Monday, December 7, 2015

Ofisa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Atiwa Mbaroni Kwa Kuruhusu Usafirishaji wa Magogo 665

POLISI mkoani Rukwa inamshikilia Ofisa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Michael Mwingira ili kusaidia uchunguzi wa magogo 665 na mbao za mti wa mkurungu vilivyokuwa vinasafirishwa kinyume cha sheria kwenda China.

Mwingira ni Ofisa Forodha wa TRA katika Kituo cha Forodha kilichopo kijijini Kasesya wilayani Kalambo mkoani Rukwa katika mpaka wa Tanzania na nchi jirani ya Zambia. Hata hivyo, kwa mujibu wa maofisa wa TRA na Misitu mkoani Rukwa thamani ya magogo na mbao zilizokamatwa haijaweza kufahamika mara moja.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Said Magalula alimwamuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda kumtia mbaroni ofisa huyo wa TRA ili asaidie uchunguzi; pia aliamuru ahamishwe mara moja na kupangiwa kituo kingine cha kazi. 
 
Aidha, amempa wiki moja Ofisa Upelelezi Mkoa wa Rukwa (RCO) awe amekamilisha uchunguzi wa tukio hilo na kumkabidhi matokeo yake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Polisi mjini Matai wilayani Kalambo ambako lori lenye namba ya usajili T 427 ASG aina ya Scania limekamatwa likiwa limebeba kontena lenye idadi ya magogo 350, Magalula alisema imebainika magogo hayo yamesafishwa kwa kutumia hati bandia za mauzo ya nje.

“Tumeshabaini kuwepo kwa muda mrefu kwa mtandao wa kihalifu unaovuna rasilimali zetu za misitu, kuandaa nyaraka bandia za kusafirisha magogo nje ya nchi ….usafirishaji wa magogo haya kati ya Tanzania na Zambia ulishapigwa marufuku kuwa hayaruhusiwi kuuzwa nje ya nchi,” alisisitiza Magalula.

Baada ya kukagua lori hilo linaloshikiliwa katika Kituo cha Polisi mjini Matai likiwa na kontena lenye magogo hayo, Magalula aliamuru msafara wake ufike katika Kituo cha Forodha kilichopo mpakani mwa nchi ya Zambia katika kijiji cha Kasesya umbali wa kilometa 47 kutoka Matai Mjini.

Katika Kituo hicho cha Forodha cha Kasesya, Magalula alishangazwa baada ya kubaini magogo mengine na mbao vyote kwa pamoja vikiwa 315, vikiwa vimehifadhiwa karibu na jengo la forodha hiyo.

Magogo hayo yanayodaiwa kuwepo hapo kwa muda mrefu ambapo tayari yalikuwa yamebanguliwa kwa kusafirishwa China pamoja na mbao zake licha ya maofisa wa TRA kusisitiza kuwa ni sehemu ya magogo yaliyokamatwa juzi na kuzuiwa katika Kituo cha Polisi mjini Matai.

“Inasikitisha sana maofisa wa Polisi , Uhamiaji na mazao ya misitu mlioaminiwa kuulinda mpaka huu mmeshindwa kufanya hiyo ….. nitawataarifu waajiri wenu ili wawachukulie hatua za kinidhamu pia kisheria …. Mmeshindwa kutimiza majukumu yenu ipasavyo,” alisisitiza Magalula.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Wilman Ndile alieleza kuwa miti ya aina hiyo ya mkurungu ambayo inapatikana kwa wingi wilayani humo kuliko sehemu nyingine nchini, imepata soko lenye ushindani mkubwa katika nchi za Mashariki ya Mbali.

“Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Kalambo iliweka mtego na kubaini kuwa miti inaibwa kwa kuvunwa usiku wilayani kwetu kisha inavushwa hadi nchi jirani ya Zambia na kusafirishwa Mashariki ya Mbali kupitia kituo chetu cha forodha kiujanja ujanja kwa hati bandia,”alisisitiza DC.

TRA imekumbwa na kashfa kubwa katika siku za karibuni ukiwamo upotevu wa makontena zaidi ya 2,800 ambayo hayajalipiwa ushuru wa mabilioni ya Shilingi, hali iliyosababisha kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani kwa maofisa wake wa ngazi za juu akiwamo Kamishna Mkuu Rished Bade aliyesimamishwa kazi na Rais John Magufuli.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More