Thursday, April 28, 2016

Watakaolipa mishahara HEWA kuburuzwa Mahakamani

Serikali imesema vigogo wa juu katika utumishi wa umma, watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha ulipaji wa mishahara hewa, watafunguliwa kesi ya jinai.

Aidha, imesema ifikapo Julai mosi, mwaka huu Halmashauri zote nchini ziwe zimefunga na kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato yake ya ndani na zimetakiwa kusitisha ukusanyaji kwa njia ya mawakala.

Katika hatua nyingine imesema hadi kufikia Machi, 2016, watumishi 90 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na wengine kufikishwa mahakamani kwa kukiuka taratibu na sheria za kazi wakiwemo wakurugenzi watendaji (DED) wa halmashauri watano ambao wamevuliwa madaraka.

Hayo yalisemwa kwa wakati tofauti na mawaziri wawili katika Ofisi ya Rais, walipowasilisha hotuba za bajeti kwa ofisi zao kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini Dodoma jana. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki akiwasilisha hotuba ya ofisi hiyo, alisema kuanzia sasa kiongozi wa serikali wakiwemo wa ngazi za juu watakaobainika kuhusika kwa njia moja au nyingine katika kufanikisha ulipaji wa mishahara hewa watafunguliwa kesi za jinai.

Waziri huyo alisema uchumi imara na endelevu katika nchi yoyote unahitaji uwepo wa utumishi wa umma uliotukuka unaozingatia utawala bora, utawala wa sheria, maadili na mifumo thabiti ya usimamizi na utekelezaji.

Alisema mipango na bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa ofisi hiyo imezingatia dhamana hiyo ambayo imebeba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuleta mabadiliko makubwa katika utumishi wa umma kwa kuimarisha uwajibikaji na uadilifu.

Alisema utekelezaji wa dhamira hiyo utasaidia kujenga utumishi wa umma uliotukuka kwa kuondokana na matumizi mabaya ya madaraka, kuondokana na ukiukwaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa umma, kuondokana na ucheleweshaji wa maamuzi, kutosimamiwa kwa uwazi na kutowajibika kwa viongozi na watumishi.

“Ni lazima tuwe na viongozi wa umma wanaozingatia maadili yao ya kazi na ndio maana tunasisitiza kuwa viongozi wote watakaobainika kuhusika na ulipaji au kusaidia kulipa watumishi hewa mishahara, tutawafungulia kesi za jinai,” alisema Kairuki.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene akiwasilisha hotuba ya bajeti yake, alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, watumishi 78 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa walichukuliwa hatua za kinidhamu na kijinai.

Alisema kati ya watumishi hao, ma-DED watano wamevuliwa madaraka na kupangiwa kazi nyingine na wakurugenzi watatu wamefunguliwa kesi mahakamani na kesi hizo bado zinaendelea.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More