, Mbeya, Kigoma na Mtwara
Baadhi ya walimu wakuu walioshiriki mafunzo hayo



Na Fredy Mgunda,Lindi

Katibu Tawala Wilaya ya Nachingwea Mbarouk Balozi amefunga mafunzo  ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shule za msingi yaliyoendeshwa kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi za Mikoa wa Simiyu, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara chini ya mradi wa BOOST na kusimamiwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM).

 

Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo, Balozi amewataka walimu hao kwenda kuboresha utendaji kazi katika vituo vyao vya kazi kwa kihakikisha wanasimamia kikamilifu shughuli za ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa ubora.

 

"ADEM imemaliza kazi yake ya kuendesha mafunzo haya kwa walimu wakuu katika Mikoa sita nchini, ni wajibu wa Walimu Wakuu mliopatiwa mafunzo haya kwenda kuyatumia katika utendaji wenu wa kila siku ili kufikia adhma ya Serikali ya kuboresha elimumsingi nchini" Amesema. Balozi

 

Balozi aliwataka Walimu Wakuu kuongoza shule kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma na kusimamia miradi ya elimu wanayotakiwa kusimamia kwa ufanisi kwani kupitia mafunzo hayo wamejengewa uwezo kuhusu usimamizi wa rasilimali za shule hususani fedha na miradi ya ujenzi inayotekelezwa shuleni.

 

Balozi alimalizia kwa kuupongeza uongozi wa ADEM kwa kuendesha mafunzo hayo kwa umahiri mkubwa na kuwataka kuendelea kuendesha mafunzo hayo kwa umahiri huo huo katika Mikoa iliyobaki.

 

Nae Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi -ADEM Dkt. Alphonce Amuli ameeleza kuwa hadi sasa ADEM imeshatoa mafunzo kwa walimu wakuu 4,522 katika awamu ya kwanza ya mafunzo hayo, na katika awamu hii mafunzo hayo yametolewa kwa Walimu Wakuu 4,620 katika Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Simiyu, Mbeya, Kigoma na Mtwara kuanzia februari 15 hadi machi 13, 2024.

 

Dkt. Amuli aliwataka walimu kutumia mafunzo hayo katika kuboresha utendaji na usimamizi wa shule ili kuleta tija na thamani ya fedha iliyotumika kuyaendesha ionekane.

 

alisema kuwa Lengo la mafunzo ni kumjengea uwezo Mwalimu Mkuu kutekeleza majukumu yake ya kusimamia shule hususani katika kuhakikisha shughuli za shule zinafanyika kwa ubora na ufanisi unaotakiwa. Mwalimu Mkuu ni mtendaji muhimu katika ngazi ya shule.

 

Dkt. Amuli alisema kuwa baada ya mafunzo hayo, washiriki watafuatiliwa na kupimwa katika maeneo yote waliyowezeshwa,Miongoni mwa viashiria vya utekelezaji wa mafunzo kwa Mwalimu Mkuu ni pamoja na uwepo wa taarifa zifuatazo,Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule,Mpango wa kushughulikia malalamiko kwa Watumishi, wanafunzi na jamii,Mpango wa Motisha kwa wafanyakazi na wanafunzi,Miundombinu bora ya shule,Matokeo chanya ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni.


Thursday, October 5, 2023

DED MAKUFWE AWANOA WASIMAMIZI WA MIRADI YA ELIMU NA AFYA MAKETE.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete,  Ndg. William Makufwe (kushoto) akizungumza na Wasimamizi wa miradi ya Elimu na Afya, katika ukumbi wa Mikutano Bomani...akiwa pamoja Mganga mkuu wa Halmashauri Dkt. Ligobert Kalisa.

Na Fredy Mgunda, Makete.


MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete,William Makufwe, amewataka watumishi kuanzia ngazi ya kijiji hadi makao mkuu ya Halmashauri, ambao wanasimamia miradi kuhakikisha watimiza wajibu wao ili iweze kukamiliaka kwa wakati.

Makufwe amesema hayo wakati akizungumza na watendaji wa kata, vijiji, wakuu wa shule , waganga wafawidhi pamoja na wakuu wa idara na vitengo katika ukumbi wa mikutano Bomani,lazima viongozi washirikiane katika kukamilisha miradi ambayo imeletwa katika maeneo yao.

“hakikisheni mnashirikiana katika kukamilisha miradi sio kuachiana, kila mmoja ashiriki kikamilifu, hasa watendaji wa kata mnatakiwa kushirikiana moja moja katika kila mradi ambao unatekelezwa katika kata au kijiji husika, ili miradi ikamilike kwa wakati”

Amewataka watendaji kata pamaoja na wahusika wengine, kutoingiza maslahi binafsi katika utafutaji wa mafundi ambao watakuwa wakitekeleza ujenzi wa miradi ya serikali ili waweze kusimamiwa vizuri.

