Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa (Mb) akijibu maswali Bungeni Mjini Dodoma Leo Novemba 10, 2017.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa (Mb) akijadili jambo na Mhe Jenista Joakim Mhagama ambaye ni Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu
Na Mathias
Canal, Dodoma
Serikali imesema kuwa Mpango wa Serikali wa kuwapelekea
wakulima wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma mbegu mpya za Kahawa ni mahususi kwa
ajili ya kuinua uzalishaji kwa kutekeleza Mpango
Mkakati wa Kuendeleza Zao la Kahawa katika kipindi cha miaka 10 yaani mwaka (2011
– 2021).
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa (Mb) amebainisha
hayo leo Novemba 10, 2017 Bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge
wa Jimbo la Mbinga Mhe Martin
Mtonda Msuha (Mb) Aliyetaka kufahamu kuhusu kushuka Kwa takwimu katika miaka ya
hivi karibuni ya uzalishaji wa Kahawa
Wilayani Mbinga kwa mkulima mmoja mmoja (out growers) ambapo alitaja sababu
za mojawapo zilizopelekea kushuka kwa uzalishaji huo kuwa ni pamoja na kuzeeka
kwa miti ya kahawa.
Mhe
Mwanjelwa alisema kuwa Katika mpango huo, utafiti na
usambazaji wa miche bora itatolewa ili kuondokana na miche yenye tija duni na
iliyozeeka. Ambapo Utekelezaji wake unafanyika kwa kushirikiana na wadau
hususani Tanzania Coffee Research Institute (TaCRI).
Alisema, Kituo cha Utafiti na uzalishaji miche cha Ugano kilichopo
Wilayani Mbinga, katika mwaka 2016/2017 kilizalisha na kusambaza miche bora ya
kahawa 270,869 na kazi mpaka hivi sasa inaendelea.
Aidha, Mfuko wa Maendeleo ya Kahawa (Tanzania
Coffee Developemnt Fund (TCDF) umefadhili na kupunguza bei kutoka
shilingi 300 kwa mche mmoja hadi shilingi 150 kwa vituo vyote nchini vilivyoko chini ya TaCRI ili miche hiyo isambae kwa kasi.
Mhe Mwanjelwa alisema mnada wa kahawa huendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Kahawa Na. 23 ya Mwaka 2001 hivyo Serikali
haina mpango wa kuanzisha soko la mnada wa kahawa Wilayani Mbinga au mahali
pengine nchini kwa sababu uwepo wa miundombinu ya mashine ya kielektroniki ya
kuendeshea mnada iliyopo Moshi, maabara ya kuonjea kahawa, wataalamu wa
kuendesha mnada huo, gharama za mnunuzi ambapo atalazimika kwenda katika kila
mnada kama utawekwa kila mahali ambapo kahawa inazalishwa.
Alisema
uzoefu unaonyesha kuwa nchi nyingi duniani huweka mnada sehemu moja tu ili
kurahisisha uendeshaji. Aidha, tangu kuanzishwa kwake kabla uhuru, mnada
uliwekwa Moshi kwa kuwa ndiko kulikuwa na wanunuzi na biashara ukilinganisha na
maeneo kama Kagera ingawa uzalishaji unafikia hadi asilimia 40 ya nchi nzima.
“Mnada
unauza kahawa ikiwa kwenye maeneo ya uzalishaji (Ex-Mbinga, Ex-Mbeya n.k.)
kinachopelekwa Moshi ni sampuli tu kwa ajili ya uonjaji. Aidha, Serikali imeanzisha
Soko
la Bidhaa (Commodity Exchange) ili kupunguza
gharama za uendeshaji wa masoko ya mazao ikiwemo kahawa” Alikaririwa Mhe
Mwanjelwa
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa kifungu Na. 29 (ii) cha Kanuni
za kahawa 2013, ni kosa kwa mtu yeyote
kununua matunda ya kahawa (ripe cherry) hivyo Serikali inakataza biashara ya
kahawa mbichi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa amemuagiza
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma sambamba na wahusika
wengineo wote kwamba hairuhusiwi kabisa uuzaji wa kahawa mbichi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment