Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Spring Valley
iliyoko katika manispaa ya Iringa wakiwa katika mafunzo ya vitendo
shuleni hapo
Wanafunzi wa shule ya wasichana ya Spring valley wakicheza muziki katika sherehe za kumaliza kidato cha nne
NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAZAZI na Walezi wameaswa kuwasomesha watoto wa kike na
kuachana na fikra potofu kuwa kumsomesha mtoto wa kike ni kupoteza rasilimali
fedha kwani maisha ya sasa bila elimu ni changamoto kubwa kwa mtoto wa kike.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kenneth Komba kutoka Idara ya Elimu
mkoa wa Iringa kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza wakati alipokuwa
mgeni rasmi wakati wa mahafali ya kumi kidato cha nne katika shule ya Sekondari
ya Wasichana ya Spring Valley iliyopo Mkoani Iringa.
Alisema kuwa mtoto wa kike akipatiwa elimu kuna uwezekano
mkubwa kwa taifa kuwa na maendeleo kutokana na kuwajibika kwao katika maisha ya
kila siku hivyo wazazi na walezi ni muhimu kuwasomesha watoto wa kike kwa lengo
la kuendeleza ndoto walizonazo.
Alisema kuwa jukumu la kusomesha elimu ya msingi hadi
sekondari ni la serikali lakini wazazi na walezi wanaosomesha shuleni hapo ni
kuisaidia serikali hivyo ipo tayari kupokea changomoto zote katika shule hiyo
na kushirikiana kuzitatua.
Komba aliipongeza shule ya sekondari Spring Valley kwa kuwa
moja ya shule zinazofanya vizuri mkoani hapa kielimu na tabia kwani ni moja ya
shule ambazo idara ya elimu haipati malalamiko ya mara kwa mara kutoka shuleni
hapo.
Aidha Komba aliwataka wahitimu hao kusoma mazingira ya
maisha popote watakapokuwa na kuamua namna ya kujiajiri ili mradi isiwe
shughuli zinazopingana na sheria na maadili ya kijamii, kama vile kuuza madawa
ya kulevya, ukahaba, unyang'anyi na mambo mengine yanayofanana na hayo ambayo
watajiingiza matatani na kuonekana wabaya.
Awali mkuu wa shule ya Wasichana Spring Valley, Adia Mbwanji
alisema kuwa uongozi wa shule hiyo umeweka mikakati mbalimbali itakayotekelezwa
mwaka 2018 ikiwemo ujenzi wa ukuta upande wa Kusini mwa shule, upanuzi wa
maktaba, ununuzi wa gari la shule na kukarabati mifumo ya maji taka na maji
safi.
Alisema kuwa shule hiyo inayomilikiwa na kanisa la Baptist
Convention of Tanzania imejipanga kujenga chumba cha kompyuta na kununua
komputa zenyewe ili kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi kuendana na ulimwengu wa
sayansi na teknolojia.
Kwa upande wao wahitimu kwa kupitia msoma risala, Happy
Njavike walisema kuwa shule hiyo inatakiwa kuboresha ujenzi wa jengo la maabara
vifaa vyake vinunuliwe ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kujifunza kwa
vitendo hasa masomo ya sayansi kwa lengo la kukuza ufaulu na kuongeza ujuzi
katika masomo ya sayansi.
0 comments:
Post a Comment