“hakikisheni mhandisi wa wilaya anashirikishwa katika utafutaji wa mafundi ambao wataenda kutekeleza miradi hiyo ya serikali ili kuwe na ufanisi katika ujenzi” alisema Makufwe

Sambamba na hayo DED Makufwe amewataka wasimamizi wa miradi, kufanya manunuzi kwa wakati kwasabu serikali imetoa pesa za kutosha, hivyo kila mtu awajibike kwa nafasi yake ili miradi iweze kukamilika kwa wakati,

 Makufwe amewata wasimamizi hao wa miradi kutunza vifaa vyote ambavyo vimenunuliwa kwaajili ya ujenzi.

Hata hivyo, amewasisitiza watumishi hao kuhakikisha wanafuata utaratibu katika ufanyaji wa manunuzi ili kutoingia katika matatizo na serikali, ikiwa ni pamoja na kufanya manunuzi kwa idhini ya wahusika hususani kitengo cha manunuzi.

“hakikisheni mnashindanisha bei za bidhaa ambazo mnataka kuzinunua ili mpate bei ambazo zinaeleweka, sio kwasababu una mahusiano na mdau fulani basi unampa tenda”.

Kwa upande mwingine, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi katika kuendeleza miradi ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja kama vile , Elimu na Afya ili kuhakikisha watanzania wanapata huduma stahiki na bora.

Thursday, July 22, 2021





Na Fredy Mgunda,Irnga.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amesema kuwa wakandarasi watakao chelewesha au kujenga chini ya kiwango miradi ya kimaendeleo katika halmashauri ya Manispaa ya Iringa watarudia kwa gharama zao kwa ubora ule ule unatakiwa kutokana na thamani ya mradi husika.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya kimaendeleo katika manispaa ya Iringa, mkuu wa wilaya Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa amefanikiwa kukagua miradi mingi ambayo imejengwa kwa viwango vinavyotakiwa ila tatizo kubwa lipo kwa wakandarasi ambao wamekuwa wakipewa tenda za ujenzi wa miradi hiyo.

alisema kuwa wakati wa ziara aligundua kuwa wakandarasi wengi wameshalipwa fedha serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya serikali ila wamekuwa wanaichelewesha kwa makusudi na kusababisha kuchelewa kuanza kufanya kazi kwa miradi hiyo.

Moyo alisema kuwa miradi mingi ilijengwa kwenye halmashauri ya Manispaa ya Iringa imejengwa kwa ubora unatakiwa kulingana na thamani ya fedha iliyotakiwa kutumika katika mradi husika.

Alisema kuwa watendaji wa Manispaa ya Iringa wanatakiwa kusimamia vilivyo fedha ambazo zinakuwa zinatolewa kwa ajili ya miradi ya kimaendeleo ili kusaidia kuwa na miradi iliyojengwa kwa viwango bora.

Moyo aliwataka wananchi wa manispaa ya Iringa kuhakikisha wanatunza miundombinu ya miradi ambayo imejengwa kwenye mitaa yao ili kuhakikisha miradi hiyo inatoa manufaa ambayo yamekusudiwa na serikali ya kuchangia kukuza maendeleo.

Mkuu huyo wa wilaya ya Iringa alifanikiwa kutembelea mbalimbali kama vile kukagua ujenzi wa choo cha zahanati ya Kitanzini,kukagua shule ya msingi Azimio,ujenzi wa choo cha shule ya msingi chemchem,ujenzi wa jengo la zahanati ya Itamba,ujenzi wa maabara shule ya sekondari ya Mivinjeni,ujenzi wa madarasa manne ya shule ya msingi mawelewele,ujenzi wa shule ya sekondari ya Kwakilosa na kutembelea ujenzi wa madarasa mawili shule ya msingi Njia Panda.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema kuwa wameyapokea maagizo yote yaliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo na watayafanyia kazi ili kuondoa kasoro ambazo zimejitokeza kwenye baadhi ya miradi ambayo kamati hiyo wameitembelea.

Aliwataka watendaji wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi unaotakiwa ili kutumia fedha za wananchi vizuri kuendana na mradi ambao unakuwa unatekelezwa kwenye maeneo yao.





Monday, June 14, 2021

DC KASESELA : AWATAKA KAMPUNI YA MWENGA KUTENGENEZA MITA ZA WATEJA WAKE


Kaimu mkuu wa wilaya Mufindi ambaye ni mkuu wa wilaya ya Iringa Richad Kasesela akitoa neno kwenye mkutano wa maombi ya kurekebisha bei ya umeme wa Mwenga Power Limeted katika kijiji cha Igoda kilichopo wilaya ya Mufindi
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa wadau wanaotumia umeme wa kampuni ya Mwenga


Na Fredy Mgunda,Iringa.

