Friday, October 9, 2015

LORI LAUA 7 MBEYA



Watu saba wamefariki dunia baada ya kugongwa na lori la mafuta wakiwa kwenye promosheni ya vinywaji baridi katika Mtaa wa Simike jijini hapa.
Katika ajali hiyo, watu watatu walikufa papohapo na wengine wanne walifia Hospitali ya Rufaa Mbeya, wakati wakipatiwa matibabu.
Daktari wa hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema zaidi ya majeruhi wanne walifikishwa hospitalini hapo kwa matibabu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Nyigesa Wakyo aliwataja waliokufa kuwa ni Rashidi Mwakipololo (21), Rose Osward (7), wakazi wa Simike, Mariam Mwameze (24), Grace Msimba (36), wa Ilemi, Frederick Mwanyila (17) wa Mbozi na watoto wawili wenye umri wa kati ya miaka mitatu na mitano. Aliwataja majeruhi kuwa ni Happy Wener (31), mkazi wa Simike na mtoto Shadrack Joseph (4).
Shuhuda wa ajali hiyo, Ambindwile Kipasi alisema lori hilo lililokuwa na tela liliingia kwenye kundi la watu likiwa kwenye mwendo kasi na kusababisha ajali hiyo.
Kipasi alidai huenda lori hilo lilimshinda dereva baada ya kufeli breki kwenye mteremko unaoanzia eneo la Kadege hadi Kituo cha Jengela.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More