Monday, April 11, 2016

Mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi na Jeshi la polisi Kuwekwa hadharani leo

Mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises uliosababisha kashfa ya ufisadi wa mabilioni ya fedha katika Jeshi la Polisi, leo unatarajiwa kuwasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
 
Mkataba huo huenda ukawasilishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ili kutoa fursa kwa wajumbe wa kamati hiyo kuupitia kipengele kwa kipengele kabla ya viongozi wa jeshi hilo kuanza kuhojiwa juu ya ufisadi huo.
 
Kupitia mkataba huo wa 2011, Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa tenda ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.
 
Tayari kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine katika vituo 14 tu katika jiji la Dar es Salaam ambavyo pia havijulikani vipo maeneo gani.
 
Uwasilishwaji wa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo la PAC, ambapo Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly alitoa siku sita kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba huo.
 
Jana Aeshi alisema baada ya kamati yake kupokea mkataba huo wajumbe wataupitia na kuujadili kwa kina ili kuona kama kuna upungufu.
 
“Kesho (leo) ndiyo tarehe 11, tutapokea  mkataba kama tulivyowaomba watuletee, wakituletea tutausoma na kuujadili kwa kina kisha tutawaapa maelekezo,” alisema Aeshi.
 
Alisema iwapo kamati yake haitaridhishwa na maelezo ya viongozi wa Jeshi la Polisi kuhusu mkataba na fedha zilizotumika, upo uwezekano mkubwa wa kuundwa kwa kamati maalumu.
 
“Kama vifaa vimefungwa katika vituo vyote, ni matumaini yetu vitakuwa vinafanya kazi, huwezi kufunga vifaa ambavyo ni vibovu…kama maelezo tutakayoyapokea hayataridhisha kuna uwezekano wa kuundwa kwa kamati ya uchunguzi,” alisema Aeshi.
 
Hivi karibuni Kamati ya PAC ilibaini kuwapo kwa viashiria vya ufisadi katika Jeshi la Polisi kwa kuwaeleza waandishi wa habari kuwa Kampuni ya Lugumi ililipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37 za mkataba wote.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More