MKUU wa wilaya ya Mufindi ameitaka kampuni ya Mwenga Power Services Limited kutengeneza mita za wateja zilizoharibika kwa wakati ili wananchi waendelee kufanya shughuli za kimaendeleo kwa kutumia nishati ya umeme ambayo inatolewa na kampuni hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano wa maombi ya kurekebisha bei za umeme zinazotolewa na kampuni ya Mwenga,kaimu mkuu wa wilaya hiyo ambaye ni mkuu wa wilaya ya Iringa,Richad Kasesela alisema kuwa kampuni hiyo inatakiwa kutengeneza kwa wakati mita ambazo zimeharibika kwa wakati ili wananchi wasikose huduma hiyo.

Kasesela alisema kuwa jukumu la kuzitengeneza mita za umeme zilizoharibika ni jukumu la kampuni ya Mwenga Power Services limited ili kuondoa athari ambazo mteja anaweza kukutana nazo akiamua kuitengeneza yeye mwenyewe.

Alisema kuwa ni kosa kubwa kwa wananchi kutengeneza mwenyewe mita ambazo zimeharibika wakati mafundi wa kampuni ya Mwenga wapo kwa ajili ya hilo na wanajua namna ya kuzitengeneza na zisilete madhara  kwa wateja.

Kasesela aliongeza kuwa watumishi wa kampuni ya Mwenga Power Services limited wanatakiwa kutoa huduma bora kwa wateja ili kuondoa malalamiko ambayo wananchi wamekuwa wakiyatoa kwenye ofisini ya mkuu wa wilaya ya Mufindi.

Alisema kuwa nishati ya umeme inachangia kwa asilimia kubwa kukuza uchumi wa wananchi kwa kuwa wanategemea nishati hiyo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali hata kutimiza majukumu ya kuleta maendelea kwa ujumla.

Kasesela aliwapongeza mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA) kwa namna wanavyofanya kazi zao kwa kushiikiana na wananchi ili kuhakikisha wanaondoa kero  ambazo hazina msingi kwenye kuleta maendeleo na kukuza uchumu kwa wananchi.

Aidha Kasesela alimalizia kwa kuwaomba wananchi wa vijiji 32 kuendelea kutumia umeme unaozalishwa na kampuni ya Mwenga Power Services limited ambao unagharama  nafuu na unasaidia kukuza uchumi wa wananchi wa vijiji hiyo na taifa kwa ujumla.

 

kwa upande wake kaimu mkurugenzi mkuu wa EWURA,Nzinyangwa Mchany alisema kuwa ili kampuni iruhusiwe kurekebisha bei ni lazima afuate kanuni za EWURA za umeme na gesi asilia za maombi ya kupanga bei za mwaka 2017 zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2021 ambapo kuna hatua saba za kuzifuata.

Alisema kuwa wanatakiwa kupokea maombi,kupitia maombi na kuomba ufafanuzi mbalimbali kutoka kwenye mamlaka,kuweka mkutano wa hadhara(taftishi) ,kupokea maoni ya maandishi ,kufanya uchanbuzi wa kina na kuwasilisha mapendekezo kwenye bodi,kutoa maamuzi ya bodi na kutangaza maamuzi ya bodi kwenye gazeti la serikali na magazeti ya kawaida.

Mchany alisema kuwa sheria ya EWURA inasema kuwa kama kuna mtu hajaridhika na maamuzi hayo anahaki ya kukata rufaa kwenye baraza la ushindani wa haki katika biashara.

Alimalizia kwa kuwaambia wananchi kuwa maoni hayo ya marekebisho ya bei za umeme za kampuni ya Mwenga Power Services Limited kuna vikao ambavyo vitakaliwa ili kuhakikisha pande zote mbili zinaridhika kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi.

Naye  meneja wa fedha wa kampuni ya Mwenga Power Services Limited,Deograsias Massawe alisema kuwa Mwenga Power inazaidi ya kilomita 400 za laini za kusambaza umeme wenye nguvu ya gridi na umeme jadidifu katika vijiji37(vijiji 32 na 5 katika Wilaya za Mufindi na Njombe,mtawalia).

Massawe  alisema kuwa Mwenga Power inazaidi ya wateja 5,400 waliounganishiwa umeme katika Wilaya za Mufindi na Njombe na Hadi sasa Mwenga Power inatransifoma 80 za kupooza umeme huu unawafaidisha watu zaidi ya100,000 na kwa jinsi usambazaji unavyopanuka na kunatarajia kuwa faidisha watu wengi zaidi.

Alisema kuwa wanategemea kuhakikisha pande zote mbili zitanufaika kwa marekebisho hayo mapya ya bei za umeme wa kampuni ya mwenga. 

 


  

Tuesday, June 5, 2018

Chumi ashikilia shilingi kuitaka Serikali kutoa fedha za Miradi Viporo kama ilivyoahidi, Spika aokoa jahazi

Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi ameitaka serikali kutoa fedha za miradi viporo kama ilivyoahidi kwa kuwa mwaka wa fedha unaelekea mwishoni.

