Monday, April 11, 2016

Wabunge Wahoji Uhalali wa Kisheria wa Rais Magufuli kuhamisha fedha za Muungano na Kuzipeleka Kwenye Ujenzi wa Barabara Mwanza

Baadhi ya Wabunge wamehoji uhalali wa kisheria wa Rais John Magufuli kuhamisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe ya Muungano na kuzipeleka kwenye ujenzi wa barabara katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Wabunge hao walihoji hilo wakati wa semina iliyofanyika jana katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam , iliyoendeshwa na Dk Haji Semboja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Harold Sungusia wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali alihoji juu ya mamlaka ya Rais katika kutumia fedha ambazo zilishapangiwa bajeti na Bunge na kuzipeleka kwenye maeneo mengine.

Alihoji pia juu ya nidhamu ya Serikali katika usimamizi wa Bajeti iliyopitishwa na Bunge. Mbunge huyo alisema dhana ya mgawanyo wa madaraka haipo kwa sababu Serikali ina nguvu kuliko Bunge na Mahakama hivi sasa.

Alisisitiza kuwa nguvu hiyo ndiyo inayomfanya Rais afanye kitu chochote anachotaka.

Mbunge wa Viti Maalumu, Lucia Mlowe alisema moja ya majukumu ya Bunge ni kuisimamia Serikali, lakini anashangaa kuona yenyewe ikilisimamia Bunge katika mambo mbalimbali.

Alisema hata suala la Rais kuhamisha fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe ya Muungano, ni kuingilia madaraka ya Bunge, kwa sababu fedha hizo tayari zilikuwa zimeidhinishwa kwa ajili ya matumizi hayo.

“Naomba kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu hapa, Rais ana mamlaka gani ya kuhamisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya jambo fulani? Pia, ni namna gani wabunge tunaweza kuisimamia Serikali kama hamna uwiano kati ya mihimili hii mitatu,” alihoji mbunge huyo.

Akijibu hoja hizo, Dk Semboja alisema Sheria ya Bajeti ya 2015, inampa mamlaka Rais kupeleka fedha katika eneo analoona inafaa.

Alisema sheria hiyo inatoa sharti moja, kwamba Rais kupitia Waziri wa Fedha, atatoa taarifa bungeni juu ya matumizi ya fedha hizo.

Dk Semboja alisema mamlaka hayo yanatambuliwa pia katika Ibara ya 137 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, hivyo Rais hajakosea kuhamisha fedha hizo kwenda kujenga barabara isipokuwa taarifa ya matumizi itolewe bungeni hata kama matumizi yanaonekana.

“Bunge lazima lifahamishwe kuhusu matumizi ya fedha hizo.Kama ni udhaifu wa kipengele hiki, basi unaanzia kwenye Katiba,” alisema Dk Semboja.

Pia, Sungusia alisema, “Fedha ambazo Rais hawezi kuziingilia ni zile zilizo kwenye consolidated fund (mfuko hodhi), nje ya hapo anaweza kufanya lolote,” alisema mwanasheria huyo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More