Thursday, April 28, 2016

Wafanyakazi 8,000 Hawajawasilishiwa Michango ya NSSF

Wafanyakazi takriban 8,000 ambao ni wanachama wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) hawajawasilishiwa michango kutoka kwa waajiri wao yenye thamani ya Sh bilioni 21.4.

Kutokana na hali hiyo, NSSF imetoa muda wa miezi miwili kwa waajiri wote nchini ambao hawajawasilisha fedha za michango hiyo kwa shirika hilo, kuwasilisha mara michango hiyo kabla ya Julai mosi, mwaka huu.

Kwa mujibu wa shirika hilo, endapo muajiri yeyote atashindwa kutekeleza agizo hilo katika muda huo uliotolewa, NSSF haitakuwa na njia nyingine zaidi ya kuwaburuza waajiri hao mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Aidha shirika hilo, lilibainisha wazi kati ya waajiri sugu wasiowasilisha kwa wakati michango ya wafanyakazi wao kwa shirika hilo, ni Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (Tazara) na baadhi ya kampuni za ulinzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa NSSF, James Aigo alisema ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya NSSF kwa mwajiri kutowasilisha michango ya mfanyakazi wake.

Aigo alisema kwa mujibu wa sheria hiyo waajiri wote wanatakiwa wawasilishe michango ya wafanyakazi wao ndani ya siku 30 kutoka tarehe ya mwisho wa mwezi husika.

 “Lakini kuna baadhi ya waajiri kwa sababu wanazozijua wenyewe, wanashindwa kutekeleza hitaji hili la kisheria kikamilifu kwa kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati,” alisisitiza Aigo.

Alisema kwa mwaka huu wa fedha unaoisha Julai mosi, mwaka huu, takribani wafanyakazi 8,000 ambao ni wanachama wa shirika hilo hawajawasilishiwa michango kutoka kwa waajiriwa wao.

Alisema kati ya hao wafanyakazi 3,234 wanatokea Dar es Salaam, ambao ni sawa na asilimia 60 ya wafanyakazi wote ambao hawajawasilishiwa michango na waajiri wao yenye thamani ya Sh bilioni 21.4.

Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji na Miradi, Mseli Abdallah aliwataka wateja waliopangisha na kununua nyumba kwa mkopo kupitia nyumba za NSSF, kukamilisha malipo yao kabla ya kutolewa kwenye nyumba hizo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia taarifa hiyo wakati Bw James Oigo Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Shirika la Taifa la  Hifadhi ya Jamii NSSF akizungumza nao katika mkutano huo.
Baadhi ya maofisa wa shirika hilo wakiwa katika mkutano huo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More