Chumi alitoa hoja hiyo wakati Bunge limekaa kama Kamati kujadili bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ambapo alisema kuwa, ni Serikali yenyewe ndio ilizitaka Halmashauri kuwasilisha miradi viporo ambayo mingi ilitokana na nguvu za wananchi.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Ashantu Kijaji alisema kuwa Serikali inafanya uchambuzi wa miradi hiyo ndipo itoe fedha.

Hata hivyo, Chumi alihoji ni uchambuzi gani ikiwa miradi hiyo ilianishwa na kuchambuliwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri na Tamisemi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi upi huo ambao serikali inaufanya ikiwa Halmashauri kwa kushirikiana na Tamisemi walishafanya? Naomba Waheshimiwa Wabunge mniunge mkono, tujadili jambo hili

Baada ya kauli hiyo, wabunge wengi walisimama kuunga mkono hoja. 

Hata hivyo, Spika ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti, aliitaka Serikali kuona uzito wa hoja hiyo na kwenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, jambo hili ni zito, mimi niwaombe Serikali, mlichukulie uzito unaostahili, Mheshimiwa Chumi unasemaje baada ya msisitizo huu

Akihitimisha hoja yake, Mbunge huyo wa Mafinga Mjini alisema kuwa, kwa msisitizo uliotoa Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Serikali italifanyia kazi kwa uzito huo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti umeshasema kwa msisitizo, na wewe Mwenyekiti ndiye uliyekikalia kiti, narejesha shilingi na kuisihi Serikali itoe fedha hizo ili kuongeza morali ya wananchi kujitolea katika shughuli za maendeleo

Akizungumza na mwandishi wetu baadae, Chumi alisema kuwa katika Jimbo la Mafinga Mjini waliainisha kukamilisha miradi ya ujenzi wa kituo cha Afya Bumilayinga, kukamilisha Zahanati za Kitelewasi, Kisada, Ulole na nyumba tatu za wauguzi, na ukarabati wa madarasa katika shule ya Msingi Kikombo.

Monday, June 4, 2018

MKURUGENZI WA NGOTI GREEN ACADEMY AWATAKA WAZAZI KUWALEA WATOTO KIMAADILI


 Mkuu wa shuleya Ngoti Green Academy  Jonson Mtewele kushoto akiwa na mkurugunzi wa Ngoti Green Academy Thomas Ngoti ambaye alikuwa anatoa neno kwa wazazi waliofika kwenye kikao cha pamoja baina ya wazazi walimu na wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo
 Mmoja wa wazazi walifika katika shule ya Ngoti Green Academy akitoa neno mbele ya wageni waalikwa na mkurugunzi wa Ngoti Green Academy Thomas Ngoti 
Picha za pamoja baina ya wazazi,walimu na viongozi wa shule ya Ngoti Green Academy  
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Ngoti Green Academy 

NA FREDY MGUNDA,IRINGA

Mkuu wa shule ya Ngoti Green Academy  amewataka wazazi na walezi mkoani Iringa kuwalea watoto katika maadili yanayostahili ili kuwa na kizazi chenye maadili na uwajibikaji kwa jamii na kuleta maendeleo ya nchi na familia zao.

Akizungumza na wazazi wa shule ya Ngoti Green Academy mkuu wa shule hiyo Jonson Mtewele alisema kuwa maadali ya mtanzania yanazidi kupotea kutoka na mmong’onyoko wa utandawazi

“Mimi nasema kuwa saizi tamaduni za kimagharibi zimeharibu sana utamaduni wenu maana wananchi wengi wanaiga bila kujua wanaiga maadili gani ndio maana saizi watoto wetu wengi wamekuwa hawana maadili” alisema Mtewele

Mtewele aliwataka wazazi kuacha kuwafundisha tamaduni za kimagharibi ambazo hazina maadili ya kimaendeleo kwa watoto wadogo ambao ndio wamekuwa waathirika wakubwa kwenye hizi tamaduni za kimagharibi.

“Mtoto kutoka mwaka mmoja hadi miaka nane ndio umri wa mtoto kupokea vitu vipya kichwani mwake ndio maana nasema ukikosea kumlea mtoto katika umri huo basi waweza kulea mtoto akiwa hana maadili yatayomuwezesha kufanikiwa katika maisha yake” alisema Mtewele

Aidha Mtewele alisema shule ya Ngoti Green Academy inawafundisha wanafunzi katika mfumo wa maadili ya dini kutoka na matendo ya bwana yesu aliyaonyesha duniani na kuwa mfano wa maadili bora.

“Tunataka mtoto akue katika maadili ya kikristo kwa maana kuwa tunamtaala wenye tabia njema siti ambazo bwana yesu alizionyesha akiwa duniani upole,unyenyekevu na wakati furani kukubali kuonewa na sio lazima abishe kila kitu na tunavyomuelekeza kwa namna hivyo tumegundua kuwa watoto watakuwa kati hali hiyo” alisema Mtewele  

Mtewele aliongeza kuwa shule hiyo inapokea watoto kuanzia mwaka mmoja hadi miaka nane kwa kuwa huo ndio wakati mzuri wa kuwalea watoto kimaadili na kuwajengea uelewa wa maisha ya baadae.

