Friday, November 17, 2017

DC KASESELA AONGOZA OPARESHENI KWA WAFANYABIASHARA WASIOTUMIA EFD

Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela akiongozana na meneja wa TRA na maafisa wake mkoa wa Iringa akikagua matumizi ya mashine za kutolea risiti.

NA DENIS MLOWE, IRINGA
 
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ameongoza opareshEni kubwa ya kuwasaka wafanyabiashara wasiotumia risiti za mashine (EFD) katika madukani mbalimbali manispaa ya Iringa.
 
Katika oparesheni hiyo iliyofanywa katika eneo la Miyomboni ilihusisha wafanyabiashara wa maduka mbalimbali ambapo wengi wao wamekutwa na makosa ya kutotumia mashine hizo katika uuzaji wa bidhaa au wakati mwingine kuandika bei ya chini kuliko bidhaa.
 
Akizungumza mara baada ya oparesheni hiyo, Kasesela amewataka wafabiashara kutumia mashine za kutolea risiti kila wanapouza bidhaa zao na jamii kudai risiti kila wakati baada ya kubaini asilimia kubwa hawatumii EFD mara kwa mara..
 
Alisema kuwa serikali inawategemea sana wafanyabiashara kulipa kodi lakini serikali haitasita kuwachukulia hatua wafanyabiashara wasiolipa kodi zao kwani wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
 
Kasesela alisema kuwa changamoto ambazo wamezibaini kwa wafanyabiashara hao ni kutotumia mashine mara kwa mara na kuwataka TRA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa wafanyabiasharac wote na wakibainika wasiotii sheria wafungiwe maduka yao.
 
Katika oparesheni hiyo jumla ya maduka mawili yalifungiwa ambapo Kasesela aliwapatia siku tatu kuhakikisha wanamaliza kulipa kodi, na kubadilisha majina ya umiliki wa biashara kwa mamlaka mapato Tanzania.
 
Kwa upande wake Meneja mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa, Lampson Tulianje amesema kuwa wafanyabiashara wa wengi wana mwitikio mdogo wa kutoa risiti za EFD baada ya kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali na kubaini hilo.
 
Tulianje alisema kuwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa zao pasipo kuwapatia risiti za mashine za Kielektroniki (Efd) wateja wao mara kwa mara hali inayokosesha TRA mapato hivyo pindi wakibainika wanafikishwa katika vyombo vya sheria na kuchukua mali zao hadi wamalizapo.
 
Alisema kuwa kampeni hiyo imeendelea kufanyika katika maduka yote mkoani hapa kwa kushtukiza hali ambayo wanakutana nayo ni wafanyabiashara hao kutoa risiti kwa wateja wachache tofauti na wanavyowahudumia wateja wengi kwa siku.
 
Alisema kuwa kutona na hali hiyo TRA mkoa wa Iringa itaendelea kufanya zoezi hilo kuhakikisha wafanya biashara wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za biashara katika mauzo ya bidhaa zao kwa kutoa risiti kwa kila mteja wanayemhudumia.
 
Tulianje alisema kuwa kila bidhaa inayouzwa inapaswa kutolewa risiti, zikiwamo bia hivyo, maafisa wa TRA watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wafanyabiashara wote ambao wanahitajika kutumia mashine hizo wanatumia ili kuingizia mapato serikali.
 
"Lengo la TRA sio kuwafungia biashara hawa wafanyabiashara lakini endapo watashindwa kufata sheria hatua stahiki zitachukuliwa bila hofu yoyote na hatupendi kuwapiga faini lakini italazimika kufanya hivyo, kwani tunasimamia sheria na imeonekana idadi kubwa ya wafanyabiashara mkoani hapa hawatumii mashine za EFD kama ambavyo inatakiwa,"alisema.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More