Wednesday, November 4, 2015

Sakata la Z'bar Lakwamisha Vyama Vya Siasa Kumuaga Rais Kikwete

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeahirisha kwa mara ya pili  hafla ya vyama vya siasa kumuaga Rais Jakaya Kikwete baada ya  kumaliza miaka 10 ya uongozi wake kwa mujibu wa katiba. 
 
Hafla hiyo inayoratibiwa na Baraza la Vyama vya Siasa ilipangwa  kufanyika jana baada ya Oktoba 2, mwaka huu kuahirishwa ili kutoa  fursa kwa Rais Kikwete kushughulikia mvutano wa uchaguzi wa Zanzibar  ulioibuka kufuatia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta matokeo  yote ya uchaguzi huo. 
 
Vyama vilivyoalikwa kushiriki hafla hiyo ya kumuaga Rais Kikwete ni  Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya  Wananchi ( Ukawa) vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Cuf), NLD na vyama  vingine vya upinzani.
 
Akitangaza kuahirishwa kwa hafla hiyo  kwa mara ya pili, jijini Dar  es Salaam jana, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,  alisema kikao hicho kimeahirishwa tena kutokana na Rais kubanwa  na  majukumu mengine ya kitaifa ikiwamo suala la Zanzibar.
 
 “Tumeamua kuahirisha  hadi siku tutakayotangaza tena kutokana na  Rais kukabiliwa na majukumu mengine na suala la Zanzibar bado  linashughulikiwa,” alisema.
 
Alisema akiwa msajili wa vyama vya siasa  amefurahishwa na hatua ya  Rais Kikwete  kulishughulikia suala la Zanzibar  kwa vitendo ili   kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa  nchini.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More