Thursday, April 28, 2016

Madiwani wa Chadema Wilayani Hai Wasusa Kuhudhuria Kikao cha Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadiki

Madiwani  wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Helga Mchomvu, wamesusa kuhudhuria kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki wakati akizungumza na viongozi wa vitongoji, vijiji, kata, viongozi wa taasisi za serikali na dini.

Sadiki alifika wilayani Hai jana, ikiwa ni moja ya ziara zake katika wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kuzungumza na viongozi mbalimbali wanaowakilisha wananchi, pamoja na kusikiliza kero zinazozikabili wilaya hizo.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Usharika wa Hai Mjini, madiwani hao ambao wote ni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hawakuonekana hata mmoja huku eneo walilokuwa wameandaliwa likibaki na viti vilivyo wazi.

Awali, Mkuu wa Mkoa alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kwa lengo la kupokea taarifa ya wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mchomvu aliwasili kwa kuchelewa na muda ulipofika wa kuelekea ukumbini, alitokomea kusikojulikana.

Hali hiyo ilimshangaza Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa ambaye alisema siasa ziliisha baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, lakini inashangaza kwenye masuala ya maendeleo ya wananchi bado viongozi wanaendelea kuziendekeza.

Byakanwa alisema, licha ya madiwani wote 17 wanaounda Baraza la Madiwani Wilaya ya Hai kuwa ni wa Chadema, bado wanasimamia na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho chama kilichopewa ridhaa na Watanzania kuongoza kwa awamu nyingine ya tano.

“Ni jambo la kushangaza kuona viongozi waliochaguliwa na wananchi wanashindwa kuwakilisha wananchi wao katika kupeleka na kuzisemea kero zao mbalimbali zinazowakabili, na badala yake wamekuwa wakisusa vikao vya kupanga maendeleo. Kwa siasa hizi wananchi hawawezi kupata maendeleo,” alisema Byakanwa.

Akiwasilisha taarifa za kutofika kwa madiwani hao, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Hai, Rosemary Kuringe alisema, amewasiliana na madiwani wake na kuelezwa kuwa hawakupata taarifa za ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa.

Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na viongozi mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Saidi Mderu alikiri kutoa taarifa kwa madiwani wote katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani kilichofanyika Aprili 22, mwaka huu.

“Kwa suala hili la viongozi hawa kususa, namwachia Mungu, niliwapa taarifa madiwani wote tena nilisisitiza, cha kushangaza wakati Mkuu wa Mkoa amewasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri alifika akiwa amechelewa lakini wakati tumekuja kwenye ukumbi hatukumuona,” alisema Mderu.
Mkuu wa Wilaya ya Hai ,Gelasius Byakanwa akizungumza katika kikao hicho.
Mkurugenzi wa Halmshauri ya wilaya ya Hai,Said Mderu akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa katika kikao hicho.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More