“Tumeruhusiwa kuwapokea watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi miaka nane baada ya hapo inakuwa vigumu kupokea watoto wa zaidi ya miaka hivyo kwa mjibu ya mtaala ambao tunao” alisema Mtewele

Naye mkurugunzi wa Ngoti Green Academy Thomas Ngoti alisema kuwa shule hiyo inatoa elimu iliyobora ambayo inatakiwa kitaifa na kimataifa kutokana na mtaala ambao wanautumia.

“Ngoti Green Academy inatoa elimu kwa upana wake ndio maana wazazi wengi wameanza kuwaleta watoto wao hapa kwa ajili ya watoto wao kupata elimu bora ambayo inapatika hapa nadio huo ubora wake” alisema Ngoti

Ngoti aliongeza kuwa wanampango wa kwenda kwenye ngazi ya sekondari na chuo kikuu kwa kuwa wamekuwa wakitoa elimu iliyobora hivyo hata serikali inawaamini kwa kuwa wanamtaala mzuri wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi ambao watakuwa wanasoma kwenye sekondari na chuo kikuu.

“Ngoti Green Academy Thomas ni chombo kamili cha kuandaa watoto wadogo ambao bado hawajalishwa vitu vingi kichwani na ndio maana wanataka kuanziasha sekondari na chuo kikuu ili wanafunzi weweze kupata elimu bora kwa mtaala bora ambao wanautumia” alisema Ngoti

Ngoti alisema kuwa Ngoti Green Academy inapatikana maeneo ya Mtwivila sehemu inaitwa Mwambusi au unaweza kutembelea makao mkuu ya kampuni yalipo jingo la IMUCU gorofa namba moja chumba na kumi na nane lakini unaweza kupiga namba 0765800310 au 0718056561 hapo ndio itakuwa kazi rahisi kuwapata.

UMEME NI NISHATI MBADALA ILIYO NAFUU KWA MATUMIZI YA NYUMBANI: KAMOTE

 Bw. Ally M. Koyya, (kulia), kutoka idara ya Masoko TANESCO, akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea kwenye banda la Shirika hilo kwenye maonesho ya Nishati Mbadala yanayokwenda sambamba na Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Juni 4, 2018.


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

SHIRIKA la Umeme Nchini (TANESCO) limesema hakuna sababu yoyote kwa wananchi kuogopa kutumia nishati ya umeme kwa matumizi mbalimbali ya nyumbani kwani ni nafuu mno ukilinganisha na nishati nyingine.
Afisa Mazingira wa Shirika hilo, Bw.Yusuf Kamote, amesema hayo kwenye maonesho ya Nishati mbadala ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo Juni 4, 2018, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Mkaa ni ghali tutumie Nishati mbadala”.
“Siku zote tunasema umeme wa TANESCO ni umeme wa bei nafuu, jambo la msingi ambalo wananchi wanapaswa kuelewa ni matumizi sahihi ya vifaa vya umeme kulingana na mahitaji.” Alisema.
Alisema kwa mfano mtu anatumia kifaa kinachohitaji WATI 100 (100watts) kwa saa moja lakini anatumia kifaa cha WATI 200 (200Watts) kwa saa na kwa mahitaji yanayofanana, bila shaka hayo sio matumizi bora ya umeme.
Bw. Kamote pia alishauri, wananchi wanapotaka kununua vifaa vya umeme, wanapaswa kukague kiasi cha umeme kinachohitajika kwenye kifaa husika anachotaka kununua na vifaa hivyo hupimwa kwa kutumia WATI (Watt ).
“Ukitumia pasi ya umeme ya WATI 1000 (1000Watts), kwa saa moja ni sawa na kutumia Unit 1 ya umeme kwa hivyo hakuna sababu ya kununua pasi ya umeme ya WATI2000 (2000Watts), kwa matumizi ya kawaida kwani pasi ya aina hiyo kwa matumizi sawa na ile ya WATI1000, matumizi yake yataongezeka, kutoka unit 1 hadi uniti 2.” Alifafannua.
Akieleza zaidi Bw. Kamote hakuna sababu tena ya kutumia mkaa kama nishati ya kupikia kwani hivi sasa yapo majiko ya umeme ambayo yanasaidia kudhibiti matumizi yaumeme yasiyo sahihi kwani.
“Kinachohitajika mpishi unatakiwa kuandaa vyakula unavyotaka kupika kabla ya kuwasha jiko lako la umeme, vyakula vikiwa tayari hapo ndipo unatakiwa kuwasha jiko lako tayari kwa kupika.” Alisema na kuongeza
Maonesho hayoyakliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais,  yalizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki iliyopita na yanatariwa kufungwa na Rais John Magufuli, Jumanne Juni 5, 2018.

