Sunday, December 6, 2015

RC amsihi Yussuf Manji akubali kuachia Coco Beach

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amemuomba mmiliki wa Kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na mfanyabiashara Yussuf Manji kutumia busara kukubali kuuachia ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sadiki alisema Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi katika uamuzi wake imeiamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni ya Q Consult kwa ajili ya kampuni hiyo kuendeleza ufukwe huo hata hivyo Manispaa ya Kinondoni imekata rufaa.

“Kampuni ya Q Consult kwa busara tu iachane na kesi, ikubali kurudisha ufukwe huo chini ya mamlaka ya Kinondoni ili iweze kuuendeleza ufukwe huo kwa manufaa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na sio kwa manufaa ya mtu mmoja kama anavyotaka mtu huyo,” alisema Sadiki.

Alisema wananchi wafahamu kuwa ufukwe huo wa Coco haujauzwa, kama watu wanavyodai na kwamba kesi hiyo iko mahakamani, ambapo Ofisi ya Manispaa ya Kinondoni kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekata rufaa.

Akielezea sakata hilo, Sadiki alisema kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na Manji mwaka 2007 iliingia mkataba na Manispaa ya Kinondoni kuendeleza ufukwe huo.

Alisema, hata hivyo, baadaye Manispaa ya hiyo ilivunja mkataba huo baada ya Kampuni ya Q Consult kushindwa kutimiza masharti, jambo ambalo liliifanya kampuni hiyo kwenda mahakamani.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi iliamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni hiyo kwa ajili ya kuendeleza ufukwe huo.

“Kama nilivyosema kupitia mwanasheria mkuu wa Serikali tumekata rufaa katika uamuzi huo kwasababu tunaamini haukuwa sahihi, hata hivyo mwekezaji huyo namshauri tu anaweza kufanya maamuzi akaachana na kesi hiyo na kuamua kurudisha ufukwe huo uendelee kutumiwa na Watanzania wote,” alisema Sadiki.

Kwa kampuni hiyo kushinda kesi hiyo, inamaanisha kuwa mwekezaji huyo endapo ataendeleza eneo hilo, wananchi hawatakuwa na fursa hiyo tena, kama wanavyoutumia sasa.

Sadiki alisema tayari serikali imefanya mazungumzo na moja na benki hapa nchini kwa ajili ya kupata mkopo, ambao utasaidia kuendeleza eneo hilo ili liendelee kubaki chini ya Manispaa ya Kinondoni na kutumiwa na watu wote.

HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More