Friday, October 30, 2015

Mambo Yaliyombeba Dr. Magufuli Kushinda Urais Wa Tanzania

Tanzania  imeandika historia mpya, ambapo jana imempata Rais Mteule wa Awamu ya Tano, Dk John Pombe Magufuli, ambaye alikuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu uliohitimishwa Jumapili ya Oktoba 25, mwaka huu.

Dk Magufuli ambaye katika kampeni ya kuwania urais alikuwa na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, si mgeni katika safu za uongozi wa Tanzania kwa kuwa amekuwa serikalini kwa miaka 20, akishika majukumu mbalimbali ambayo yalitumiwa na Watanzania kumpima.

Moja ya sifa yake kubwa tangu alipotangaza nia ya kugombea urais kupitia chama hicho mwishoni mwa Mei mwaka huu, ni uadilifu katika utendaji kazi wake katika majukumu tofauti aliyokabidhiwa Rais huyo mteule wa Awamu ya Tano, anatajwa kuwa katika majukumu yote ya kitaifa aliyowahi kukabidhiwa, alionesha sifa ya juu ya uaminifu na uadilifu, ambao umeelezwa kwa namna mbili tofauti.

Ujenzi barabara 
Kwanza ni uongozi wake wa miradi mikubwa ya fedha nyingi, ambayo kwa muda wote wa uongozi wake hakuwahi kukumbwa na kashfa. Kwa mfano mwaka huu tu, alikuwa akiongoza Wizara ya Ujenzi, iliyokuwa na bajeti ya Sh trilioni 1.2 na Mfuko wa Barabara uliokabidhiwa zaidi ya Sh bilioni 866.

Katika miaka 15 aliyoongoza Wizara hiyo ya Ujenzi, katika ngazi hiyo alisimamia miradi ya zaidi ya Sh trilioni 9.5, lakini hakula hata senti tano, badala yake alijenga mtandao mrefu wa barabara za lami nchi nzima.
 
 Usimamizi 
Namna ya pili ya kuzungumzia uadilifu wake ni usimamizi wake wa watendaji na wadau wa sekta ya ujenzi, ambao amekuwa akiwapa kazi za mabilioni ya shilingi na kuisimamia kwa karibu katika kuwatumikia Watanzania.

Dk Magufuli amekuwa akisimamia makandarasi zaidi ya 8,500, wahandisi zaidi ya 15,000 na wakadiriaji majengo zaidi ya 1,300, ambao wamekuwa wakinufaika na kazi za Serikali za mabilioni ya shilingi.

Kama angetumia vibaya nafasi hiyo na angetaka kumuomba au kushinikiza kila mmoja wao ampe Sh milioni moja tu kwa mwaka, angeweza kujikusanyia pato binafsi lisilo halali la zaidi ya Sh bilioni 100 kila mwaka. Pamoja na kuwa karibu na kishawishi hicho, lakini Dk Magufuli hakushiriki kuhujumu hata senti moja na hana historia wala hakuwahi kutajwa popote kutumia vibaya nafasi yake hiyo katika sekta yenye maslahi makubwa ya kifedha.

Ukali kwa wazembe 
Badala ya kuomba michango ya kujinufaisha kutoka kwa wadau hao wa ujenzi, Dk Magufuli alijikuta akifukuza kazi makandarasi zaidi ya 3,000 wa ndani na nje ya nchi, bila kujali utajiri wao, pale makandarasi hao walipozembea kazi au kufanya kazi chini ya kiwango.

Namna ya tatu inayotumika kuelezea uadilifu wa Dk Magufuli, imeelezwa mara kadhaa na Jaji Joseph Warioba, ambapo alisema mwaka 1996 alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuongoza Tume ya Kero za Rushwa, alikuta sekta ya ujenzi ikinuka rushwa kubwa. Lakini, anafafanua kuwa baada ya Dk Magufuli kuanza kufanya kazi katika sekta hiyo, kelele ya rushwa katika sekta hiyo imetoweka. Uchapakazi Mbali na uadilifu, Dk Magufuli pia anatajwa kuwa mchapakazi.

Hata Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi mara kadhaa amempa jina la ‘simba wa kazi’, huku Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake, akimpa jina la ‘tingatinga’ ambalo huwa halishindwi kazi katika mazingira yoyote ya ujenzi, huku wananchi wengine wakimuita ‘jembe’. Matokeo ya uchapakazi wake, yanaonekana katika sekta ya ujenzi, alikofanya kazi kwa miaka 15 tu, ambapo amefanikiwa kusimamia ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa zaidi ya kilometa 17,700.

Kazi hiyo imeweka historia ambayo hata wakoloni, Wajerumani na Waingereza, waliotawala Tanganyika wakati huo tangu mwaka 1884/1885 mpaka wakati wa Uhuru mwaka 1961, zaidi ya miaka 75 walijenga mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilometa 1,360 tu. 
 
Wasifu wake
Dk Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 Chato (sasa Mkoa wa Geita), hivyo jana alipotangazwa kuwa Rais Mteule wa Awamu ya Tano, ilikuwa siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake, ambapo alitimiza miaka 56.

Dk Magufuli ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka 1991 – 1994 alisoma Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza. Mwaka 1985 – 1988 alisoma Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemia na Hisabati. Mwaka 1981 – 1982 alisoma Diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.

Kati ya mwaka 1979 – 1981 alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Juu ya Sekondari Mkwawa, Iringa. Mwaka 1977 – 1978 alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza. Mwaka 1975 – 1977 alisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera. Mwaka 1967 – 1974 alisoma Shule ya Msingi, Chato. Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mpwapwa mkoani Dodoma.

Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha. Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma. 
 
Uzoefu wa kazi 
Kuanzia mwaka 2010 alikuwa Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato. Mwaka 2008 – 2010 Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato). Mwaka 2005 – 2008 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato).

Mwaka 2000 – 2005 Waziri wa Ujenzi, na Mbunge wa Biharamulo Mashariki. Mwaka 1995 – 2000 Naibu Waziri wa Ujenzi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki. Mwaka 1989 – 1995 Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Co-operative Union (Ltd) Mwanza. Mwaka 1982 – 1983 Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati). Amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa. Ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Ameoa na ana watoto kadhaa.
 
 Mchakato wa urais 
Dk Magufuli alitangaza rasmi nia yake ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwishoni mwa Mei mwaka huu, baada ya CCM kutangaza rasmi ratiba ya mchakato wa urais kwa wanachama wake. Aliingia kwenye harakati za kuwania nafasi ya urais kimya kimya, tofauti na makada wengine wa CCM ambao walihutubia Taifa.

Lakini, kimya chake kiliufanya mchuano wa uchaguzi wa nafasi hiyo ndani ya CCM, uliokuwa na wagombea 42 kuwa mkali zaidi. Baada ya hapo, waliorejesha fomu walikuwa wagombea 38 na kati ya hao baada ya kujadiliwa na vikao vya juu vya Chama, ikiwemo Kamati Kuu, wagombea watano - Dk Magufuli, Bernard Membe, Dk Asha Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ally na January Makamba, ndio waliofanikiwa kupelekwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.

Baada ya Nec, ambako wagombea hao walijadiliwa na kupigiwa kura, Dk Magufuli, Balozi Amina na Dk Migiro ndio waliofanikiwa kuingia tatu bora, ambapo walifikishwa katika Mkutano Mkuu na kuomba kura na baada ya kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano huo, akapatikana Dk Magufuli kupeperusha bendera ya CCM.
 
 Ahadi zake Dk
 Magufuli katika mikutano yake ya kampeni, alikuwa akiahidi kushusha bei ya vifaa vya ujenzi hasa saruji, mabati na misumari, ili wananchi aliosema atapigania kila mmoja awe na kazi ya kumpa kipato, wajenge nyumba bora.

Katika kuongeza idadi ya Watanzania wanaofanya kazi ili kufikia lengo hilo, Dk Magufuli alisema katika kila mtaa na kijiji, Serikali yake itatoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ndogo za wanawake na vijana. Mbali na kutoa mikopo hiyo izunguke katika ngazi ya kijiji na mtaa, Dk Magufuli pia alisema Serikali yake itazuia kila aina ya usumbufu, unaofanywa kwa wafanyabiashara hao, ikiwemo kukamatwa kwa bodaboda na mama ntilie.

Kwa wakulima, alisema atahakikisha pembejeo sahihi zinatolewa kwa wakati na mazao yatakayovunwa, itakuwa marufuku kwa Serikali kukopa mazao yao kwa kuwa atahakikisha mbali na wakulima kupata bei nzuri ya mazao yao, watakapoiuzia Serikali itakuwa bidhaa kwa fedha taslimu. 
 
Aidha, aliahidi kuondoa ushuru unaosumbua wafanyabiashara wadogo na wakulima, ili wafanye biashara kwa uhuru wajipatie kipato halali.

Dk Magufuli pia alisema baada ya kusambaza umeme, atahakikisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vinajengwa vijijini ili kusindika mazao ya kilimo shambani ili kutoka shambani bidhaa za mazao hayo ziuzwe katika masoko ya ndani na nje ya nchi. 
 
Kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, Dk Magufuli aliahidi kukabiliana na migogoro hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa ardhi zaidi kwaajili ya wakulima na wafugaji, ili kuondoa uhaba wa ardhi uliosababisha ugomvi wa maeneo ya kulishia mifugo na kulima.

Lakini pia aliahidi kunyang’anya mashamba ambayo yamehodhiwa na watu bila kutumiwa, na kuyagawa kwa wakulima na wafugaji wasio na maeneo ya kilimo. 
 
Katika elimu, alikuwa akiahidi kuhakikisha kuanzia mwakani, wanafunzi kutoka darasa la awali mpaka kidato cha nne, wanasoma bila kulipa ada, ili kuondolea wazazi usumbufu wa watoto wao kurudishwa nyumbani kwa kukosa ada.

Kwa wanafunzi wa elimu ya juu, aliwahakikishia kuwa hakutakuwa na usumbufu wa kupata mikopo na kuwataka wanahusika na kazi hiyo, kuwa tayari kwa kuwa atataka kila mwenye sifa ya kusoma elimu ya juu, apate mkopo.
 
 Katika sekta ya afya, aliahidi kujenga zahanati kwa kila kijiji na mtaa, kituo cha afya kwa kila kata na hospitali ya rufaa katika kila mkoa, na ameahidi kukomesha kero ya kukosekana dawa katika hospitali za Serikali.

Katika kero ya maji, alikuwa akisema kama amefanikiwa kujenga zaidi ya kilometa 17,700 za barabara ya lami, hatashindwa kujenga mabwawa na mtandao wa mabomba kwenda kwa wananchi ili kukomesha kero hiyo.

Pia aliahidi kujenga barabara mbalimbali za lami za kuunganisha wilaya na za mijini, huku akiahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi, ifanane na ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), taasisi aliyoianzisha na kuitetea, ambayo leo watu wengi wanatamani kuitumikia kutokana na maslahi mazuri na mafanikio yake.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More