Friday, December 4, 2015

Sijachangiwa na Mfanyabiashara Yeyote Kuingia Ikulu.


Rais Dk. John Magufuli, amesema hakuna mfanyabiashara aliyemchangia  kumuwezesha kuingia Ikulu katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, ili aweze kusimamia ipasavyo makusanyo ya kodi kwa faida ya wananchi.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta binafsi, katika kikao cha pamoja kilichoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Baraza la Biashara la Taifa ( TNBC) kwa ajili ya kufahamiana.

Alisema wakati wa kampeni hadi kufikia siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu, hakupokea senti yoyote kutoka kwa wafanyabiashara kwa kuwa alijua akiingia madarakani anakwenda kufanya kazi tu.

“Nilijiepusha na fedha, mchango wowote kutoka kwa wafanyabiashara, kama yupo mfanyabiashara yeyote alinichangia hata shilingi mbili asimame hapa aseme, nilikwepa kwa sababu nilitaka iwe kazi tu,”alisema.

Rais Magufuli aliwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa kuweka mbele maslahi ya umma, ili kuwasaidia wananchi wanyonge badala ya kushirikia kuwakandamiza.

Alisema Tanzania ni tajiri na ina rasilimali nyingi, lakini kinachokosekana ni kushindwa kuweka mbele maslahi ya umma

Alisema anatambua sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa katika kujenga uchumi na kazi kubwa ya serikali katika uchumi wa soko ni kujenga mazingira mazuri kwa sekta binafsi.

“Napenda kuwahakikishia kuwa serikali ya awamu ya tano itajenga mazingira mazuri zaidi kwa ajili ya ustawi wa sekta binafsi, nitapunguza na kuondoa vikwanzo na urasimu unaokwamisha uwekezaji wa biashara nchini,” alisema.

Rais Magufuli pia alisema ataangalia uwezekano wa kupunguza utitiri wa kodi na ushuru ambao umekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara na wananchi.

Alirejelea mfano wa mkoa wa Kilimanjaro na Kagera wakati wa kampeni alipewa kilio cha wakulima wa zao la kahawa kutozwa kodi zaidi ya 26 na kusababisha kusafirisha kwa njia ya magendo kwenda Uganda.

“Soko la kahawa duniani ni lilelile, lakini Uganda hawana kodi hizi, biashara nyingine ni biashara ya sukari, tukiungana pamoja na kufanya kazi pamoja kwa kuweka mbele maslahi ya taifa nchi hii itaendelea,”alisema.

Akizungumzia sekta ya Benki, Rais alisema anafahamu kuwa Tanzania kuna benki 54 ambazo zote zinafanya biashara na serikali lakini hazijajikita maeneo ya vijijini ambako ndiko kuna wananchi.

“Nimefanya uchambuzi fedha zilizowekwa na mashirika ya umma ambazo ni fedha za serikali ni zaidi ya Sh. bilioni 550, benki zinachukua kiasi cha fedha na kwenda kuziweka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hapa inakuwa benki inafanyabiashara na serikali kwa kutumia fedha za serikali, hivyo ni sawa na serikali kufanya biashara kwa fedha zake,”alisema.

Rais alisema mashirika mengine yamewekeza fedha kwenye benki hizo na hazizalishi riba yoyote.

Kuhusu sekta ya viwanda,Dr. Magufuli alisema inashangaza kuona Tanzania ina mifugo mingi inayoweza kuzalisha ngozi kwa wingi lakini hakuna viwanda vya ngozi vinavyozalisha na kutengeneza viatu inashindwa na Ethiopia ambayo haina ngozi.

“Kuna umuhimu gani viatu vya kuvaliwa na wanajeshi, wananchi na hata sisi tuagize kwa nchi ambazo hazina ng’ombe, unajua wenzetu wanatucheka sana na kutuona hatufai,” alisema.

Alisema vipo viwanda vilivyobinafsishwa na vingine vimegeuzwa sehemu ya kuhifadhi mifugo, huku akitolea mfano wa mji wa Morogoro ambao ulikuwa mji wa viwanda lakini kwa sasa vyote vimekufa.

“Mfano mkoani Arusha kuna kiwanda kinakusanya maziwa ya ng’ombe kutoka kwa wafugaji, lakini yanapelekwa Kenya kuyahifadhi kwenye vifungashio na kuyarudisha nchini kuuza, ingewezekana kabisa kufungashia nchini na kuuza,’ alisema na kuongeza:

“Serikali tupo, sekta binafsi tupo, TNBC wapo, makatibu wakuu wapo, wawaziri wapo na rais nipo. Nazungumza hivi siyo kwamba nafurahi, inasikitisha, nazungumza haya kwa kuwa najua hakuna Tanzania kama hakuna nyinyi,” alisema.

Akizungumzia sekta ya utaliii,Rais alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ambavyo vinaweza kuliingizia taifa fedha nyingi, lakini kuna ujanja mwingi ikiwamo wageni kulipa fedha kwenye nchi zao na kuja nchini kutalii, jambo ambalo linaikosesha serikali mapato.

“Unaweza kusema watalii milioni 1.1 wameingia nchini na kujiwekea malengo ya watalii milioni mbili, tujiulize wanaingiza shilingi ngapi, wanalipia nchini au kwao, wanaweza kuacha fedha kwao alafu nyie mnakuja kuona sura zao na kuhesabu idadi, ni afadhali wakaja watano lakini tukapata fedha nyingi,” alisema. 
  
Alisema ni lazima kujiuliza kwanini Misri inapata watalii wengi na haina vivutio vingi kama Tanzania, hivyo ni lazima vikwazo vyote vikaondolewa nchini.

Aidha, Rais aliwataka wafanyabiashara hao kujenga viwanda vya kusindika samaki katika ukanda wa kusini, kwa kuwa kuna eneo la kutosha kwa ajili ya kazi hiyo.

Alisema Bahari Kuu kuna raia wa nje wanaendesha uvuvi haramu na wana meli kubwa zenye viwanda vya kusindika samaki ambazo husafirishwa kwenda nje moja kwa moja, jambo ambalo linaweza kufanywa na wafanyabiashara au wawekezaji wa Tanzania.

Rais alisema amechoka kuona Tanzania inachezewa na kugeuzwa shamba la bibi na wafanyabiashara wake wakidharauliwa mbele ya nchi nyingine na kwamba wakati umefika wa kuwekeza ili kujenga heshima ya nchi na kukuza uchumi wa Taifa.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More