Monday, March 28, 2016

AJALI YA BASI LA LUPONDIJE EXPRESS KUTOKA MWANZA - IRINGA YAUA HAPA MKOANI IRINGA

 Askari   polisi na  wasamaria  wema  wakisaidia  kutoa maiti  kutoka katika  basi la Lupondije Express namba T 798 AKV kutoka Mwanza - Iringa baada ya  kupinduka  eneo la Mteremko wa Ipogolo mjini Iringa.
 Gari la kikosi  cha  Zimamoto na uokoaji  likiwa  eneo la  tukio  kusaidia  kuokoa maisha ya majeruhi



 Mkuu  wa  wilaya ya  Iringa Bw  Richard  Kasesela   kushoto  akiwa na kamanda wa  polisi mkoa  wa Iringa Bw Peter Kakamba  wakisaidia  kuokoa  majeruhi na kutoa maiti


WATU  zaidi ya   wane  wakufa  papo  hapo na  wengine  zaidi ya 20 kujeruhiwa  vibaya  baada  ya  basi lenye  namba  za  usajili    T 798 AKV mali ya Lupondije Express Kutoka  Mwanza kuja  Iringa  kupinduka  eneo la  Mteremko  wa Ipogolo  mjini  Iringa  wakati basi hilo   likielekea  kufaulisha  abiria  wa  Mbeya.


Imeelezwa   kuwa baadhi ya  abiria    waliokufa  katika  ajali   hiyo na  majeruhi   ni  wale ambao   walitakiwa   kushuka stendi kuu ya mabasi  ya mabasi  yaendaye  mikoani mjini Iringa ila dereva  wa basi aligoma   kuwashusha  stendi na  kupitiliza nao  kwenda Ipogolo    kufaulisha abiria  wa Mbeya  kwanza  ndipo arudi   kuwashusha  stendi.


Ajali   hiyo  imetokea  majira ya  saa 2 usiku baada ya  basi  hilo  kufeli  breki katika  mteremko  huo huo mkali kabla ya  kupinduka .


Wema  Zuberi  ni  mmoja kati ya majeruhi  wa ajali  hiyo aliyekuwa ametoka mkoani  Dodoma  kuelekea  Mbeya  aliueleza mtandao  huu  wa matukiodaima Blog   kuwa  mwendo  wa  basi hilo  toka  amepanda  Dodoma  kuja  Iringa  haukuwa  mkali  sana   ulikuwa ni  mwendo wa kawaida .


Japo  alisema  kuwa   baada ya  kuingia  mjini  Iringa katikati ya  mji  ndipo dereva  wa basi   hilo alionyesha  kuendesha basi   hilo kwa mwendo mkali  zaidi  kiasi  cha  baadhi ya  abiria  kulalamika mwendo huo na  kutaka   kushushwa ila dereva  hakuweza  kusikia zaidi ya  kuwapuuza  abiria  hao.


“Abiria  wengi   walionyesha   kumlalamikia   dereva   huyo kwanza  kutokana na  kuwapitiliza  stendi pasipo  kuwashusha na pili mwendo  kasi ambao  alikuwa  akienda nao   ili  kufanikisha  kutufaulisha abiria  tuliokuwa   tukielekea  Mbeya “


Alisema kabla ya  kufika  eneo  hilo ambalo  basi  lilipinduka kuna kona kali na mteremko  mkali  na kilichoonekana haraka  haraka ni  dereva   kushindwa kukata  kona   hiyo baada ya Breki  kufeli   na   hivyo  kulazimika  kuhama  njia  na  kugonga kingo za  barabara  hiyo na  kupinduka .


Mkuu  wa  wilaya ya  Iringa  Bw  Richard Kasesela akizungumza na  mwandishi  wa  habari  hizi eneo la   tukio alisema  kuwa zoezi la  kuendelea  kutafuta  miili  iliyobanwa na basi  hilo imekuwa  ngumu  kutokana na kukosekana  kwa gari la kuinua  basi hilo na  tayari  amemwagiza  meneja  wa Tanesco kuleta  gari  hilo na  iwapo  dereva   hayupo  basi kuamka  na  kuendesha  mwenyewe .


Hata   hivyo  alisema  kuwa kuanzia   sasa  dawa  ya  madereva  hao  ni  kuwashughulikia kwani kama Rai imekwisha   tolewa  mara  nyingi na  bado  ajali  zinaendelea   kutokea.


Kamanda   wa  polisi  wa mkoa  wa Iringa  Bw  Peter Kakamba  ambae  pia  alikuwepo  eneo la  tukio kusaidia  kuokoa majeruhi na kutoa maiti katika basi hilo  pamoja na mkuu  huyo  wa  wilaya wananchi  mbali mbali walioongozwa na askari  polisi ,alisema  kuwa hadi majira  ya saa 5 usiku wakati tunakwenda mitamboni bado ilikuwa ni  mapema  kuweza kujua  ni  watu  wangapi    wamepoteza maisha  kwani  zoezi  lilikuwa  bado  linaendelea.



Kamanda huyo aliahidi  kutoa  taarifa mara  tu zoezi hilo  litakapokamilika kwa kuinua  basi hilo na kutazama kwa  kina kama kuna  miili ambayo  imefunikwa   chini ama lah.


Mwandishi  wa habari  hizi  alishuhudia  miili  minne ikiwa tayari  imetolewa katika basi hilo huku majeruhi   wengi  wakiwa   wamepata majeraha  makubwa  mikononi ,miguuni na kichwani,Majeruhi  wa ajali   hiyo wamelazwa Hospitali ya  Rufaa ya  mkoa  wa Iringa 

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More