Monday, April 11, 2016

Waziri Mkuu Awaweka Kitanzini Wakurugenzi wa Halmashauri Nchini

WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema Mkurugezi yeyote wa Halmashauri nchini atakayeshindwa kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya wanawake na vijana ataondolewa.

Amesema suala la kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha wanawake na vijana kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi ni la lazima na si hiari.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo jana (10 Aprili, 2016) alipokuwa anazungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Kitandi, Mtimbo,  Likunja, Nkowe na Namahema ambako alifanya mikutano ya hadhara.

“Halmashauri ambayo itashindwa kutenga asilimia 10  kwa maana asilimia tano kwa ajili ya vijana na tano kwa ajili ya akinamama Mkurugenzi wake atakuwa anatafuta safariiri,” alisema Waziri Mkuu, Majaliwa.

Waziri Mkuu, Majaliwa yupo wilayani Ruangwa, Lindi kwa ajili ya ziara ya kikazi inayolenga kukagua shughuli za maendeleo, ambapo amewasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutimiza wajibu wao na serikali haitamvumilia yeyote atakayeshindwa.

Pia Waziri Mkuu, Majaliwa aliwataka wananchi hao kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili zitakapofika sh milioni 50 za kila kijiji zilizoahidiwa na Rais, Dk. John Magufuli waweze kunufaika.

Alisema fedha hizo ambazo zitatolewa kuanzia mwezi Julai mwaka huu zitagawiwa katika vikundi mbalimbali vilivyosajiliwa na si kwa mtu mmoja mmoja hivyo amewataka watendaji wa kata na vijiji kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, Majaliwa alisema serikali imefuta tozo tano kati ya tisa za zao la korosho zilizokuwa kero ya muda mrefu na kufanya wakulima wachukie mfumo wa Stakabadhi ghalani.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More