Monday, November 27, 2017

JUMIA YATANGAZA KUANZA RASMI KWA KAMPENI YA ‘BLACK FRIDAY’ NCHINI TANZANIA


Meneja Mauzo Jumia Tanzania, Iddy Mkumba, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu kuanza rasmi kwa kampeni ya 'Black Friday hapa nchini inayoendeshwa na Jumia. Kushoto Meneja Uhusiano wa Umma wa kampuni hiyo, Geofrey Kijangwa.


Na Mwandishi Wetu

KAMPENI itadumu kwa muda wa siku 11, kuanzia Novemba 24 mpaka Desemba 4 Itawawezesha wateja kupata ofa za huduma hoteli, chakula na manunuzi ya bidhaa mbalimbali mtandaoni kwa punguzo la mpaka 80% Wateja kuokoa muda kwa kupelekewa bidhaa zao popote walipo kwa malipo nafuu
Dar es Salaam - Novemba 24, 2017. Katika kuelekea kipindi cha msimu wa sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya, Jumia Tanzania imezindua kampeni inayokwenda kwa jina la ‘BLACK FRIDAY’ inayoanza Novemba 24 mpaka Desemba 4 kwa lengo la kuwarahisishia watanzania kufanya huduma na manunuzi mbalimbali mtandaoni kwa punguzo kubwa la bei la mpaka 80%.

Kampeni hiyo ambayo inazihusisha kampuni za Jumia zilizojikita zaidi kwenye huduma na manunuzi kwa njia ya mtandao nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, itawawezesha wateja wake kununua bidhaa mbalimbali kupitia Jumia Market; kufanya huduma za hoteli kupitia Jumia Travel pamoja na huduma ya kuagiza chakula kupitia Jumia Food.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Meneja Mauzo wa Jumia Tanzania, Iddy Mkumba amesema kwamba katika kipindi hiki cha kuelekea msimu wa sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya wameshusha bei za bidhaa zao tofauti kwa punguzo la mpaka 50%.

“Tunafahamu kwamba kipindi hiki watanzania wengi wapo makini sana na namna wanavyotumia pesa zao. Na kwa kupitia ofa hizi kabambe za punguzo la bei kwenye bidhaa mbalimbali wataokoa pesa za kutosha ambazo wanaweza kuzielekeza kwenye matumizi mengine. Kwenye mtandao wetu wa Jumia mteja atajipatia bidhaa tofauti sawasawa na anavyokwenda dukani. Lakini faida kubwa atayoipata ni kuzikuta bidhaa na bei zake zote zikiwa sehemu moja, kuchagua na kufanya manunuzi papo hapo mahali popote alipo,” alisema Bw. Mkumba.
“Kampeni hii itaanza rasmi leo siku ya Novemba 24 na kudumu mpaka Desemba 4. Bidhaa ambazo zinapatikana ni pamoja na vyombo vya umeme kama vile luninga, simu, tablet, kompyuta, feni, pasi, redio, kamera, ving’amuzi na nyinginezo lukuki; vifaa, vyombo na samani za nyumbani; nguo za wanawake, wanaume na watoto; vifaa vya michezi; bidhaa za urembo na vipodozi. Kwa mfano, katika kipindi hiki” cha ‘Black Friday’ simu aina ya Tecno Spark inapatikana kwa Sh. 185,000 kutoka Sh. 240,000; luninga ya ukubwa wa inchi 40 yenye ubora wa LED inapatikana kwa Sh. 683,000 kutoka Sh. 740,000,” aliongezea Meneja Mauzo wa Jumia Tanzania.

Kuhusu ubora wa bidhaa na huduma zinazopatikana kwenye mtandao wao, Bw. Mkumba alihitimisha kwa kusema kuwa, “Wateja wasiwe na wasiwasi juu ya ubora wa bidhaa zetu kwani tunashirikiana na makampuni na wafanyabiashara wanaouza bidhaa halisi kabisa. Kwa kuongezea pia baada ya wateja kuchagua bidhaa wanazozitaka kupelekewa atafanya malipo pale wanapohakikisha zimewafikia. Lengo la kufanya hivyo ni kujenga na kuonyesha uaminifu kwa kile tunachokifanya ukizingatia kwamba sekta ya manunuzi kwa njia ya mtandaoni bado ni ngeni miongoni mwa watanzania walio wengi. Hivyo basi ningependa kumalizia kwa kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hii ya punguzo la bei ili kuokoa pesa. Mbali na jijini Dar es Salaam, tumefungua huduma zetu kwenye mikoa ya Visiwani Zanzibar, Dodoma, Mwanza, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Iringa na Musoma.”
Mbali na manunuzi ya bidhaa tofauti mtandaoni, katika kujiandaa na msimu wa mapumziko ya mwisho wa mwaka Jumia Travel nao wametangaza ofa za punguzo la bei kwenye hoteli mbalimbali nchini la mpaka 80% katika kipindi hiki cha kampeni hii ya ‘BLACK FRIDAY.’

