Monday, April 18, 2016

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) Yalalaimika Kukandamizwa na Serikali

Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) umeitaka Serikali kutafakari upya Sheria ya Asasi za Kiraia ili kuyaondolea mzigo wa uendeshaji Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) badala ya kuyafungia kutokana na sababu mbalimbali. 

Hivi karibuni Serikali kupitia kwa Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ilifuta usajili wa NGO’s 110 kwa kuendesha shughuli zao kinyume cha Sheria ya NGOs Na 24 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005. 

Kwa mujibu wa msajili huyo, mashirika hayo ni yale ambayo hayajawasilisha taarifa za mwaka kwa kipindi cha miaka miwili bila kutoa sababu za msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Hebron Mwakagenda alisema kuna haja kwa Serikali kuangalia mashirika hayo kabla ya kukimbilia kuyafungia. 

Aliiomba Serikali ifute ada ya mwaka na ilipwe wakati wa kusajili tu na aliikosoa pia sheria hiyo akisema inayalazimisha mashirika hayo kupeleka taarifa zao Dar es Salaam kutoka kila kona ya nchi badala ya kupeleka kwenye ngazi za wilaya.

“Maofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri za wilaya ambao pia ni wasajili wasaidizi na waratibu wa shughuli hizi wapewe mamlaka ya kupokea taarifa za utendaji kila mwaka kwa niaba ya msajili ili kuepusha usumbufu wa kusafiri hadi Dar es Salaam.” Alisema Hebron Mwakagenda

Edmund Simon wa asasi ya Umoja wa Wawezeshaji kutoka Kigoma iliyo chini ya mtandao huo, alisema Serikali inapaswa kuzisaidia NGOs na asasi badala ya kuzikandamiza.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More