Thursday, March 3, 2016

Zuio la Uchaguzi Meya wa Dar Lageuka Kaa la Moto.

Baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kulikana zuio llilotumika kuahirisha uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, suala hilo limekuwa sawa na kaa la moto na hakuna mtu anayetaka kulishika.
Jana Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando, ambaye alikuwa mwenyekiti wa uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Jumamosi iliyopita,  jana alisema hajui lilikotoka zuio hilo kwa  kuwa alipewa tu na wanasheria wa jiji ili alisome kama lilivyo.

“Baada ya kufika eneo la tukio (kwenye ukumbi wa Karimjee), nilikabidhiwa zuio hilo nilisome. Suala la kujua kama limeisha muda wake au la naomba uwasiliane na mwanasheria wa jiji au mwanasheria wa mkoa, wao ndio walikuwa nalo na hata nilivyopoteza vitu vyangu vingine, hilo (zuio) wao wanalo,” alisema Mmbando.

Baada ya kutimiza wajibu wake, kama alivyotakiwa na wanasheria hao, alisema ndipo zilipozuka vurugu na yeye kupoteza nyaraka zake ikiwa pamoja na ajenda na miongozo ya kikao hicho.

Kwa upande wake, Mwanasheria wa Jiji la Dar es Salaam, Jackline Mosha, alisema hakupitia tamko hilo kabla ya kumpa aliyekuwa mwenyekiti wa uchaguzi huo na kwamba alilikuta kwenye ukumbi huo bila kujua limetoka wapi.

Alisema walijua kuna zuio hilo baada ya kufika katika viwanja vya Karimjee siku hiyo ya uchaguzi.

“Zuio lilitoka Februari 5, sisi tulijua siku ya tukio, tulimkabidhi mwenyekiti Mmbando alisome, hatukufahamu kama limeisha muda wake.

“Hatukupata muda wa kulipitia na kujiridhisha kwa sababu haikuwa siku ya kazi kwa mahakama. Hata hivyo zuio hili hatukupewa mapema, wangetupa mapema tungejiridhisha na yote hayo tungeyajua kabla ya siku ile,” alisema.

Kuhusu madai kuwa walitumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya hivyo, alisema wao ni wanasheria na kwamba wanafanya kazi kitaalamu.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, amesema kuwa tayari ameagiza apelekewe taarifa rasmi na Theresia Mmbando, ili kubaini ukweli kuhusu zuio hilo kama lilikuwa la kweli au la.

Waziri Simbachawene alitoa kauli hiyo juzi na kusisitiza kuwa kwa wakati huo hakuwa na taarifa zinazothibitisha  zuio la kuahirishwa kwa uchaguzi huo lililosomwa na Mmbando kama ni la kweli au la.

“Kwa sasa kama wizara hatuna cha kusema kuhusiana na tukio zima lililitokea siku ile. Kama mnavyojua Katibu Tawala alipigwa anaumwa, yeye ndiye aliyesoma zuio hilo hivyo tunasubiri apone atuandalie taarifa kamili,” alisema na kuongeza:

“Kama Waziri sijapokea taarifa zozote zinazosema zuio hilo lilikuwa halali au la. Tusubiri kwanza atuandikie hiyo taarifa yake ili tufanye ulinganisho ndipo wizara itapata cha kusema,” alisema.

Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika kwanza Desemba, mwaka jana, ukapangwa kufanyika Januari 23, mwaka huu lakini na baadaye kupangwa kuwa Februari 8.

Februari 8, mwaka huu, madiwani baada ya kufika viwanja vya Karimjee kwa ajili ya uchaguzi, walikabidhiwa barua ambazo hazikueleza sababu za kuahirishwa kwake bali utafanyika utakapopangwa tena na ndipo ulipopangwa kufanyika Jumamosi iliyopita.

Jumatatu wiki hii, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Warialwande Lema, alikanusha taarifa kwamba   mahakama hiyo imetoa zuio la uchaguzi huo.

“Mahakama ilitoa amri ya zuio la muda Februari 5, mwaka huu la kuzuia uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 8 na ilipanga kusikiliza maombi hayo Februari 15 lakini walalamikaji hawakufika mahakamani,” alisema na kuongeza:

“Mahakama ilipanga tena maombi hayo kusikilizwa Februari 23, mwaka huu, lakini pia walalamikaji hawakutokea mahakamani.”

Walalamikaji katika shauri hilo walikuwa Susan Massawe na Saad Khimji, dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.

Akiendelea kufafanua, Hakimu Lema alisema baada ya walalamikaji kushindwa kufika, mahakama iliondoa maombi ya zuio yaliyokuwa yamewasilishwa  mbele yake na walalamikaji pamoja na zuio lililokuwa limetolewa awali.

“Aliyesema mahakama imetoa zuio ni uongo kwa kuwa walitumia amri ambayo ilipitwa na wakati. Sijui chochote kuhusu zuio la Februari 27, mwaka huu,” alisema Hakimu Lema.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Cyprian Mkeha, alisema baada ya maombi hayo kuondolewa mahakamani, hajapokea maombi mengine kuhusu kuzuia uchaguzi huo

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More