Thursday, March 31, 2016

Rais Magufuli Azungumzia Uteuzi wa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi

Rais John Magufuli amewatoa hofu wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuhusu uteuzi wao kwa kuwataka kuchapa kazi kwa bidii ili wawe na nafasi nzuri ya kuteuliwa badala ya kufanya kazi kwa wasiwasi jambo ambalo matokeo yake yatakuwa kuondolewa.

Dk Magufuli alitoa kauli hiyo juzi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Chato mara baada ya kutua kwa helikopta akitokea Mwanza kuelekea nyumbani kwake Kijiji cha Rubambangwe kwa mapumziko.

Akiwahutubia mamia ya wananchi waliokuwa wamefurika uwanjani hapo, Dk Magufuli alisema anatambua kuwa bado hajachagua wakuu wa wilaya na wakurugenzi hali ambayo imewafanya baadhi yao kuwa na wasiwasi na kushindwa kutekeleza majukumu inavyotakiwa.

“Kama wewe ni mchapakazi mkuu wa wilaya, mkurugenzi una wasiwasi gani? Tena unapokuwa na wasiwasi ndivyo uwezekano wa kung’olewa unakuwa mkubwa,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na kuongeza:

“Lazima niwaambie waheshimiwa wakuu wa wilaya, ukiwa na wasiwasi hutafanya kazi na sisi tunakuona tu unafanya kazi kwa wasiwasi utaondoka tu kwani wasiwasi ni dalili nzuri ya kukufanya uondoke.”

Aliwatoa hofu akisema hata watakaoondolewa kwenye nafasi hizo watapangiwa kazi nyingine lakini akawaambia kwamba hata kama wataondolewa wasihofu kwani haitakuwa mbaya kwa kuwa hawakuzaliwa na ukurugenzi au ukuu wa wilaya.

Alisema Watanzania wanatakiwa kumwamini na kurudia kauli yake kwamba hatawaangusha akiahidi kuondoa kero ambazo zimegeuka mzigo kwa wananchi.

“Wako wengine walianza kulalamika natumbua mno majipu, siyo kutumbua tu ikiwezekana kuna mengine nitayakata kabisa na mguu wake, Tanzania lazima iwe yenye neema, haiwezekani kuwa na wafanyakazi 5,000 wanaolipwa mishahara mikubwa halafu Watanzania milioni 50 wanalia… nitakwenda kujibu nini kwa Mungu,” alisema.

Alisema ataendelea kuwatumbua (kuwawajibisha viongozi wazembe) hata kama wanafika 50,000 ilimradi Watanzania milioni 50 wapate neema ya kufaidika na rasilimali yao.

Alisema watu katika nchi hii wanaishi bila raha na kuwaahidi kuwa itapatikana kwa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii hasa vijana na kuacha tabia ya kucheza pool huku mama zao wakienda shambani kulima na kusubiri kula tu.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More