Tuesday, April 5, 2016

TAKUKURU Yajitosa Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji

Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza rasmi kuingilia kati na kutafutia ufumbuzi tatizo la rushwa katika migogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini.

Taasisi hiyo imewaonya viongozi wa vijiji wenye tamaa na kuchangia kuibuka kwa migogoro hiyo na kuwataka wakae chonjo kwani wakati wa kuishughulikia migogoro hiyo umefika.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa taasisi hiyo mkoani Morogoro, Emmanuel Kiyabo alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya kazi za Takukuru mkoani humo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

Aliwataka viongozi wa vijiji kuachana na tamaa ya kupokea fedha kutoka kwa wafugaji na kuingiza mifugo hovyo, hali inayosababisha uhaba wa ardhi na migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Mkoa wa Morogoro ni moja wa mikoa yenye migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji hasa wilaya za Kilosa na Mvomero ambayo wakati mwingine imesababisha vifo vya watu na maelfu ya mifugo.

Mkuu wa Takukuru aliwataka pia wakulima kuacha tamaa ya kupokea malipo ya fidia ya mazao yao kutoka kwa wafugaji isivyo halali. 

Alisisitiza wafugaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kusafirisha mifugo na kuingiza katika maeneo mapya bila kuathiri maisha ya wenyeji wao.

Alisema katika kipindi hicho cha miezi mitatu, taasisi hiyo ilifanya udhibiti na kushauri idara mbalimbali za Serikali namna ya kuziba mianya ya rushwa ikiwamo kuweka mikakati inayopimika ya kudhibiti mianya hiyo iliyobainika.

Aidha, alisema katika kipindi hicho pia jumla ya miradi ya maendeleo 16 yenye thamani ya Sh bilioni 3.4 ilikaguliwa na baadhi ya miradi hiyo iligundulika kuwa na vitendo vya udanganyifu katika matumizi ya fedha za Serikali na kusisitiza kuwa uchunguzi unaendelea.

Hata hivyo, alisema katika uchunguzi wanaoendelea nao wameweza kuokoa fedha za Serikali Sh milioni 14.4 zilizokuwa mikononi mwa baadhi ya watuhumiwa. Alisema fedha hizo zimeingizwa kwenye akaunti maalumu ya Serikali ya fedha zilizookolewa.

Alisema Takukuru iliokoa Sh milioni 13.2 ikiwa ni gharama ya kuweka alama za barabarani katika Manispaa ya Morogoro, akieleza kuwa mkandarasi alilipwa bila kuweka alama hizo katika barabara za Kitope, Kingo, Mlapakolo na Nguzo.

Lakini mara baada ya taasisi hiyo kuanza uchunguzi na wahusika kufahamu kuwa wanachunguzwa, waliweka alama hizo kwa mujibu wa mkataba.

Pia alisema katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Machi mwaka huu, Takukuru ilifungua kesi 12 katika Mahakama za Wilaya za Ulanga, Morogoro, Kilosa na Mahakama ya Mkoa ambazo watuhumiwa wake walihusika kuomba na kupokea rushwa.

Mkuu huyo wa Takukuru alisema katika kipindi hicho, pia taasisi hiyo mkoani Morogoro ilipokea jumla ya taarifa 105 zinazohusisha malalamiko dhidi ya idara na taasisi mbalimbali za Serikali ambazo ni serikali za vijiji, mitaa, vitongoji, afya, utumishi, sekta binafsi, mabaraza ya usuluhishi, ardhi, maliasili, kilimo, maji, jeshi la wananchi wa Tanzania, manunuzi, mamlaka ya vitambulisho vya Taifa, Bodi ya Tumbaku, ujenzi na fedha.

Naye Mkuu wa Takukuru mkoani Shinyanga, Gasto Mkono alisema katika kipindi cha miezi mitatu wamepokea taarifa 39 kutoka kada mbalimbali ikiwemo kufuatilia miradi ya maendeleo iliyojengwa chini ya kiwango.

Alisema tayari kesi 13 zipo mahakamani zikiwemo kesi zingine mpya nne zilizofunguliwa kipindi hicho zinazohusika na masuala ya utoaji hongo huku miradi saba ikiwa katika uchunguzi na miwili imebainika kuwa na kasoro.

Mkono aliyekuwa anazungumza na waandishi wa habari alisema kutokana na kukithiri kwa rushwa ndogondogo katika kada mbalimbali kumesababisha wananchi kuichukia Serikali.

“Machi 21, mwaka huu, Alex Filipo ambaye ni askari wilayani Kishapu alituhumiwa kuomba kiasi cha Sh milioni moja kutoka kwa mganga wa kienyeji, Jidala Ngusa aliyemkamata kwa kufanya uganga bila kibali askari alikamatwa akipokea kiasi cha Sh 50,000 ikiwa sehemu ya mwendelezo wa malipo ya fedha hizo,” alisema Mkono.

Alisema Takukuru inaendelea kutoa elimu katika jamii na idara zinazolalamikiwa kwa vitendo vya rushwa mkoani hapa ni serikali za mitaa, ardhi, afya, sekta binafsi, polisi, magereza, mahakama, elimu na kwenye vyama vya siasa hasa nyakati za uchaguzi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More