Monday, March 28, 2016

Watu sita wamefariki dunia na wengine zaidi ya 38 kujeruhiwa na kulazwa kwenye hospitali ya rufaa mkoa wa Iringa

 Askari   polisi na  wasamaria  wema  wakisaidia  kutoa maiti  kutoka katika  basi la Lupondije Express namba T 798 AKV kutoka Mwanza - Iringa baada ya  kupinduka  eneo la Mteremko wa Ipogolo mjini Iringa. 


 NA RAYMOND MINJA IRINGA
Watu sita wamefariki dunia  na wengine zaidi ya 38 kujeruhiwa na kulazwa kwenye hospitali ya rufaa mkoa wa Iringa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Iringa kupinduka kwenye mlima Ipogolo uliopo Manispaa ya Iringa.

Mganga mkuu wa mkoa wa Iringa Robert Salim alisema waliokufa kwenye ajali hiyo ni sita ambapo wawili kati ya hao walifariki wakiendelea kupata matibabu kwenye hospitali hiyo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Peter Kakamba alisema ajali hiyo ilitokea jana (juzi) saa 3:30 usiku baada ya basi la Lupondije aina ya Scania lenye namba za usajili T798AKV mali ya Lupondije Express Kutoka  Mwanza kuja  Iringa  kupinduka  eneo la  Mteremko  wa Ipogolo  mjini Iringa  wakati basi hilo   likielekea  kufaulisha  abiria  wa  Mbeya.


Alisema majeruhi 38 walifikishwa hospitali ya Iringa ambapo 11 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 27 wamelazwa wachache wakiwa mahututi.


Wema  Zuberi  ni  mmoja kati ya majeruhi  wa ajali  hiyo aliyekuwa ametoka mkoani  Dodoma  kuelekea  Mbeya  aliueleza  kuwa  mwendo  wa basi hilo  toka  amepanda  Dodoma  kuja  Iringa  haukuwa  mkali  sana kwani  ulikuwa ni  mwendo wa kawaida .


Japo  alisema  kuwa   baada ya  kuingia  mjini  Iringa katikati ya mji  ndipo dereva  wa basi   hilo alionyesha  kuendesha basi   hilo kwa mwendo mkali  zaidi  kiasi  cha  baadhi ya  abiria  kulalamika mwendo huo na  kutaka   kushushwa ila dereva  hakuweza  kusikia zaidi ya  kuwapuuza  abiria  hao.


“Abiria  wengi   walionyesha   kumlalamikia   dereva   huyo kwanza kutokana na  kuwapitiliza  stendi pasipo  kuwashusha na pili mwendo kasi ambao  alikuwa  akienda nao   ili  kufanikisha  kutufaulisha abiria  tuliokuwa   tukielekea  Mbeya “


Alisema kabla ya  kufika  eneo  hilo ambalo  basi  lilipinduka kuna kona kali na mteremko  mkali  na kilichoonekana haraka  haraka ni dereva   kushindwa kukata  kona   hiyo baada ya Breki  kufeli   na hivyo  kulazimika  kuhama  njia  na  kugonga kingo za  barabara  hiyo na  kupinduka

RPC Kakamba aliwataja waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo kuwa ni Banenda Helen (45) raia wa Kongo, Mbuyi Leoni (52) raia wa Kongo, Jojina Nyamboko (26) mkazi wa Songea,  Magambo Masunga (51) mkazi wa Mwanza, Felister Mwinuka (19) mkazi wa Njombe, Tubilisiusy Selestine  (33), Said Kitonyi (17), Richard Bett (33) raia wa Kenya na Jofa Abonga
(30)mkazi wa Geita.

Wengine ni Victor Lameck (25), mkazi wa Kagera, Pius Samwel (20) mkazi wa Mara, Michael Hadu (46) mkazi wa Madaba Songea, Hassan Mfaume (20) mkazi wa Iringa, Heriet Mwitinda (29) mkazi wa Arusha, Kiliana Kalinga (22) mkazi wa Mbeya, Hima Kifyasi (32) mkazi wa Bariadi, Omary Hassan (35) mkazi wa Makambako, Zuo Pawa (30) mkazi wa Mbeya, Chacha John (26) mkazi wa Iringa.

Wengine Timoth Sichoni (24) mkazi wa Dodoma, Ishimwe Jasmin (9) rais wa Rwanda, Mkagasana Sarafina (41) rais wa Rwanda, Zaina Kisaka (26) mkazi wa Manyara, Sara Sichone (26) mkazi wa Mwanza, Ivon Magaiwa (22)mkazi wa Mafinga, Solomoni Angolisye (58) mkazi wa Dodoma, Ivan
Huwen (33) na mwingine ambaye hajajuliakana jina kutokana na kuwa na hali mbaya.

Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva na kuwa dereva wa basi hilo alikimbia mara baada ya ajali kutokea na kupitia mwajiri wake wanaendelea kumtafuta dereva huyo ili kuja kujibu tuhuma zinazomkabili

Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu  wa  wilaya ya  Iringa  Bw Richard Kasesela alisema  kuwa zoezi la  kuendelea  kutafuta  miili iliyobanwa na basi  hilo imekuwa  ngumu  kutokana na kukosekana  kwa gari la kuinua  basi


Hata   hivyo  mkuu huyo wa wilaya alisema  kuwa kuanzia   sasa  dawa ya  madereva  hao  ni  kuwashughulikia kwa uzembe wanaofanya  kwani kama Rai imekwisha   tolewa  mara  nyingilakini   bado  ajali zinaendelea   kutokea

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More