Wednesday, April 13, 2016

Tanzania yaongoza Afrika kwa kulima ufuta Kidunia Inashika Nafasi ya 3

TANZANIA imetajwa kuwa inaongoza kwa kulima na kuzalisha ufuta Afrika huku ikishika nafasi ya tatu ya duniani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Maendeleo, Naliendele, Dk Omary Mponda, alisema kuwa Tanzania imefikia hapo baada ya jitihada kubwa zilizofanywa na serikali.

Jitihada hizo zinafanyika kupitia watafiti wake wa masuala ya kilimo kwa kutafiti na kugundua mbegu bora zinazostahimili ukame, magonjwa na wadudu.

Mtaalamu huyo ambaye pia ni mtafiti kiongozi na mratibu wa mbegu za mafuta, alisema kwa sasa Tanzania inazalisha wastani wa tani 460,000 kutoka tani 38,000 zilizokuwa zikizalishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Alisema kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), Tanzania imepanda kutoka nafasi ya saba kidunia mwaka 1998 hadi kufikia nafasi ya tatu ikitanguliwa na India na Mayama.

“Hiki kituo cha utafiti kilianza mwaka 1945 wakati huo kilikuwa kinashughulikia korosho peke yake, lakini kufikia mwaka 1978 tulianza kuingiza utafiti wa mbegu za karanga na ufuta ambapo mpaka sasa tumeshagundua mbegu aina 12 ambazo wakulima wetu wanazitumia”, alisema.

Mtaalamu huyo aliyebobea katika masuala ya utafiti wa mbegu za mafuta, alisema kuwa zao hilo miaka ya nyuma lilikuwa linalimwa katika mikoa ya Kusini ambayo ni Mtwara, Lindi na Ruvuma. Alisema kutokana na hamasa kubwa inayofanywa na wataalamu wa kilimo, tayari mikoa kadhaa inalima zao hilo.

“Huko nyuma hata eneo lililokuwa likilimwa ufuta lilikuwa dogo sana, lakini sasa ni zaidi ya hekta 650,000 zinalimwa ufuta nchi nzima…sasa haya ni mafanikio makubwa na yanayopaswa kujivunia na hiyo inatokana na ugunduzi huu wa mbegu bora”, alisema.

Ufuta ni moja kati ya mazao yanayoongeza kipato kwa makusanyo ya ndani kwa baadhi ya halmashauri za wilaya ikiwemo wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo Ruangwa, msimu uliopita ilipata Sh milioni 400 kutokana na ushuru wa mauzo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More