Wednesday, December 13, 2017

KATIBU MARCO MBAGA: TUTASHINDA KWA KISHINDO UCHAGUZI WA KATA YA KIHESA

 Akizungumza na blog hii ofisini kwake eneo la sabasaba katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa  Marco Mbaga akiwahakikishia wananchi na wanachama wa chama cha mapinduzi (CCM) kuwa watashinda katika uchaguzi mdogo wa kata ya Kihesa.

Na Fredy Mgunda,Iringa

VYAMA vya siasa vyenye ushindani katika medani za siasa nchini, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) vimeanza majigambo ya kushinda uchaguzi wa mdogo wa kata ya Kihesa mkoani Iringa.
 
Pamoja na manispaa ya Iringa na kata ya kihesa kujulikana kama ngome imara ya kisiasa kwa vyama vya upinzani hususan CHADEMA, safari hii viongozi wa CCM wamejiapiza kwa gharama yoyote wataisambaratisha ngome hiyo kwa kushinda kata hiyo kwa ushindi wa kishindo tena zaidi hata walioupata katika kata ya Kitwiru

Akizungumza na blog hii ofisini kwake eneo la sabasaba katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Manispaa ya Iringa  Marco Mbaga alisema pamoja na kwamba hawajaanza kampeni, lakini Chama chao kina uhakika wa kushinda Kata hiyo kwa kishindo

Katika mahojiano hayo, Mbaga alizifananisha kampeni za CHADEMA ambazo kuwa ni sawa na baiskeli ya mbao ambayo hata ikitangulia kuanza safari haitafika mbali itakuwa imeachwa na chombo chenye kasi (CCM) na kufika mwisho wa safari ya ushindi.

“Hapa ninapozungumza na wewe tupo kwenye vikao vya mkakati wa kufanikisha ushindi katika Kata hiyo,wenzetu CHADEMA tayari wameenda kuchukua fomu ya mgombea wao sisi bado lakini nikuhakikishie tumewatanguliza kama baiskeli ya mbao ambayo tutaipita wakati haijafika kokote,”

Aidha alipoulizwa sababu za kujiamini wakati Kata hiyo iliyokuwa mikononi mwa CHADEMA kabla ya diwani waliochaguliwa kujiuzulu kwa kile kilichodaiwa na Mbunge wa Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa ni kununuliwa na CCM, Mbaga alisema washindani wao hawana sera.

“Washindani wetu hawana sera wala ajenda mahususi ambayo wataitumia kuwashawishi wapiga kura ambao kwa mujibu wa utafiti mdogo niliofanya tayari wameng’amua kuwa CHADEMA hawawezi kuwaletea maendeleo zaidi ya kuwatukana majukwaani viongozi wakuu wa kitaifa akiwemo Dk. John Magufuli.

“Hivi jiulize ni mpiga kura gani atakuwa tayari kumchagua kiongozi ambaye ni lazima baadaye atakwenda kuomba hela za kujenga miundombinu ya barabara, maji ,afya na elimu huku akifahamu ilani inayotekelezwa ni ya chama kilichoshika dola ambayo kwa sasa ni CCM?” alihoji Mbaga.

Kuhusu uwezekano wa nafasi finyu ya  ushindi wa chama chake bila kusaidiwa na vyombo vya dola , Mbaga aling’aka na kushangazwa na madai hayo kwa kile alichosema kuwa ni jambo lisilowezekana katika ulimwengu wa teknolojia.

“Vyama vyote vinao mawakala katika vituo huku kura zikijumlishwa na matokeo kusambazwa katika mitandao hata kabla ya majumuisho,hizi ni dalili za kushindwa hata kabla kura hazijapigwa ,sisi tutashinda kihalali kwa vile serikali inayoongoza inatimiza wajibu wake na wananchi hasa wapiga kura wanaona kwa macho yao ,watatuchagua kwa hayo sio vinginevyo “ alisema Mbaga.

Aidha Mbaga alisema kuwa wamedhamilia kufukuza panya  wote katika manispaa ya Iringa ili kuondoa usumbufu unaojitokeza katika kuleta maendeleo kwa wananchi ambao bado wanaimani na chama cha mapinduzi

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More