 Wanafunzi wa shule ya sekondari Kanosa ya jijini Dar es Salaam, wakipatiwa maelezo ya kitaalamu na wataalamu wa TANESCO (Kushoto).
Afisa Mazingira wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Bw. Yusuf Kamote, (kulia), akimsikiliza Afisa Uhusiano wa Shirika hilo, Bi. Samia Chande.


 Wanafunzi wa shule ya sekondari Kanosa ya jijini Dar es Salaam, wakipatiwa maelezo ya kitaalamu kuhusu matumizi bora ya nishati ya umeme walipotembelea banda la Shirika hilo leo Juni 4, 2018.
 Bw. Ally M. Koyya, (kulia), kutoka idara ya Masoko TANESCO, akimsikiliza mwananchi huyu aliyefika kwenye banda la Shirika hilo kupata elimu ya umeme.

VIONGOZI 11 WA UPINZANI WARUSHIWA KOMBORA LA UFISADI ZITTO KABWE ATAJWA KUWA NI NAMBA MOJA

 Mwanasheria Patrobas Katambi.
Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), ambaye kwa sasa ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwanasheria Patrobas Katambi, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu viongozi wa upinzani kujinufaisha kupitia elimu na vyeo vyao. Soma taarifa hiyo hapa chini.

TUHUMA NZITO ZISIZOKANUSHIKA ZINAZOWAKABILI VIONGOZI WA UPINZANI KUJINUFAISHA KUPITIA ELIMU NA VYEO VYAO.

Ndugu, Watanzania na Ndugu Waandishi wa habari, Asasi za Kiraia na Taasisi zote wadau wa Maendeleo Tanzania, nawasalimu kwa Jina la Amani. 

Nchi yetu tumepewa na Mungu, utajiri wa Rasilimali za kila aina, ila Watu wake ni Masikini na Nchi ni Masikini Kiuchumi. 
Sababu kubwa ni makosa ya Aina ya siasa, Mifumo na Uongozi katika Uamzi, Mipango, Utekelezaji, Rushwa na Mgongano kati ya Maslahi binafsi  na Uzalendo (Ufisadi).

Ugonjwa wa Kukosa Uzalendo na Uaminifu ndio chanzo ya cha Serikali ya CCM awamu ya Tano, Chini ya Uongozi wa Mhe. Rais JP Magufuli kuamua kufanya Uchunguzi na Mabadiliko katika Sheria, mifumo, miundo, na utendaji ili kuinusuru Nchi yetu na Taasisi washirika Kiuchumi.

Bila upendeleo wa utoaji taarifa(Double Standard), Vyombo vya Habari kwa niaba na faida ya Watanzania leo wajue wapo Mafisadi wakubwa kutoka Vyama vya Upinzani, Walipata wapi Uhalali na Uhodari wa kuchambua na kutuhumu wenzao kwa ufisadi huu? Sio vibaya nao Watanzania wakawajua na kutoa hukumu bila Upendeleo, ili kuisaidia Nchi kupata Viongozi Wazalendo wa kweli.

Ikumbukwe hakuna dhambi kubwa au ndogo, dhambi ni dhambi, Ulaji ni ulaji, Haramu ni haramu, Wizi ni wizi.

Haramu ya Kiongozi wa CCM au Serikali, haiwezi kuwa Halali kwa Kiongozi wa Upinzani (Haramu ni Haramu tu.)

Katika list hii ya Mafisadi-Mibuyu 11 wa Upinzani. 

Leo naanza na mmoja (kwa machache) ambae ni Mhe.
Zitto Kabwe (MB. ACT)Kigoma mjini.

Anajipambanua na kuhubiri yeye ni Mzalendo na Mjamaa...
Ikiwa yafuatayo yanamkabili anapata wapi uhalali wa kunyooshea watu vidole?

1. Mhe. Zitto alipokea hongo kutoka Barrick kuzibwa mdomo pamoja na vifaa vya kukarabati shule jimboni kwake  vyenye thamani ya Dola $20.000 kinyume na sheria (CSR), baada ya kuwa mwiba kwao katika kudai mabadiliko ya mikataba ya madini isiyo na faida kwa Taifa.Mchakato wote  ulimnufaisha kwa zaidi ya Tshs Bilioni 1. Baada ya hongo, ghafla alikuwa mkimya kwenye Bunge na katika Kamati ya Rais JK chini ya Jaji mstaafu Mark Bomani,  hakukomaa kuizungumzia kabisaa "The Boman Report" na hata katika utungaji sheria mpya ya madini-2009 hakua mpingaji kama ilivyotarajiwa, Ukweli huo ambao hajaukanusha mpaka leo,  umethibitishwa na uchunguzi uliofanywa na Adam Hooper kwenye report yake aliyoiwasilisha chuo kikuu cha Carlton mwezi July, 2011 kwa mujibu wa gazeti la Guardian la Uingereza la Sept4, 2011.Je! hii sio kutumia cheo kutishia ili apewe hongo kwa taasisi,makampuni au Serikalini.

