Thursday, April 28, 2016

Msajili wa Vyama Avikaba Koo Vyama 21 Vya Siasa Ambavyo Havijakaguliwa.

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ametoa miezi mitatu kwa vyama 21 ambavyo havijakaguliwa kuwasilisha hesabu zake.

Kauli ya Jaji Mutungi imekuja siku nne baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu katika vyama vya siasa 22 vyenye usajili wa kudumu, CAG alieleza kati ya vyama hivyo, chama cha CUF pekee ndicho kilikuwa kimepeleka hesabu zake kwa kipindi cha miezi sita, kati ya Januari hadi Juni 2015.

Alisema vyama vingine 21 havikuwasilisha vitabu vya hesabu kwa ajili ya ukaguzi kinyume na kifungu cha 14 cha Sheria ya vya ma vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.

Akizungumza jana nje ya viwanja vya Bunge, Jaji Mutungi alisema ukaguzi wa fedha katika vyama ni suala la kisheria na lina mchakato wake, akisisitiza kuwa ofisi yake imeisoma taarifa ya CAG na inaifanyia kazi kwa kuvipa vyama hivyo miezi mitatu.

“Kwa mujibu wa sheria tunatakiwa kuvikumbusha vyama kufanya ukaguzi na tulifanya hivyo mwanzoni mwa mwezi huu (Aprili).

"Tuliviandikia barua vyama vyote. Ila kutokana na kuibuliwa kwa suala hili tumeviandikia barua na kuvipa miezi mitatu kukamilisha hesabu zao,” alisema.

Alisema ofisi yake haiwezi kuweka shinikizo kuhusu suala hilo kwa maelezo kuwa jambo hilo  linafanyika kwa matakwa ya kisheria.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More