Tuesday, March 15, 2016

Serikali yawapongeza wadau wa afya katika mapambano ya Ugonjwa wa Kisukari nchini

(Imeandaliwa na Andrew Chale, modewjiblog)
DSC_7f173 
Dk. Kigwangalla akipata picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wanaosomea masomo ya Sayansi na udaktari ambao wanapambana na magonjwa ya Kisukari. Dk. Kigwangalla aliwapongeza wanafunzi hao kwa juhudi zao hizo ambapo amewahakikishia juu ya Serikali kuwa na mipango endelevu ikiwemo kuwaendeleza zaidi kwa kushirikiana na wadau na wafadhiri mbalimbali.

DSC_6989 
Dk. Kigwangalla akiagana na viongozi mara baada ya kumaliza kwa ufunguzi wa kongamano hilo linaloendelea leo na kufikia tamati hiyo kesho Machi 16.2016.


Serikali imewapongeza wadau kwa kutoa huduma za chanjo ya ugonjwa wa Kisukari ikiwemo kusaidia vijana wadogo wanaosomea masomo mbalimbali ya kisayansi hapa nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamano la tatu la ugonjwa wa Kisukari kwa nchi za Afrika Mashariki,Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto, Mh. Dkt. Hamisi Kigwangalla, amebainisha kuwa Serikali kupitia wizara hiyo ina mpango kabambe wa kuhakikisha inapambana na tatizo la ugonjwa wa Kisukari hapa nchini ambapo pia amewataka wadau wasichoke kushirikiana katika mapambano hayo.

Aidha, amewapongeza vijana walio katika vyuo vikuu hapa nchini licha ya kupata tiba ya ugonjwa wa Kisukari, lakini kwa hali yao hiyo bado wana moyo wa kusoma kuhakikisha wanafika mbali hivyo Serikali inajisikia faraja na kuwataka wadau kuwa na moyo huo huo wa kusaidiana na Serikali.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wakiwemo vijana wanafunzi na wengine wakiwemo waliotoa igizo namna ya ugonjwa Kisukari jamii unavyouweka kando, wameeleza kuwa kitendo cha dozi ya Kisukari kuuzwa kinawapa shida watu wengi kwani wapo wanaopoteza maisha kwa kukosa pesa za kutumikia dozi hiyo.

Hata hivyo, walimuomba Naibu Waziri Dk. Kigwangalla kuhakikisha Serikali wanaliangalia hilo ili dozi ya Kisukari yaani Insulini, ipatikane bure kwa watumiaji wake.

Kongamano hilo lililozinduliwa jana Machi 14.2016, ni la siku tatu na linatarajiwa kufikia tamati, kesho Machi 16.2016. Ambapo linajumlisha wataalaam wa utafiti wanasayansi katika ugonjwa wa Kisukari ( pre – congress training – applied research in diebetes) na kuandaliwa na asasi inayojulikana kama (EADSG) The Eafrica diabetes study group.
 
Asas hii ilianzishwa mwaka 2011 ili kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa huo na kuutafiti pamoja na kutafuta tiba.

Awali akiongea na waandishi wa Habari, Mratibu wa Kongamano hilo Doctor Kaushik Ramalya, amesema wageni mbalimbali wapo katika majadiliano na uchunguzi huo wa Kisayansi, ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu wa namana ya kutua matatizo yatokanayo na ugonjwa huo.

UTAFITI:
Aidha utafiti uliotolewa hivi karibuni umeonyesha kuwa katika kila sekunde sita mtu mmoja hufa kutokana na ugonjwa wa kisukari ( vifo zaidi ya milioni 5.0 hutokea duniani). Mmoja katika watu wazima 11 ana ugonjwa wa kisukari ( watu milioni 415 duniani kote wanaishi na Kisukari). 

Moja katika vizazi saba, huadhirika na ugonjwa wa kisukari katika kipindi cha ujauzito na kujifungua.Robo tatu (75%) ya watu wenye ugonjwa wa kisukari wanaishi katika nchi chini na kipato cha kati. 

Zaidi ya watu wazima wengi wanakufa kutokana na ugonjwa wa kisukari kuliko kutokana na VVU / UKIMWI, kifua kikuu na hata malaria.wastani wa milioni 14.2 watu wazima wenye umri kati ya 20-79 wana ugonjwa wa kisukari katika Kanda ya Afrika. 

Afrika inaongoza kwa wagonjwa wa kisukari ambao haujatambuliwa, kutokana na kutocheki afya zao; zaidi ya 66.7 % ya watu wenye ugonjwa wa kisukari hawajui kuwa wana ugonjwa wa kisukari. 

Mtu ana kisukari aina ya 2 (Type 2 Diabetes) anaweza kuishi kwa miaka kadhaa bila kuonyesha dalili yoyote, madhara yanayoweza kujitokeza ni pamoja na ugonjwa wa figo , moyo kushindwa kufanya kazi, ugonjwa wa jicho na kusababisha upofu na matatizo ya mguu na kusababisha ulema.

Mataifa ya Afrika kwa idadi kubwa ya watu wenye ugonjwa wa kisukari ni pamoja na Afrika Kusini (2.3 milioni ), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (1.8 milioni ) , Nigeria ( milioni 1.6 ) na Ethiopia (1.3 milioni).

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More