Wednesday, December 9, 2015

UKAWA Wajazana Kortini Kanda ya Ziwa Kutetea Nafasi zao za Ubunge

KESI za kupinga matokeo ya ubunge zimezidi kumiminika katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, ikiwamo za kupinga matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya (Chadema). 
 
Kesi nyingine zilizofunguliwa mahakamani ni za majimbo ya Nyamagana, Ilemela na jimbo la Kwimba, ambapo walalamikaji wamewasilisha malalamiko mbali mbali ikiwamo ya vitendo vya rushwa.

Kesi ya kwanza iliyofunguliwa ni ya ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini ambayo imefunguliwa na Magambo Masato na wenzake watatu wakipinga matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo hilo, Ester Bulaya.

Kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2015 mara ya kwanza ilifunguliwa Novemba 18 mwaka huu, juzi ilikuwa mara ya kwanza kupelekwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo ambayo ipo kwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe, walalamikaji wa kesi hiyo wamewasilisha malalamiko mahakamani hapo wakidai kwamba Bulaya alipata ushindi kwa njia ya rushwa.

Bulaya aweka pingamizi
Mlalamikiwa katika kesi hiyo, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya, mapema juzi aliwasilisha hoja za msingi kuweka pingamizi kwa walalamikaji kufungua kesi mahakamani.

Hoja alizowasilisha Bulaya ni kwamba walalamikaji hawana mamlaka ya kufungua na kuendesha kesi ya aina hiyo kwani hawajaonesha ni namna gani imeathiri haki zao kama wapiga kura.

Pili katika shauli walillowasilisha mahakamani hawakuonesha ni namna gani vitendo vya rushwa walivyodai vilikuwa vikifanywa na Mawakala wa Bulaya havijaoneshwa, pia shauri hilo limekiuka kifungu cha 12 (D) cha sheria ya uchaguzi.

Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29 mwaka huu, itakapo tajwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kuisikiliza.

Kesi ya Wenje
Aliyekuwa Mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza, Ezekiah Wenje, juzi alitinga Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, kuomba kupunguziwa gharama za uendeshwaji wa kesi.

Pia Wenje katika kesi hiyo anawashitaki, Mbunge wa Nyamagana Stanslaus Mabula (CCM), Msimamizi wa Uchaguzi huo, Tito Mahinya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo amewasilisha malalamiko mahakamani hapo kwamba uchaguzi huo haukuwa haki na huru, kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Hata hivyo katika kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2015, Wenje aliwakilishwa mahakamani hapo na Wakili Outa na upande wa walalamikiwa waliwakilishwa na Wanasheria wa Serikali, Mtalemwa, Kitia Tuloke na Ajuaye Bilishaga.

Kesi ya Highness Kiwia
Novemba 25 mwaka huu aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Ilemela, Highness Kiwia, alifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi, Angelina Mabula (CCM) pamoja na kuwashitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi huo, John Wanga.

Kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2015, mlalamikaji katika kesi Kiwia hakufika mahakamani hapo, ambapo kwa upande wa walalamikiwa waliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Malongo.

Kesi ya Wenje na Kiwia zimeahirishwa ampapo ya Wenje itatajwa Desemba 10 mwaka huu na ya Kiwia hadi Desemba 14 mwaka huu, huku Msajili, Kabwe amedai kuwa endapo siku hiyo mlalamikaji Kiwia hatatokea kesi itatupiliwa mbali.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More