Sunday, April 24, 2016

Serikali Yapangua Hoja Moja ya UKAWA

SIKU moja baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kususa kuchangia hotuba za bajeti, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri, amesema serikali haikukosea kuipa Wizara ya Ujenzi fedha zaidi ya zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge.

Hoja hiyo ni moja kati ya tatu ambazo juzi ziliibuliwa bungeni na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Badala ya kuwasilisha Mpango Mbadala wa Maendeleo wa Taifa na maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mpango wa serikali pamoja na maoni ya kambi hiyo kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu, juzi Mbowe alisema wabunge wa upinzani watakuwa wanaingia kwenye Ukumbi wa Bunge lakini hawatachangia hotuba ya bajeti mpaka pale hoja zao zitakapojibiwa.

Mbowe alidai kuwa uamuzi wao huo umetokana na Serikali kufanya kazi bila kuwa na mwongozo wa utendaji kazi kwa wizara mbalimbali, kuvunjwa kwa Katiba na sheria za nchi na kupokwa uhuru na madaraka ya muhimili wa Bunge.

Mwenyekiti huyo wa Chadema na Mbunge wa Hai, alikwenda mbali zaidi akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imekiuka sheria kwa kuipatia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Sh. bilioni 607.4 ikiwa ni fedha za ndani kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2015/16 wakati Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 191.6.

Wakati Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, aliyeongoza kikao cha juzi akieleza kuwa madai ya upinzani ni mazito na kushauri waende mahakamani, Serikali imejibu moja ya hoja tatu za Mbowe.

Akiongea na waandishi wa habari  katika  jengo la Wizara ya Fedha na Mipango  jana asubuhi, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Mwanri, alisema Serikali ya Awamu ya Tano haijafanya makosa kuipa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kiasi hicho cha fedha.

Ofisa huyo wa serikali alisema Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 inaruhusu Ofisa Masuhuli na Waziri kufanya uhamisho wa fedha za mradi mmoja kwenda kutekeleza mradi mwingine.

"Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 inaruhusu Ofisa Masuhuli kufanya 'reallocation' (uhamisho) ya matumizi ya fedha lakini isizidi asilimia saba ya 'Vote' (Fungu) husika," alisema na kuongeza:

"Sheria hiyo pia inamruhusu Waziri kufanya 'reallocation' ya matumizi ya bajeti husika lakini haipaswi kuzidi asilimia 10. Pesa ilizopewa Wizara ya Ujenzi zimezingatia sheria na fungu walilopewa limo ndani ya sheria."

Florence alisema wizara hiyo ina madeni makubwa ya wakandarasi, hivyo kutoyalipa ni kuendelea kukuza mzigo kwa serikali kwa kuwa riba inaongezeka.

"Serikali iliamua kutoa kiasi hicho cha fedha (Sh. bilioni 607.4) ili kuyapunguza madeni ya Wizara ya Ujenzi. Tukumbuke kuwa wizara hii, ndiyo yenye madeni makubwa," alifafanua zaidi ofisa huyo wa serikali.

Katika maelezo yake ya msingi aliyoyawasilisha bungeni juzi, Mbowe alisema kuwa kwa kuipa wizara hiyo kiasi hicho cha fedha badala ya Sh. bilioni 191.6 zilizoidhinshwa na Bunge, Serikali ya Awamu ya Tano imevunja kifungu cha 41(1) cha Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Katiba hiyo, kifungu hicho kinasema: “Serikali itawasilisha bungeni kwa idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango kilichoidhinishwa na Bunge au kwa madhumuni ya kugharamia mahitaji ambayo hayakupangwa”.

Mbowe alisema utaratibu huo pia unatiliwa nguvu na Sheria ya Fedha za Umma wa mwaka 2001 (Public Finacne Act, 2001) ambayo kifungu cha 18 (3) na (4) inaitaka serikali kupeleka bungeni bajeti ya nyongeza (mini-budget) kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More