Friday, March 25, 2016

Kamati ya Bunge yashindwa kujadili Deni la taifa

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeshindwa kujadili Deni la Taifa na kuagiza kukutana na idara na taasisi sita, zinazohusika na deni hilo.

Uamuzi huo wa kamati ulifikiwa jana jijini Dar es Salaam wakati Kamati hiyo ilipokutana na Wizara ya Fedha na Mipango, kujadili taarifa yao ya fedha kwa mafungu tofauti.

Idara na taasisi hizo ni Idara ya fedha za Nje, Idara ya Sera na Uchambuzi, Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tume ya Mipango na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akitoa uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hillary, alisema kamati hiyo haiwezi kujadili na Wizara ya Fedha, Deni la Taifa kama ambavyo linaonesha katika kifungu kinachotakiwa kujadiliwa, kwa sababu, wizara hiyo inaelekezwa kulipa tu.

“Tumeshindwa kujadili Deni la Taifa na Wizara ya Fedha leo (jana), hawa wanapokea maelezo ya kulipa tu, hawajui vyanzo vya madeni vimetokea wapi, sasa tumeona tukutane kwanza na hizo idara na taasisi husika watuambie chanzo na deni likoje,” alisema Hillary.

Alisema idara hizo na taasisi zitaandikiwa barua ili wanapokutana na kamati waje na maelezo yanayojitosheleza kuhusu deni hilo la taifa ili baada ya kamati kuhoji na kuelewa, ndipo wakutane na wizara kuendelea na mjadala.

Awali wakati kamati hiyo ikijadili na wizara hiyo kuhusu ripoti yake ya hesabu, wajumbe wa kamati hiyo walihoji kero ya wastaafu ya kucheleweshewa malipo yao ya pensheni na mirathi.

Akichangia mjadala huo, Mjumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Abdallah alihoji ucheleweshaji wa malipo kwa wastaafu kutoka Hazina na kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Alisema wastaafu wengi wakiwemo walimu wamekuwa wakisumbuliwa kupeleka barua za ajira na hati za malipo ya mshahara kwa mwezi, jambo ambalo ni kero na wakati mwingine wastaafu hao huwa wamepoteza kumbukumbu hizo kwa kuwa ni za muda mrefu, jambo ambalo linawafanya wacheleweshewe stahiki zao.

Akijibu hoja hizo na nyingine, Mhasibu Mkuu wa Serikali, Francis Mwakapalila aliomba radhi kwa wastaafu wote ambao wamekuwa wakisumbuliwa kupeleka vielelezo hivyo na kusisitiza kwamba ni wajibu wa mwajiri kuwa na vielelezo vya watumishi wake.

Mwakapalila alisema hivi sasa utaratibu unaotumika kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina hauna usumbufu na kwamba mirathi na pensheni zinazolipwa na Hazina huenda moja kwa moja kwenye akaunti za wahusika na hazipitii tena Hazina Ndogo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More