Wednesday, October 28, 2015

JWTZ Yavamia Kijiji Kuondoa Vizuizi Barabarani

Vijana wa Jeshi la Wananchi jana walivamia nyumba za wananchi waliokaribu na barabara kuu ya kutoka Mbeya kwenda Malawi katika wilaya ya Rungwe na kuwataka waamke kuondoa vizuizi vya moto, magogo na mawe vilivyokuwa kwenye barabara hiyo.

Kazi hiyo ilifanywa baada ya  vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Ukawa kuweka vizuzi  vya moto, magogo na mawe kwenye barabara  hiyo  ikiwa ni ishara ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Rungwe.

Wanajeshi walifika Kijiji cha Ndaga saa 4.00 usiku ambako waliyakuta magari yakiwamo mabasi sita yaliyoshindwa kuendelea na safari ya kwenda Tukuyu, Kyela na Malawi baada ya kuwekewa vizuizi.

Vijana wa Jeshi la Wananchi  waliamua kutembea kutoka Ndaga hadi Tukuyu wakitoa vizuizi na kuwaamsha wananchi walio karibu na barabara ili washiriki kazi hiyo huku wakitoa kichapo kwa waliokuwa wakichelewa kuamka.

Waliopigwa ni pamoja na  wagonjwa na wazee kadhaa wakiwamo wachungaji ambao walikutwa wamelala usiku huo.

Kiongozi mmoja wa Kijiji cha Katumba ambaye aliomba jina lihifadhiwe alisema hatua ya jeshi ilitokea baada ya vijana wanaodaiwa kutoka Mbozi,Tunduma na Mbeya mjini wakishirikiana na wafuasi wa Ukawa kufanya vurugu tangu saa 10,00 jioni ya juzi baada ya kutangazwa matokeo ya ubunge katika Jimbo la Rungwe.

Naye  mkazi wa Kijiji cha Kiwira  Tujobe Mwakipu  alisema vijana hao walifanya vurugu bila kuzuiwa na wanasiasa waliogombea ubunge.

Alisema vurugu zilianza baada ya kutangazwa matokeo ya Ubunge ambayo yalimpa ushindi mgombea wa CCM, Saul Amon kwa kura  47,862  akimshinda mpinzani wake wa karibu, John Mwambigija aliyepata kura 43,613.

Alisema vurugu zilianzia Tukuyu mjini ambako vijana walikusanyika kudai matokeo na yalipotangazwa hawakuridhika na kuanza kuchoma barabara kuanzia saa 10 ya jioni.

Akizungumzia yaliyowakuta wazee ,John Mwampi wa Kijiji cha Ntokela  alisema  usiku wa kuamkia jana wananchi wengi walipigwa na wanajeshi  waliovamia nyumba zao kuanzia saa 7.00 usiku hadi 12.00 asubuhi walipomaliza kazi ya kuondoa vizuizi kwenye barabara kuu hiyo maeneo ya Ndaga, Ntokela, Kiwira, KK, Mwabegele  na Katumba.

Mwampi alisema wanajeshi walifika eneo la KK saa 10.30 na kuwaamsha kwa bakora wananchi wenye nyumba zilizo karibu na barabara huku wakiwataka wakatoe mawe, magogo na moto uliokuwa ukiwaka katikati ya barabara.

Naye Mchungaji Yesaya Kilindu wa kitongoji cha Ntupwa katika Kijiji cha KK wilayani Rungwe alisema wanajeshi waliingia kwenye nyumba yake saa 10.00 usiku na kuanza kuwatandika bakora huku wakiwaamuru wakaondoe mawe na magogo kwenye barabara  kuu.

‘’Walituchapa sisi na pia walikwenda nyumba ya Mwalimu chaula ambako waliwapiga na kuiba simu yenye tamani ya Sh200,000’’,alisema na kufafanua kwamba tukio hilo lilikuwa baya.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Moses Mashaka  alipoulizwa  alisema kamati ya usalama ya wilaya ilikuwa ikiendelea kufuatilia nyenendo za vijana na kwamba haikuwa na taarifa za kutoa kwa vyombo vya habari.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Ahmed Msangi alipoulizwa alisema polisi waliwadhibiti vijana waliofanya vurugu na kuwakamata kadhaa, lakini alisita kuzungumzia zaidi akisema bado wanawasaka wengine.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More