Tuesday, October 27, 2015

CCM Walalamikia Kitendo Cha Maali Seif Sharif Hamad Kujitangaza Mshindi......Wadai Walikamata Kura Feki za CUF Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema, Maalim Seif amevunja katiba na sheria kwa kujitangaza mshindi kabla ya matokeo halali ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec).

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya chama hicho Kisiwandui, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na sheria namba 11 ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kutangaza matokeo zaidi ya Zec.

Alisema bila ya hekima na busara za wananchi, kitendo hicho kingeweza kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani na kuitaka Zec kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mgombea huyo wa urais wa Cuf.

“Tumesikitishwa sana na Zec kushindwa kuchukua hatua ikiwamo kukemea kitendo cha mgombea mmoja kujitangaza mshindi kati ya wagombea 14 wanaowania nafasi hiyo. Tunaomba Tume ya Uchaguzi ifanyekazi kwa mujibu wa katiba na sheria bila ya kumuogopa mtu yoyote,” alisema.

Katika mkutano huo, Vuai aliambatana na Spika wa Baraza la Wawakilishi aliyemaliza muda wake. Pandu Ameir Kifichio, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ na wajumbe wa timu ya kampeni ya mgombea urais wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein. 
 
Aidha, alisema CCM imesikitishwa na tukio la kukamatwa karatasi bandia za kupigia kura katika Jimbo la Chonga, mkoa wa Kusini, Kisiwani Pemba.

Alisema kwamba karatasi hizo zinaonekana zimetegenezwa Afrika Kusini na wakala mmoja wa Cuf katika kituo cha kupiga kura anahusishwa na mpango huo pamoja na msimamizi mmoja wa kituo hicho na kutaka sheria ichukuliwe dhidi ya kitendo hicho

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More