Wednesday, November 4, 2015

Chadema Kupinga Ushindi wa Hussein Bashe Mahakamani

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Nzega mkoani Tabora kimetangaza kwenda mahakamani kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Mbunge wa jimbo la Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM).
 
Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Hawa Mniga alimtangaza Hussein Bashe kuwa mshindi baada ya kupata kura 18,774 akifuatiwa na mgombea wa Chadema, Charles Mabula aliyepata kura 9,658.
 
Akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa kuwashukuru wananchi kwa kukipigia kura chama hicho, Mwenyekiti wa jimbo hilo Mabula alisema uchaguzi huo haukuwa huru na haki kutokana na kasoro nyingi kujitokeza na baadhi ya vituo kuwa na zaidi ya karatasi tatu za matokeo.
 
Alisema rushwa ilitawala siku ya kupiga kura ikiwa na vurugu licha ya kuripotiwa katika mamlaka husika hakuna jitihada zilizochukuliwa.
 
Alisema kwa sasa wanasheria wanaendelea na mikakati ya kuandaa kesi na muda wowote shauri hilo litafunguliwa katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Tabora ili haki iweze kutendeka na kila mgombea apate kura halali alizopigiwa na wananchi.
 
“Uchaguzi huu haukuwa huru na haki rushwa zilitolewa sana,vurugu na udanganyifu mkubwa katika vituo mbalimbali hivyo tunaona sasa njia mbadala ya kupata haki zetu ni mahakamani na hapa sitoweza kusema hoja zote hapa lakini ushahidi umekamilika na muda wowote tutapanda mahakamani,” alisema.
 
Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Nzega, Omary Omary ambaye ni Diwani wa kata ya Bukene aliwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hicho wakati chama hicho kinapinga matokeo ya ubunge mahakamani.
 
Alisema kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro nyingi ambazo zitaweza kutatuliwa na Mahakama na kuongeza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea na shuguli zao za maendeleo ikiwa na kudumisha amani na utulivu.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More