Thursday, April 28, 2016

Korea Kuleta Walimu wa Sayansi na Hisabati ili Kupunguza Uhaba wa Walimu Nchini

SerikaliI ya Korea imepanga kuleta nchini walimu wa masomo ya hisabati na sayansi kwa shule za sekondari, kusaidia kupunguza uhaba wa walimu wa masomo hayo.
Itatekeleza azma hiyo kupitia Mpango wake wa Kusambaza Walimu wa Kikorea katika nchi Zinazoendelea (KTDP).

Akizungumza jana alipotembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais wa Taasisi ya Elimu ya Kimataifa (NIIED), Kim Kwangho, alisema nchi yake imekuwa ikisambaza walimu.
Alisema mpaka sasa wamesambaza walimu 61 katika nchi mbalimbali zinazoendelea; na mwaka huu watasambaza walimu 140 kwa nchi 15.

“Tumeona katika kuunga mkono juhudi za serikali kuongeza walimu wa masomo ya sayansi na kwa mara ya kwanza mwaka huu taasisi yetu itasambaza walimu 10 hapa Tanzania kati yao watano watahusika katika masomo ya hisabati na wengine watano watahusika na masomo ya Sayansi,” alisema Kwang-ho.

Aidha alisema licha ya kusambaza walimu hao, Serikali ya Korea inatoa ufadhili kwa wanafunzi wenye vipaji kimataifa ili kuendeleza masomo yao katika taasisi za elimu ya juu nchini kwao, lengo likiwa ni kusaidia kukuza viongozi wa baadae wenye elimu.

Kwang-ho alisema waombaji wa ufadhili huo ni wale waliosoma tu Shahada ya kwanza na shahada ya Uzamili nchini; na haitawahusu wale wote ambao wamewahi kusoma Korea.

Katika hatua nyingine, Kwang-ho alisema Korea ina mpango wa kufungua kituo cha kutoa kozi ya lugha ya Kikorea katika chuo kikuu hapa nchini, lengo likiwa ni kupanua wigo wa fursa kwa wanafunzi wa Kitanzania kujifunza lugha hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Masuala ya Mahusiano Kimataifa, Opportuna Kweka alisema tayari rais huyo ameshakutana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala na kujadili uwezekano wa kuanzisha kituo hicho.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More