Friday, April 29, 2016

Trump Achekwa Baada Ya Kushindwa Kulitamka Jina la Nchi yetu Tanzania

Mgombea wa urais kupitia chama cha Republican nchini Marekani ambaye amekuwa akiongoza kwenye kinyang’anyiro hicho, Donald Trump amejikuta akikosolewa vikali kuhusu upeo wake juu ya sera za nje pale aliposhindwa kulitamka bayana jina la Tanzania.

Drump ambaye Jumanne aliyopita alivuna ushindi wa kishindo kwenye majimbo yote manne yaliyopiga kura za mchujo alijikuta akitumbukia kwenye kadhia hiyo wakati akielezea vipaumbele vya Marekani kuelekea mataifa ya kigeni.

Alikuwa akigusia juu ya mashambulizi ya mabomu yaliyotokea katika ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali huku watu kadhaa wakipoteza maisha.

Akiwa katika hali ya kujiamini, Trump alisema kuwa iwapo ataingia madarakani moja ya vipaumbele vyake ni kuendelea kutetea masilahi ya Marekani na kudhihirisha hilo aliamua kutolea mfano mashambulizi hayo ya kigaidi.

Lakini wakati akilitaja jina la Tanzania, mfanyabiashara huyo alijikuta akigusa hisia za wengi pale alipolitaja jina hilo kinyume na inavyotamkwa. “ Ona mashambulizi yaliyotokea katika miaka ya 1990 katika ubalozi wetu nchini Tan-ZAY-nee-uh”.

Matamshi hayo yalizusha mjadala mkubwa huku baadhi ya wakosoaji wake wakiingia kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kumuelezea kama ni mtu asiyekuwa na upeo mkubwa kuhusu siasa za kimataifa.
Baadae kambi ya kampeni ya Trump ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema kuwa kuteleza kwa mgombea wao katika matamshi ya jina halisi la Tanzania hakumaanishi kuwa uwezo wake kuhusu masuala ya usalama,diplomasia ya kimataifa na biashara ya kimataifa ni wa kutiliwa mashaka.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More