Wednesday, April 13, 2016

Wabunge Wadai TANAPA Ni JIPU


SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limeingia kwenye orodha ya Taasisi za Serikali zenye matumizi makubwa ya fedha ukilinganisha na mapato wanayokusanya, jambo lililoishtua Kamati ya Bunge na kutaka shirika hilo lipunguze matumizi yake.

Hayo yalibainika jana Dar es Salaam wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), ilipokutana na Tanapa kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14.

Katika ripoti hiyo ilibainika kwamba Tanapa kwa mwaka huo wa fedha, ilitumia jumla ya zaidi ya Sh bilioni 151.7 ilhali mapato yao yalikuwa Sh bilioni 149.9 hivyo matumizi ya fedha yaliyozidi ni Sh bilioni 1.8.

Taasisi nyingine ya Serikali ambayo ilikuwa na matumizi makubwa ya fedha za Serikali ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ripoti ya CAG ya mwaka 2013/14 ilionesha kuwa ilitumia Sh bilioni 18.6 kwa ajili ya matumizi ya watumishi wake.

Wakichangia hoja mbalimbali wakati wa kupitia ripoti hiyo hapo jana, Wajumbe wa Kamati hiyo walisema kutokuwepo Bodi ya Shirika hilo, kunachangia watendaji wa shirika hilo kuliendesha ndivyo sivyo.

Mjumbe wa Kamati hiyo, Albert Obama, mbunge wa Muhigwe alisema shirika hilo ni jipu kwa sababu limejilimbikizia ulaji, kana kwamba ni chombo cha watu wachache, ilhali shirika hilo linatakiwa liwe kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa nchi.

“Haiwezekani ripoti ya mwaka 2013/14 inaonesha kuwa mapato yenu yalikuwa Sh bilioni 149.9 halafu matumizi yenu ni Sh bilioni 151.8”, yaani mnatumia chote hadi mnadaiwa sasa hii sio sawa, hili ni shirika la umma?” Alihoji Obama.

“Hapa wanakuja na maneno matamu kwamba bajeti ya mwaka huu 2016/17 wamepanga kukusanya mapato ya Sh bilioni 188 lakini matumizi yenu pia mmeainisha yatakuwa Sh bilioni 270, hii ikoje? " Alihoji Obama.

Mjumbe mwingine, Joseph Kakunda mbunge wa Sikonge, alisema Tanapa haina changamoto kubwa, zinazoifanya ishindwe kukusanya mapato makubwa zaidi ya hayo ya sasa na kusema walipaswa kukusanya zaidi ya Sh trilioni moja na sio hizo bilioni 149.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More