Wednesday, April 20, 2016

Wachina Kizimbani kwa Kukwepa Kodi

Wafanyabiashara wawili raia wa China wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la kuuza bidhaa bila kutoa stakabadhi za kodi za kieletroniki (EFD).

Washtakiwa hao ni Paishu Chea na Apple Chen ambao wote walisomewa mashtaka yao kwa mahakimu wawili tofauti na kulikiri kutenda makosa, hivyo kulipa faini ya Sh2 milioni kila mmoja ili kuepuka kifungo cha miaka mitatu.

Katika kesi ya kwanza, Mwendesha Mashtaka wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Noah Tito alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Saidi Mkasiwa kuwa kati ya Machi 14 na 16 katika Mtaa wa Narung’ombe na Kongo, Chea aliuza bidhaa za thamani ya Sh28,000 bila kutoa risiti ya EFD kinyume na sheria.

Katika kesi ya pili, Wakili wa TRA, Consolatha Andrew alidai Cheng alitenda kosa la kutotoa risiti kati ya Machi 14 na 15 katika Mtaa wa Narung’ombe na Kongo.

Andrew alidai Cheng ambaye ni mfanyakazi katika Kampuni ya Dong Shen International aliuza viatu vyenye thamani ya Sh1.4 milioni, lakini hakutoa risiti kwa mnunuzi kama sheria inavyomtaka. 

Hakimu wa mahakama hiyo, Flora Haule alimuamuru mshtakiwa huyo kulipa faini ya Sh2 milioni au kwenda jela miaka mitatu. Hata hivyo mshtakiwa alilipa faini.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More