Akifafanua zaidi juu ya ofa hiyo mbele ya waandishi wa habari, Meneja Uhusiano wa Umma wa kampuni hiyo ambayo yenyewe imejikita kwenye huduma za hoteli na ndege kwa njia ya mtandao, Bw. Kijanga Geofrey amebainisha kwamba wao wamedhamiria katika kuwahakikishia watanzania wanafurahia mapumziko yao ya siku chache zijazo kwa gharama nafuu kwenye hoteli mbalimbali wazipendazo.

“Umebakia takribani mwezi mmoja kufikia sikukuu ya Krisimasi na siku kama 36 hivi ili kuumaliza mwaka huu wa 2017 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2018. Wote tunafahamu kwamba kuna baadhi ya watu hupendelea kusafiri na kwenda kupumzika mazingira tofauti na waliyoyazoea ili kufurahia zaidi. Ikiwa ni kama sehemu ya kujipongeza na kutafakari kuumaliza mwaka uliopita lakini ni muda muafaka kwa kujiandaa na mwaka unaokuja mbeleni. Jumia Travel tungependa kuwa sehemu ya kutengeneza na kufanikisha kumbukumbu hizo muhimu kwa wateja wetu kwa kuwapatia punguzo la bei kwenye hoteli tofauti nchini Tanzania ambapo wangependa kwenda kupumzika,” alifafanua Bw. Kijanga.

“Tukiwa tunafanya kazi na hoteli zaidi ya 1000 nchini Tanzania, wateja watapata fursa ya kupata huduma ya malazi kulingana na bajeti waliyonayo. Punguzo linaanzia 10% mpaka 80% kwa hoteli zote Tanzania,” alisema Meneja huyo wa Uhusiano wa Umma na kuhitimisha kwamba, “Lakini kwa wateja ambao watatumia huduma zetu kwa mara ya kwanza, mbali na punguzo la bei tulilonalo sasa pia watajipatia nyongeza ya ofa ya punguzo la 20% zaidi.”
Mbali na Jumia Market na Travel kutoa ofa hizo, nao Jumia Food nao wametoa punguzo la bei la kuanzia 15% mpaka 35% kwa wateja watakaoagiza chakula kupitia mtandao huo. Ofa hiyo ambayo ni maalum kwa ajili ya kampeni hii ya ‘Black Friday’ itawapatia fursa wateja kuagiza chakula na kupelekewa mpaka walipo kwa karibu nusu bei. Kwa mfano, chakula ambacho kilikuwa kinapatikana kwa Sh. 10,000 hivi sasa kinaweza kupatikana kwa mpaka Sh. 8.500 au 6,500!
‘BLACK FRIDAY’ ni jina lisilo rasmi baada ya siku ya kutoa shukrani (Thanksgiving) nchini Marekani ambapo kwa kawaida huwa ni Alhamisi ya nne ya mwezi wa Novemba. Siku hii huchukuliwa kama kuanza kwa msimu wa manunuzi ya bidhaa mbalimbali kujiandaa na Sikukuu za Krisimasi, utamaduni ambao ulianza tangua miaka ya 1952. Wakati wa kipindi hiki maduka mengi na wafanyabiashara hufungua mapema au kwa mara moja huku yakitoa punguzo kubwa kwa bidhaa zao tofauti. Kufuatia umuhimu wa siku hiyo kuna baadhi ya maeneo nchini humo huifanya siku hiyo kuwa ya mapumziko ili kuwawezesha wananchi kufanya manunuzi zaidi. Kutokana na umaarufu na manufaa ya siku hiyo kwa wafanyabiashara na wateja, sehemu mbalimbali zimeiga na imeonyesha mafanikio makubwa kwani tafiti huonyesha kwamba huongoza kwa manunuzi makubwa yanayofanywa na wateja.



0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More