2. Mhe. Zitto anatuhumiwa kumiliki Ghorofa kubwa Dodoma ambalo ujenzi wake hauendani na kipato chake halali. Na awali zilipopigwa kelele akamua kusitisha ujenzi. Ghorofa hilo hajalitaja kwenye mali zake lakini ukweli uliopo ni mali yake (Kwa mujibu wa nyaraka za...)na hata mke wake mara kadhaa ameonekana akisimamia kwa kificho finishing ya jengo hilo na wapo mashahidi katika idara zote zinazohusika viwanja na ujenzi wa kuthibitisha umiliki wake.

3.  Mhe.Zitto ametajwa kwenye Jarida la The Africa Confidential liloandika kuhusu ufisadi katika Mifuko ya hifadhi ya jamii tangu awamu ya tatu,  ufisadi ambao ulihusisha vigogo wengi kwa miaka mingi. Mhe. Zitto ni miongoni mwa wanasiasa waliotajwa kwa majina, kwa namna kamati aliyoiongoza kwa miaka minane (8) ilivyofumbia macho madudu katika mifuko ya hifadhi hususani NSSF kinyume na ilivyotarajiwa.

4. Mhe. Zitto kunaushahidi kuwa, kwa miaka yote aligeuza Kamati ya PAC kama duka binafsi kwa kutisha Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi za UMMA,  baadhi ya waliokuwa wajumbe wako wanakili kupokea bahasha, ambapo wewe ulichukua kiasi kukubwa zaidi kama Mwenyekiti na kufumbia macho makosa ya wazi na ubadhirifu katika taasisi za umma kama NHC, NSSF, TANAPA,TANESCO TPA nk. mpaka baadae majipu haya yamekuja kutumbuliwa na Serikali ya awamu ya Tano. Waeleze Watanzania Uongozi wa Kamati hiyo uliupataje mara kwa mara, hata baadhi ya Wabunge wa CCM walishangazwa na ngekewa hiyo.

5. Mhe. Zitto Watanzania wanajiuiza majipu aliyoyatumbua Rais Magufuli baada ya kuingia madarakani katika Mashirika ya UMMA, kwanini Kamati yako iliyaacha na kuyafumbia macho kama hukuwa kwenye project ya kutumiwa na mafisadi?

6. Mhe. Zitto, kwanini mwanzo alionekana kuisifia sana Serikali awamu ya tano na hasa Rais Magufuli, na sasa unaipinga vikali? Je tuamini haya ni matokeo ya kukosa Uenyekiti wa PAC na badae kupoteza matumaini ya kuwa, ungeteuliwa  Uwaziri wa nishati na Madini bila kujali Chama chako kama ilivyokuwa kwa Prof. Kitila Mkumbo na Anna Mgwila? Kumbuka wapinzani wenzako walivotoka nje bungeni kupinga matokeo ya Zanzibar yeye alibaki kama mkakati wa kuishawishi CCM na Mwenyekiti wake wamuamini na upewe tena Uenyekiti wa PAC anawajua aliopanga nao huo mkakati. Baada ya hayo yote kugonga mwamba amegeuka Mbogo na nakuanza kuitafutia madoa kwa nguvu zote halali na haramu Serikali ya awamu ya tano.

7.  Mhe. Zitto, ulikaliliwa kupitia press conference akisema  na kuponda sana Muungano wa UKAWA na kusisitiza UKAWA ni "UKAWA ni Wasaka tonge"  pia siku za badae kupitia press, uliwahi kusisitiza (ushahidi upo) "Kama mtu anataka siasa za ulaghai basi aende UKAWA" akawa anaisifu Serikali ya awamu ya tano na baadae kwa kulinda maslahi yake kisiasa,  aligeuka nakuanza kuiponda Serikali ya awamu ya tano kuwa ni ya Kidikteta na inaminya demokrasia. Je! unatuambia nini Watanzania kuhusu siasa za ulaghai na usakatonge za kutumia cheo na elimu kupindisha mambo ili kulinda maslahi binafsi na si ya UMMA?

9. Mhe. Zitto, Alipofukuzwa Chadema alidai kaonewa kwa kifitna kuwa alitaka kumpindua Mhe. Mbowe katika kiti chake, na akawatuhumu CHADEMA kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha na uongozi wa Kidikteta. Je ilikuwa kweli? na kama sio kweli kwanini alisema uongo? Je Watanzania tuendelee kukuamini kwa lipi? 

10. Mhe. Zitto, Ulipotoka CHADEMA, Mhe. T Lissu alisema yale waliyokutuhumu nayo pamoja na kupewa gari mbili na Mhe. Mkono, hukukanusha bali ulielekeza tuhuma kwa  Mhe.Mbowe kama ulivyokaliliwa hapo chini, ukimjibu Mhe.Lissu Je! kwa siasa za aina hii zisizo na chembe ya uzalendo, Watanzania tuendelee kukuamini kwa yapi ya ukweli na yapi ya uongo tusiyaamini?

*Mhe.  ZITTO KABWE* Ulisema haya ukimjibu Lissu ulipofukuzwa Chadema...

"Lissu anasema nimepewa magari 2 na Mzee Mkono. Anasema kaambiwa na Mkono. Naamini Mkono alimwambia pia mwaka 2005 alimpa Freeman Aikaeli Mbowe tshs 40m ili Mbowe asifanye kampeni Musoma vijijini. Nadhani alimwambia pia mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) Mkono alimpa Freeman tshs 20m za uchaguzi wa Tarime na Freeman akasema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa. Nadhani alimwambia pia kuwa Mwaka 2010 Mkono alimpa Mbowe tshs 200m za kampeni ya Slaa. Pia hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz alimpa Mbowe tshs 100m za kampeni. Lissu anajua kuwa gazeti la Tanzania Daima limeanzishwa na fedha za chama kutoka Conservative party?

Nimefanya internship yangu kwa Mkono and Company Advocates kuhusu masuala ya mikataba. Mzee Mkono ni Mzee wangu na alisaini petition ya kumtoa Waziri Mkuu Pinda.

Lissu awaambie waliyemtuma wamwambie ukweli wote. Lissu ajue yeye ni kifaranga tu, Mimi namtaka mama wa kifaranga ajitokeze. Aeleze aliingia deal gani na Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF. Aweke wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya Umma ilipo Club Bilicanas.

They must know I am not a push over. Chacha died, I won't.

Mtu ambaye hawezi kuheshimu mke wake aliyemzalia watoto hawezi kunyooshea mtu kidole kuhusu maadili."

Mwisho wa kuku nukuu.


11. Mhe. Zitto, Je! Huoni kwamba usahaulifu wetu Watanzania, kutokusoma kwa udadisi pamoja na kutofatilia sana historia ya matukio ndio mtaji wa Wanasiasa maslahi na walaghai wanaohatarisha amani, umoja na mshikamano na maendeleo ya Taifa letu ?

12. Mhe. Zitto, Je Nini maoni yako kwa Siasa hizi  za kijasiliamali, kinafiki, chuki, fitna, uzandiki na uongo zenye ujamaa wa kibepari usio na chembe ya uzalendo kwa matendo katika maslahi na ustawi wa Taifa letu Tanzania? Je! tuendelee na siasa hizi ili tuangamie kama nchi nyingi tajiri kwa rasilimali za Kiafrika zinavyoangamizwa na Viongozi wake wenye tamaa za madaraka, mali na sifa?

13. Mhe. Zitto,  ni kwanini Mhe. Jussa aliwahi kukutuhumu na kukujibu akamaanisha wewe una ndimi mbili, Ukiwa kiongozi tunae kuamini ukweli wa kauli hiyo ni upi?

14. Mhe. Zitto, Je unaweza ukawaweka wazi watanzania Ukiwa mzalendo na mjamaa, muumini wa Azimio la Arusha na Tabora, mbali na pesa yako binafsi, ulipata wapi Milioni zaidi ya miasaba (700) za Kitanzania kuanzisha Chama ACT, na za Kampeni Uchaguzi Mkuu 2015. Ukisimamisha wagombea Ubunge na Udiwani katika majimbo 219 ukivizidi vyama kongwe vyote vya upinzani sambamba na ukwasi wa mali,hisa, na uwekezaji ulionao ndani na nje ya nchi wenye thamani ya Mabilioni kinyume na kipato chako halali,  mbali na mali ulizo orodhesha katika Tume ya Utumishi wa Umma?

15. Mhe. Zitto scandal ya Escrow na IPTL aliwahi kuchapisha kitabu/ kijarida na baadae hukukisambaza vikateketezwa. Alituhumiwa kupokea hongo kutoka kwa Sing Seth ya zaidi Tshs 50 Milioni na alikwepa kujibu tuhuma hizo.Watanzania wanakiu ya kujua ukweli juu ya tuhuma hizo?

MWISHO.

Mhe. Zitto ajue sina ugomvi wala maslahi binafsi na wewe, Kama watanzania wengine, sitilii shaka elimu yako ila natilia shaka aina ya Siasa yako, na uhalali wako wa kutuhumu wengine. Watanzania tuko tayari kukuamini endapo, utatuthibitishia tuhuma hizo za mda mrefu, sio za kweli kwa ushahidi usioacha shaka yoyote ili tuamini kuwa hautumii Elimu na cheo chako kisiasa kujinufaisha na sio kwa faida ya Taifa letu. Nipo tayari kwa lolote, hata ikibidi kwenda mahakamani.

Asanteni kwa kunisikiliza, list nitaendelea.

Na: 

Patrobas Katambi
Mwanasheria.
Mwana-CCM.
M/Kiti Mstaafu BAVICHA Taifa.
June 3, 2018.
Dar es Salaam.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More