Tuesday, April 26, 2016

Polisi Dar Yakamata Ombaomba 45 Dar, 17 Wapelekwa gerezani

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wamewakamata na kuwaondoa ombaomba 45 na 17 wamewapeleka gerezani. 
 
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na Idara ya Ustawi wa Jamii, wanafanya utaratibu wa kuhakikisha watu hao wanarudishwa mikoani walikotoka. 
 
“Kazi hii inaenda vizuri na ombaomba wachache wamebakia ambao wakiwaona askari wanakimbia na kutokomea kusikojulikana,”alisema Sirro. 

Katika tukio lingine, Polisi wanawashikilia watuhumiwa 96 wenye umri wa miaka 15-18 wanaodaiwa kujihusisha na matukio ya kuvamia nyumba na kuiba usiku. 
 
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao wanajulikana kwa jina maarufu la ‘kumi ndani kumi nje’, walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya jiji na wanaendelea kuhojiwa na polisi, upelelezi utakapo kamilika watafikishwa mahakamani. 
 
“Watuhumiwa hawa wanavunja milango kwa mawe makubwa na kuiba televisheni na simu, upelelezi unaendelea na wanaendelea kutajana hivyo tutawakamata na wengine,” alidai kamanda huyo. 
 
Wakati huohuo, Kamanda Sirro alisema makosa ya kuvunja Sheria ya Usalama Barabarani mkoani hapa, yameliingizia jeshi hilo mapato ya Sh463 milioni kwa muda wa siku 10. 
 
“Jeshi la Polisi kazi yetu ni kusimamia sheria siyo kukusanya mapato, hivyo watu wazingatie sheria,” alisema kamanda huyo. 
 
Alisema ili kupunguza matukio ya uhalifu, jamii haina budi kuhakikisha kunakuwa na vikundi vya ulinzi shirikishi katika mitaa yao na Serikali za Mitaa zinapaswa kuhakikisha jambo hilo linazingatiwa na linafanyika.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More