Thursday, April 7, 2016

idara ya afya katika mkoa wa Iringa ndiyo Sekta inayoongoza kwa malalamiko ya kuomba na kuchukua rushwa

IMEELEZWA   kwamba idara ya afya katika mkoa wa Iringa  ndiyo Sekta inayoongoza kwa malalamiko ya kuomba na kuchukua rushwa.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru)  Mkoa wa Iringa, Eunice Mmari  wakati akizungumza na wanahabari mjini hapa na kusema kuwa taasisi hiyo imepokea  malalamiko 28 ya rushwa na 14 kati ya hayo yamefunguliwa majalada ya uchunguzi na malalamiko tisa bado yanafanyiwa uchunguzi wa awali.


 Kauli ya Mmari ameitoa wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi  wa takukuru kwa kipindi cha robo mwaka cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.

 Alisema kuwa malalamiko matano yaliyoshindwa kuthibitisha makosa ya rushwa yamefungwa na imewafikisha mahakamani watuhumiwa wanne wa makosa mbalimbli ya rushwa katika kesi tatu zilizofikishwa mahakamani.

Alisema kuwa idara ya afya inaongoza kwa kuwa na malalamiko saba yanahusiana na rushwa ikifuatiwa na serikali za mitaa katika kata na vijiji ambapo malalamiko yaliyojitokeza ni sita.

Amezitaja idara nyingine ambazo zina malalamiko mengi  kuwa ni serikali za mitaa kitengo cha elimu ambapo walipata malalamiko matatu, kilimo na ushirika yalijitokeza malalamiko mawili sambamba  na baraza la ardhi na sekta binafsi waliyapata malalamiko mawili.

Alisema kuwa idara ya polisi,mahakama na wakala wa serikali upande wa Tanroads wamepokea lalamiko moja kwa kila idara  kwa kipindi cha robo mwaka cha January hadi Machi mwaka huu.

Hata hivyo ameongeza kuwa taasisi hiyo imeweka mkakati wa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kutoa elimu ya rushwa na kuwataka wananchi wasisite kutoa taarifa ya rushwa kwa taasisi hiyo ili iweze kufanyiwa kazi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More